Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-24 17:57:20    
China yafanya juhudi kusukuma mbele usawa katika kupata elimu

cri

Hivi sasa wanafunzi wengi zaidi wanaoishi katika sehemu zilizoko mbali na miji wanaweza kusikiliza mihadhara inayotolewa na wahadhiri maarufu kwa mtandao wa elimu kwa mawasiliano ya mbali; wanafunzi kutoka familia zenye matatizo ya kiuchumi wanaweza kupata elimu ya msingi na ya sekondari ya chini kwa kulipa ada ya vitabu tu. Katika miaka ya karibuni, mabadiliko yaliyotokea katika shule za China yanaonesha kuwa, idara za elimu za China zinafanya juhudi kusukuma mbele usawa katika kupata elimu.

Bibi Sun Qiaoyun ni mkulima wa mkoa wa Ningxia ulioko kaskazini magharibi mwa China, hivi sasa mtoto wake anasoma katika shule ya sekondari. Bibi Sun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kutokana na matatizo ya kiuchumi aliwahi kumtaka mtoto wake aache masomo.

"Zamani ilinibidi nilipe yuan 120 kwa karo na ada nyingine mbalimbali katika kila muhala wa masomo. Familia yangu ilikubwa na matatizo ni maskini, hatuwezi kumudu ada hizo. Baadaye niliambiwa kuwa hatuna haja ya kulipa ada hizo tena, na walimu walimtaka mtoto wangu arudi shuleni."

Sera hiyo mpya inayowafurahisha Bibi Sun Qiaoyun na mtoto wake ilianza kutekelezwa katika majira ya spring mwaka jana. Serikali imefuta karo na ada nyingine mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ya chini katika vijiji vya sehemu za magharibi ambazo ziko nyuma kiuchumi. Sera hiyo inawanufaisha wanafunzi zaidi ya milioni 50 vijijini. Ada za masomo yuan mia 1 hadi mia 2 si kubwa kwa familia tajiri, lakini kwa familia zenye matatizo ya kiuchumi huo ni mzigo mkubwa. Mwaka huu sera hiyo itatekelezwa kwenye sehemu nyingi zaidi ili kuwanufaisha wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari ya chini vijijini nchini kote. China inatekeleza sera ya elimu ya lazima ya miaka 9, hivyo sera hiyo mpya inamaanisha kuwa wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na sekondari ya chini vijijini hawana haja ya kulipa karo na ada nyingine mbalimbali.

Lakini katika hali ambayo maendeleo ya miji na ya vijiji hayana uwiano, kumwezesha kila mtu apate elimu nzuri kwa usawa si jambo rahisi. Kikao cha 6 cha mkutano wa 16 wa Chama cha Kikomunisti cha China kilichofanyika hivi karibuni kiliweka shabaha ya kujenga jamii yenye masikilizano. Kuhakikisha raia wanapata elimu kwa usawa ni sehemu kubwa ya lengo hilo. Serikali ya China itafanya juhudi kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya elimu ambazo zitafikia asilimia 4 ya thamani ya uzalishaji wa taifa. Waziri wa elimu wa China Bw. Zhou Ji alisema, fedha nyingi zitatumiwa vijijini ili kuwapatia watoto wa vijijini mazingira mazuri ya kupata elimu.

"China itatenga fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya elimu. Fedha nyingi zitatumiwa vijijini. Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2010, China itaongeza yuan bilioni 200 kwa ajili ya elimu ya lazima vijijini."

Hivi sasa idara husika za sehemu mbalimbali nchini China inafanya juhudi kutumia fedha hizo kwa mujibu wa hali ya huko. Kwa mfano mkoani Ningxia, kwenye msingi wa kufuta karo na ada nyingine mbalimbali kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na sekondari ya chini vijijini, mkoa huo pia umewapatia wanafunzi laki 5.3 wa familia zenye matatizo ya kiuchumi vitabu bure, na kutoa msaada wa fedha kwa wanfunzi kutoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi elfu 70 wanaokaa shuleni.

Licha ya kufuta karo na ada nyingine mbalimbali, serikali ya China pia imechukua hatua kuinua kiwango cha elimu vijijini, yaani kuweka nafasi maalum za walimu katika shule za vijijini vilivyoko magharibi mwa China, ili kuwahimiza wanafunzi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu waende kwenye sehemu hizo kufundisha. Kwa mujibu wa takimwu zisizokamilika, hivi sasa wanafunzi wapatao elfu 20 wamekwenda kufanya kazi katika shule zaidi ya 2800 za sehemu za magharibi. Jambo hilo litabadilisha hali ya upungufu wa walimu katika shule za vijijini za sehemu za magharibi na kuinua kiwango cha elimu. Wakati huo huo, sehemu mbalimbali zimechagua walimu wengi hodari kwenda kufanya kazi katika shule za vijijini.

