Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-25 15:09:36    
Juhudi za kuwasaidia wazee waishi kwa raha mustarehe

cri

China ni nchi yenye watu bilioni 1.3, na ni moja kati ya nchi ambazo idadi ya wazee inaongezeka kwa kasi. Hivi sasa wananchi wa China wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wamefikia watu milioni 144, idadi ambayo ni nusu ya idadi ya wazee wa bara zima la Asia. Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa watu milioni 100. Namna ya kuhakikisha wazee wanaishi kwa raha mustarehe ni suala linalofuatiliwa na jamii ya China.

Wiki iliyopita katika kipindi hiki, tulizungumzia juhudi mbalimbali za kuwatunza wazee zinazofanyika nchini China. Juhudi hizo zinawanufaisha sana wazee katika maisha yao ya kila siku. Hata hivyo Maisha ya raha mustarehe si kama tu yanahusu chakula, bali pia yanahusu afya ya kisaikolojia. Pamoja na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na uzee, wazee pia wanakabiliwa na tatizo la kisaikolojia, hususan wazee ambao waume au wake zao walishafariki dunia, wanasumbuliwa na upweke na hofu ya kifo. Wazee hao wanaonekana kuwa na huzuni, na ni rahisi kukosa matumaini ya kuendelea kuishi. Kwa hiyo katika miaka ya hivi karibuni suala la kuwatunza wazee kisaikolojia limeanza kuzingatiwa katika jamii ya China, ambapo juhudi zimefanywa zikiwa na lengo la kuwasaidia wazee waondokane na upweke unaotokana na kukosa kuwasiliana na jamaa na marafiki.

Katika eneo la kuendeleza uchumi na teknolojia la Taifa, huko Tianjin, mji wa pwani wa kaskazini ya China, kutokana na ushauri wa serikali ya huko, lilianzishwa shirika la wazee ambalo linafanya shughuli mbalimbali za maonesho ya sanaa na michezo kwenye mitaa ya makazi. Hivi sasa shirika hilo lina wanachama zaidi ya elfu moja, na asilimia 95 ya wazee wanaoishi katika eneo hilo wamewahi kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na shirika hilo. Wazee wa huko walieleza kuwa, kila ifikapo siku ya wazee ambayo ni siku ya jadi katika jamii ya China, sherehe kubwa inafanyika katika eneo hilo na kila mwanachama wa shirika la wazee anapewa zawadi ya maua. Shirika hilo la wazee pia lilianzisha vikundi mbalimbali vinavyoshirikisha wazee, vikiwemo vikundi vya baiskeli, mpira wa meza, dansi, wanamitindo wazee, upigaji picha na kwaya.

Mzee Lian Fengchun alijiunga na kikundi cha baiskeli, alieleza kuwa kushiriki kwenye shughuli za michezo na sanaa kunamfanya awe mchangamfu zaidi na kujisikia raha mustarehe. Mzee Lian alisema "Katika eneo la Taida, wazee wanaishi kwa furaha. Siku zote shirika la wazee linatufuatilia sisi wazee. Linatuhamasisha kufanya shughuli mbalimbali kama vile kusafiri kwa baiskeli kuzunguka kando ya bahari ya Bohai. Katika safari hiyo tulionesha jinsi tunavyofurahia maisha ya uzee, vile vile tulishuhudia maendeleo ya sehemu mbalimbali za nchi yetu. Kutokana na shughuli za namna hii, sisi wazee tuna matumaini makubwa zaidi ya maisha."

Pamoja na maendeleo yaliyopatikana katika shughuli za kuwahudumia wazee, serikali ya China imeweka bayana changamoto zinazoikabili katika kutimiza lengo la kuhakikisha wazee wanaishi kwa raha mustarehe. Kuongezeka kwa idadi ya wazee kunaongeza mzigo kwa mfumo wa kuwahudumia wazee. Kwa mujibu wa takwimu, kwa kila wazee elfu moja wa China wana vitanda 10 tu katika vituo vya kuwatunza wazee, huku idadi hiyo ya vitanda ni kati ya 50 na 70 katika nchi zilizoendelea. Asilimia 60 ya wazee wa China wanaishi katika maeneo ya vijiji, ambapo mifumo ya kuwahudumia wazee, matibabu na hifadhi ya jamii bado haijakamilika.

Serikali ya China imetoa ahadi kwamba, itaendelea kutenga fedha zaidi katika hifadhi ya jamii, hatua kwa hatua kukamilisha mfumo wa kuwahudumia wazee unaowanufaisha wananchi wote na unaolingana na maendeleo ya uchumi na jamii ya China, ili wazee ama wanaoishi mijini au vijijini waishi kwa raha mustarehe.

Naibu mkurugenzi wa ofisi ya kamati inayoshughulikia mambo ya wazee ya taifa ya China Bw. Li Bengong alifafanua mpango wa China katika miaka kadhaa ijayo. Alisema "Katika kipindi kati ya mwaka 2006 na 2010, tutatimiza vigezo kadhaa halisi. Kwa mfano tutaongeza vitanda milioni 2.2 katika vituo vya kuwatunza wazee wanaoishi vijijini ambao hawana uwezo wa kufanya kazi na wasio na kipato. Aidha serikali katika ngazi mbalimbali zinatakiwa kuongeza hatua kwa hatua fedha zinazotumika katika ujenzi wa vifaa vinavyowahudumia wazee, elimu ya wazee, utafiti wa sayansi unaohusu wazee, na shughuli mbalimbali zinazowashirikisha wazee. Pia tutahamasisha uwekezaji kutoka kwa watu binafsi na kutoka nje katika mambo yanayohusu wazee, ili kuanzisha utaratibu wa pande mbalimbali kutoa mchango kwa ajili ya kazi hiyo ya kuhakikisha wazee wanaishi kwa raha mustarehe."

Idhaa ya kiswahili 07-01-25