Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-23 19:08:54    
Barua 0121

cri
 Msikilizaji wetu Kaziro Dutwa wa sanduku la posta 209 Songea Ruvuma Tanzania ametuletea barua akisema, anafurahi sana kupata fursa hii ya kuweza kuandika waraka huu akiwa na matumaini makubwa kuwa sisi sote wazima wa afya na neema tele, kama ndivyo basi hii ni furaha kubwa sana kwake, anasema yeye hali yake ni njema na ya kuridhisha kabisa.

Anasema tangu mwezi wa Machi mwaka 2006 alikuwa safari ya kikazi katika kutimiza sehemu ya majukumu yake ya kila siku kama mlinzi wa amani, safari hii jukumu lake lilikuwa kuwasaidia ndugu zake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili waweze kumchagua rais wao kidemokrasia. Kutokana majaliwa ya Mungu na baraka zake, wameweza kuwasaidia wananchi wa Kongo Kinshasa kumchagua kiongozi wanayemridhia, na hatimaye akaapishwa salama salimini, hakika hali hiyo ni ya kujivunia.

Bwana Dutwa anasema pamoja na majukumu mazito aliyokuwa nayo pia aliweza kuisikiliza Radio China kimataifa mara alipopata wasaa kwani sehemu zote alizokuwa CRI inasikika vizuri sehemu hizi ni Kalemie, Goma na Lubumbashi. Aliweza kusikiliza shindano zuri na moto moto la Mimi na Radio China kimataifa tangu lianze hadi mshindi Bw. Franz Manco Ngogo alipotangazwa kuwa mshindi maalum akaalikwa kuitembelea China akiwa mgeni wa Radio China kimataifa, Bwana Dutwa anasema anachukua fursa hii kumpongeza Bw. Ngogo na washindi wengine, na vilevile washiriki wote anawaomba waendelee na moyo huo huo wa kutokata tamaa waelewe kuwa donoadonoa ya kuku humfanya ashibe.

Bwana Dutwa anasema kati ya vitu vingi vilivyomfanya afurahi sana siku alipotangaziwa amri ya kurudi nyumbani mojawapo ni CRI kwani alitegemea mara tu atakapotia mguu wake nyumbani basi atajiliwaza kwa kufungua barua na vifurushi alivyokuwa ametumiwa kama zawadi na kumbukumbu kutoka kwa Radio China kimataifa, lakini alipofika nyumbani na kuuliza iwapo kuna barua au kifurushi chochote toka Radio China kimataifa, kwa mshangao hakukuwa na barua wala kifurushi chochote, hii ilimsikitisha sana na hadi leo bado ana majonzi.

Anasema mara nyingi amewahi kumsikia mama Chen anapokuwa akijibu barua za wasikilizaji mbalimbali akisema kuwa kwa sasa wako na pilikapilika nyingi sana hapo Radio China kimataifa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka sana kwa wasikilizaji na upungufu wa nguvu kazi, haya majibu ni ya kimantiki na yamemfanya afarijike na badala ya kutulaumu, basi analazimika kutupa pole kwa kazi nzito tulizo nazo katika juhudi zetu kwenye kuboresha vipindi na radio hii kwa ujumla. Pamoja na haya yeye alipokuwa safari mambo mengi yalifanywa na viongozi wakuu wa Jamhuri ya watu wa China kwa kuwa alikuwa anapata fursa ndogo sana kusikiliza Radio China kimataifa, alitegemea siku akirudi nyumbani atakuta majarida kadhaa yakielezea matukio mbalimbali yaliyopita, lakini wapi, alinoa patupu! Haya basi yaliyopita si nywele tugange yajayo. Anawapa shukurani za pekee wasikilizaji wenzake waliokuwa wakimsalimia kupitia Radio China kimataifa wakati yeye hakuwepo nyumbani hakika salamu zao zilikuwa zikimpa moyo sana na kumfanya ajisikie yuko nyumbani japo kuwa alikuwa kwenye nchi isiyo yake na yenye mazingira ya kivita, hivyo hadi sasa anawashukuru sana na hawa wasikilizaji waliomsalimia, japo kulingana na mazingira aliyokuwepo hakuweza kuyaandika majina yao kwani kuna muda ilikuwa inambidi kuishi sehemu ambayo mwanga wa aina yoyote hauruhusiwi hata hivyo baadhi ya wale anaowakumbuka ataendelea kusalimiana nao bila matatizo mara tu atakapopata kadi za salamu toka Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Dutwa kwa barua yake ambayo imetupa picha kuhusu alipotekeleza jukumu lake katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, kwa kweli yeye anastahili kusifiwa kuwa ni shujaa wa kujitolea ambaye alichangia kuwasaidia wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kukamilisha uchaguzi wa rais. Siku nyingi Bwana Dutwa alikuwa hajatutumia barua, kumbe ni kutokana na kuwa na kazi kubwa. Tunamshukuru sana kwa juhudi zake za kusikiliza Radio China kimataifa, hata alipokuwa kazini akipata nafasi alisikiliza mara kwa mara matangazo yetu na kupata mengi tuliyotangaza. Na tunashukuru kwa kutujulisha kuwa kwenye miji mbalimbali kule nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama vile Kalemie, Goma na Lubumbashi, matangazo yetu yanapatikana vizuri. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Msikilizaji wetu Rose Nyakundi wa Mecheo shule ya upili sanduku la posta 469, Keroka Kenya ametuandikia barua ambayo kwanza inaanza kwa salamu, anasema ana furaha isiyo kifani kupata fursa hii ya kutoa maoni kuhusu idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Kabla hajatoa maoni pamoja na mapendekezo yake, angependa kutushuruku kwa zawadi zetu za kadi tulizomtumia ambazo zimemfurahisaha sana.