Hivi sasa China imetumia yuan bilioni 8 kwa ujenzi wa mtandao wa elimu kwa mawasiliano ya kompyuta, na asilimia 80 ya shule za vijijini zina uwezo wa kuwafundisha wanafunzi kwa njia hiyo. Shule ya Matumaini ya Nanqiao katika kijiji cha Leixi mkoani Jiangxi ni moja ya shule hizo. Mwalimu Huang Yanqun alieleza kuwa, wanafunzi wanaweza kusikiliza mihadhara ya walimu hodari wa Beijing kupitia mtandao huo. Zamani hili lilikuwa ni jambo lisilowezekana.

"Zamani hali ya shule za vijijini ilikuwa duni. Wazee wengi waliwapeleka watoto wao kusoma mijini. Baada ya mtandao wa elimu kwa mawasiliano ya kompyuta kuanzishwa, hali ya shule za vijijini imekubwa karibu sawa na ya shule za mijini, watoto wengi wamerudi kusoma vijijini."

     

Kwa mujibu wa mpango, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kila shule ya msingi na shule ya sekondari vijijini itakuwa na uwezo wa kupokea vipindi vya televisheni kupitia satelite, na kila shule ya sekondari itakuwa na darasa la kompyuta.

Kuhusu elimu ya sekondari ya juu, elimu ya ufundi wa kazi na elimu ya juu, ambazo si elimu za lazima, serikali ya China pia imechukua hatua nyingi kuwasaidia wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi. Hii imeonesha nia ya serikali ya China ya kusukuma mbele usawa katika kupata elimu. Katika miaka ya karibuni, China kimsingi imeanzisha utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi, ikiwemo kutoa msaada wa masomo, mikopo, msaada maalum kwa wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi, na kupunguza au kufuta karo kwa wanafunzi hao. Idara za elimu za China zimevitaka vyuo vikuu viwasaidie wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi kuingia vyuoni kwanza, baadaye kuwapatia msaada kwa mujibu wa hali zao, ili kuhakikisha kila mwanafunzi anaweza kuanza masomo chuoni. Kwa mujibu wa takwimu, idara husika za China zimewapatia wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi milioni 2 na laki 4 wa vyuo vikuu mikopo ya masomo yuan bilioni 20. Bw. He Zan anayesoma katika Chuo Kikuu cha Renmin ni mmoja kati ya wanafunzi hao, alisema,

"Natoka kwenye kijiji kidogo mkoani Henan. Kwa familia ambayo mapato ya kila mwezi ni yuan mia kadhaa tu, kulipa karo ya yuan elfu 4 hadi elfu 5 kwa mwaka ni jambo lisilowezekana. Lakini serikali imenipatia mikopo ya masomo, sina wasiwasi kuhusu karo, naweza kusoma vizuri."

Licha ya hayo kanuni zinazotekelezwa kwa muda kuhusu usimamizi wa fedha za mdhamini wa masomo wa taifa kwa wanafunzi wa shule za mafunzo ya ufundi wa kazi ambazo zilitolewa mwaka jana zimetunga mpango wa kimsingi kwa utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi wanaosoma katika shule za mafunzo ya ufundi wa kazi. Ofisa anayehusika wa wizara ya elimu ya China alieleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2010, serikali ya China itatenga yuan bilioni 4 kuwasaidia wanafunzi na familia zenye matatizo ya kiuchumi kupata mafunzo ya ufundi wa kazi. Kuanzia majira ya autumn ya mwaka jana, shule nyingi za ufundi wa kazi katika sehemu mbalimbali za China zimeanzisha majaribio kuwa wanafunzi wanasoma shuleni wakifanya kazi. Utaratibu huo umewawezesha wanafunzi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi wasome na kujifunza ufundi.

Lakini kutokana na hali ya kutokuwa na uwiano wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika sehemu mbalimbali nchini China, hali za shule za mijini na vijijni bado zina tofauti kubwa, na wanafunzi bado hawawezi kupata elimu sawa sawa, kazi ya kusukuma mbele usawa katika kupata elimu bado ni gumu. Waziri wa elimu wa China Bw. Zhou Ji alisema katika siku za usoni China itaendelea kuweka mkazo katika kusukuma mbele usawa katika kupata elimu, na maendeleo endelevu ya sekta ya elimu.

Idhaa ya Kiswahili 2007-01-24