Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-26 17:29:06    
Wachina waishio katika Zanzibar

cri

Katika karne zilizopita, wachina wengi waliondoka nyumbani, wakavuka bahari hadi kufika pwani ya sehemu nyingine ili kutafuta maisha bora. Katika kipindi hiki cha leo tumewaandalia maelezo kuhsu historia ya wachina waishio Unguja na maisha yao yalivyo ya hivi sasa.

Katika miaka ya 20 ya Karne iliyopita, kikundi cha wachina vijana kilifika katika sehemu ya pwani ya Tanzania na Kenya wakipelekwa na kampuni moja ya Hongkong ili kutafuta majongoo wa baharini. Wengine walikwenda Pemba, Lamu, Mombasa na Malindi, vijana 9 walifika Unguja. Hawa vijana baada ya kuishi Unguja kwa miaka kadhaa, waliipenda sana Unguja na kuamua kuweka makazi yao huko.

Baba ya Bi. Chen Lijun alikuwa mmoja kati ya kizazi cha kwanza cha wachina waliofika Unguja, baada ya miaka kadhaa, alirudi China kuoa na kwenda pamoja na mke wake Unguja na wakazaa watoto 7, Bi Chen Lijun

ambaye ni kitindamimba alizaliwa mwaka 1955. Hali kadhalika na familia nyingine, watoto wa kizazi cha pili cha wachina waishio Unguja wamekuwa wengi.

Nyumbani kwa Bi. Chen Lijun kuna picha iliyopigwa mwaka 1968. Japokuwa picha hiyo ni ya zamani, lakini imeonesha hali ya wakati ule ya wachina waliokuwa wakiishi Unguja. Kwenye picha hiyo kuna mkusanyiko wa watu wapatao 35 wa familia tisa walioishi huko Unguja.

Lakini kwa sababu Unguja ni sehemu ndogo, hawawezi kupata elimu ipasavyo, na hakuna nafasi nyingi nzuri za kazi, hivyo watoto wengi baada ya kumaliza shule ya msingi walipelekwa ng'ambo kusoma na kutafuta kazi, na kuishi kule kule. Sasa wengi wamesambaa katika nchi za Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya, na Australia. Kwa mfano Bi. Chen Lijun ana ndugu saba, lakini watano wako nje ya Unguja, ni yeye na ndugu yake mwingine tu walibaki huko.

Bi. Chen Lijun alisema sasa hivi familia yake imekuwa ya kizazi cha nne, mama yake amerudi nchini China, yeye mwenyewe ana watoto watatu, na hata amepata wajukuu, yaani kizazi cha nne. Japokuwa Bi. Chen Lijun na wachina wenzake wameishi ng'ambo kwa miaka mingi, hawajui kusoma wala kuandika lugha ya Kichina, lakini wanatilia maanani sana uhusiano na China. Bi. Chen Lijun alisema karibu kila mwaka yeye na mume wake huwa wanarudi China kuwatembelea jamaa zao, na kutembelea hapa na pale nchini China. Akasema wanafurahi sana kuona maendeleo na mabadiliko makubwa yaliyopatikana nchini China katika miaka ya hivi karibuni.

Ili kuwaelimisha watoto wao ujuzi kuhusu China, watoto wote watatu baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi walipelekwa kusoma huko Hongkong. Mtoto wake wa kwanza amerudi Unguja kuendesha mkahawa wa chakula cha kichina uitwao Pagoda. Mtoto wa kike amemaliza masomo huko Australia na kupata kazi huko, mtoto wa mwisho bado anasoma ng'ambo.

Kwa ujumla Bi. Chen Lijun na mume wake wanafurahia maisha yao ya huko Zanzibar. Zamani walifanya biashara ya majongoo wa baharini, samaki wengine, na tambi. Wakati huo kwa sababu wakazi wenyeji walikuwa hawajui majongoo ni kitu gani, na kina thamani gani, hivyo biashara ya majogoo imekuwa nzuri sana, lakini katika miaka ya karibuni, wafanyabiashara wengi wa nchi za nje wameenda Unguja kununua majogoo, wenyeji wengi wameanza kufahamu thamani ya majogoo na kumiminikia baharini kuwaokota, hivyo kiasi cha majongoo baharini kimepungua sana. Hivi sasa Bi. Chen Lijun na bwana yake wameanza kuzeeka, hivyo wameamua kuacha biashara ya majongoo na kuanzisha mkahawa wa chakula cha kichina. Kwa kuwa sasa watalii wengi wanamiminikia Zanzibar, hivyo biashara yao ya mkahawa imekuwa mzuri sana.

Licha ya mkahawa wa chakula cha kichina, pia wanashughulika na tambi ya unga, kila asubuhi wanatengeneza tambi, halafu kuzisambaza Unguja, Pemba?hata Dar es Salaam na Mombasa. Mpaka sasa wanajitosheleza na maisha yao ya huko Zanzibar. Lakini kwa sababu Zanzibar ni sehemu ndogo isiyo na hali nzuri ya kiuchumi, hivyo si rahisi kwao kufanya biashara kubwa.

Idhaa ya kiswahili 2007-01-26