La kwanza ni la muhimu, anasema angependa kutujulisha kuwa huko anakoishi, hakuna mawasiliano ya internet, kwa hiyo anatushauri kuwa kama Radio China Kimataifa ingeweza, ingekuwa vizuri kama ingekuwa na kituo cha mtandao wa internet karibu na kijiji anachoishi au karibu na mji wa karibu. Hii ndio maana hajawahi kutembelea tovuti za Radio China kimataifa. Na kuhusu habari zinazotolewa na Radio China kimataifa zinazoihusu China, anaweza kusema kuwa ni sawasawa. Lakini angependelea zaidi kama hizo habari zingekuwa zinakamilika zaidi. Kwa mfano, kama tunatangaza kuhusu tukio fulani, ni vizuri tukio lenyewe lichambuliwe kwa kina na urefu na tulifuatilie, ili wasikilizaji waweze kuielewa kwa undani.

Pia anasema anaridhishwa na utaratibu wa vipindi vya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Kwani utaratibu wa muziki huenda sambamba na wakati. Pia utoaji wa habari kuhusu yaliyojiri huenda na wakati mwafaka. Maoni ya mwisho yanahusu kipindi anachopenda zaidi. Kipindi cha Burudani za muziki, ni kipindi kinachoongoa na kuliwaza kweli kweli. Basi wakati wa kipindi hicho, mtangazaji ajulishe wasikilizaji ni kundi gani la wanamuziki ambao wametoa burudani hiyo, na kuzungumzia muziki wenyewe, kabla au baada ya kusikika, haoni kama ni vizuri kuongea katikati ya muziki..

Tunamshukuru kwa dhati kuhusu maoni na mapendekezo yake, kuanzia tarehe 27 Februari mwaka huu tutafanya mpangilio mpya kuhusu vipindi vyetu, na tutatilia maanani maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wetu ili kuboresha vipindi vyetu.

Na msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu ametuletea barua akisema kuwa, mnamo tarehe 9 mwezi Desemba mwaka 2006, ujumbe wa Radio China kimataifa ulifika mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu kwa siku moja ukielekea katika Mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania. Miongoni mwa wajumbe hao alikuwemo Mama Chen mtangazaji mashuhuri na wa muda mrefu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ambaye baada ya kuwasiliana naye kwa njia ya simu alipata fursa ya kuonana naye uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa pamoja na kufanya naye mazungumzo kwa karibu saa nzima.

Bwana Msabaha anasema, kwa kweli jambo la kufurahisha mno kwake yeye juu ya kupata fursa hiyo adhimu, ambayo hakutegemea kama itatokea. Anasema aligundua kuwa Mama Chen ni mtu mcheshi, mchangamfu na mwenye kupenda watu. Anasema kuwa ni kutokana na sababu hiyo, yeye na wasikilizaji wengine waliingiwa na wasiwasi baada ya kusikia kuwa atastaafu.

Hapa tunapenda kuwaletea wasikilizaji wetu habari ya kufurahisha, Radio China kimataifa imeahirisha kustaafu kwa Mama Chen mpaka mwaka kesho, kwa hiyo ataendelea kuchapa kazi kwa ajili ya wasikilizaji. Lakini hata hivyo hata kama akistaafu mwaka kesho, ataendelea kuwasaidia vijana wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa na kutoa mchango wake, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Sasa tunapenda kuwaletea rekodi kuhusu mazungumzo kati ya Mama Chen na msikilizaji wetu Mbarouk Msabah, huko Dubai.

Idhaa ya Kiswahili 2007-01-23