Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-24 20:25:56    
Kwa nini Israel inataka kujiunga na NATO?

cri

Gazeti la Israel Jerusalem Post tarehe 23 lilichapisha makala ikisema, serikali ya Israel inatunga mpango wa kujiunga na Jumuiya ya NATO. Hii ni hatua nyingine muhimu ya Israel kufuatia nchi hiyo kueleza wazi nia yake ya kujiunga na NATO mwezi Februari mwaka jana.

Katika kipindi kirefu Israel ilikuwa ina uhusiano wa karibu na NATO. Katika miaka ya hivi karibuni, Israel imekuwa inaimarisha uhusiano kati yake na NATO katika mapambano dhidi ya ugaidi na shughuli za usalama. Zaidi ya hayo Israel ikishirikisha na nchi wanachama wa NATO, zilifanya luteka kadhaa za kijeshi, na jumuiya hiyo inaichukulia Israel kuwa nchi ya kuzungumza nayo katika eneo la bahari ya Mediterranean, hata hivyo Israel hairidhiki na hadhi hiyo. Mwezi Februari mwaka 2006, waziri wa ulinzi wa Israel kwa mara ya kwanza alihudhuria mkutano usio rasmi wa mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya NATO, na balozi wa Israel nchini Ujerumani alieleza wazi kuwa Israel inataka kuimarisha uhusiano kati yake na NATO na kujiunga na jumuiya hiyo katika wakati unaofaa. Sasa serikali ya Israel imeanza kutunga mpango halisi wa kujiunga na NATO.

Je, ni kwa nini Israel ina hamu ya kujiunga na NATO? Wachambuzi wanasema hivi sasa hali ya Mashariki ya Kati inaelekea kuwa mbaya, Israel ikijiunga na NATO, jumuiya hiyo itaweza kuilinda Israel dhidi ya "tishio la Iran" kama Israel inavyoeleza. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran iliwahi kusema mara kadhaa kwamba, anataka Israel ifutwe kutoka kwenye ramani ya dunia. Mbali na hayo Iran haijabadili msimamo wake wa ukaidi kuhusu suala la nyuklia. Kutokana na hali hiyo, kama Israel itakuwa nchi mwanachama wa NATO, kwa mujibu wa mapatano ya ulinzi wa ushirikiano ya jumuiya hiyo, endapo Israel itashambuliwa itasaidiwa na nchi nyingine wanachama jumuiya hiyo, msaada huo ni pamoja na wa kijeshi.

Aidha Israel ikijiunga na NATO, itaweza kutumia nguvu ya ushawishi ya NATO katika kuinua hadhi yake katika eneo la Mashariki ya Kati na kupata manufaa zaidi katika masuala mbalimbali kama vile uhusiano kati ya Israel na Palestina. Kuanzia mwaka jana Israel ilikabiliwa na vitendo vya uhasama kutoka makundi mawili, kundi la Hamas la Palestina ambalo linakataa kuitambua nchi ya Israel wala kutokubali kuacha matumizi ya mabavu, na kundi la Hezbollah la Lebanon ambalo siku zote linashikilia uhasama dhidi ya Israel. Israel ilifanya operesheni mbili kubwa za kijeshi dhidi ya makundi hayo mawili, lakini badala ya kutimiza lengo lililowekwa Israel ilijitumbukiza matatani zaidi na kuyafanya mazungumzo ya amani kati yake na Palestina yaingie kwenye mvutano. Katika hali hii, serikali ya Israel inaona kuwa iwapo Israel itajiunga na NATO, itaweza kufanya shughuli nyingi zaidi za kimataifa kwa kutumia jukwaa la NATO, kwa hiyo itapata manufaa katika mazungumzo na serikali ya mamlaka ya utawala wa Palestina na kutatua matatizo ya uhusiano na nchi jirani.

Kwa upande wa NATO, inazingatia nguvu za jeshi la Israel, nguvu za shughuli za upelelezi na uzoefu katika kupambana na ugaidi, lakini nchi wanachama wa NATO zinatakiwa kufikiria suala moja kabla ya kuipa Israel wanachama wa NATO. Suala hilo ni kwamba karibu nchi zote jirani za Israel zina uhasama na nchi hiyo na ziliwahi kupambana na Israel, NATO ina uwezo wa kutosha wa kufungamana na nchi kama Israel na kuipa msaada wa watu na vitu. Kwa upande wa Israel, hivi sasa hali ya mpaka wake bado haijatulia, haiwezekani kupeleka wanajeshi wake katika sehemu nyingine ikiwemo Afghanistan, kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijeshi zinazoongozwa na NATO. Kwa hiyo kwa sasa ni vigumu kwa Israel kufanikisha lengo la kujiunga na NATO.

Idhaa ya Kiswahili 2007-01-24