Kutokana na mwaliko wa marais wa nchi nane za Cameron, Liberia, Sudan, Zambia, Namibia, Afrika ya kusini, Msumbiji na visiwa vya Shelisheli, Rais Hu Jintao wa China anatazamiwa kufanya ziara ya kiserikali katika nchi hizo kuanzia tarehe 30 Januari hadi tarehe 10 Februari. Ofisa na mtaalamu husika wa China wameona kuwa, ziara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha urafiki wa jadi na kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana na kutimiza maendeleo ya pamoja.
China ikiwa nchi kubwa kabisa inayoendelea duniani, siku zote inaweka mkazo zaidi katika kuendeleza uhusiano kati yake na nchi zinazoendelea, hasa nchi za Afrika. Kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, Rais Hu Jintao kwa niaba ya serikali ya China alitoa hatua nane za kuhimiza ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta mbalimbali.
Ifikapo mwaka 2009, misaada ya China kwa nchi za Afrika itaongezeka kwa mara moja kuliko mwaka 2006; ndani ya miaka mitatu ijayo China itatoa mikopo yenye nafuu ya dola za kimarekani bilioni 3 kwa nchi za Afrika.
Hatua hizo nane zinahusu sekta mbalimbali za siasa, uchumi, elimu, utamaduni na tiba, zinahusu kuongeza misaada na uwekezaji, kupunguza madeni, kusamehe ushuru wa forodha, vilevile zinahusu kuanzisha eneo la uendelezaji wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kuanzisha vituo vya kuendeleza ufundi wa kilimo, na kufanya semina za kuwaandaa watu wenye ujuzi. Hatua hizo zinasifiwa sana na nchi za Afrika. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Zhai Jun hivi karibuni alisema, sababu ya rais Hu Jintao kufanya ziara yake ya kwanza ya mwaka huu barani Afrika, ni kutekeleza kihalisi sera na hatua hizo za China. Alisema:
Ziara hii ya Rais Hu Jintao inalenga kuimarisha na kuendeleza zaidi urafiki wa jadi kati ya China na Afrika, aidha kupanua ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Afrika, hasa kutekeleza kihalisi makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika.
Wakati wa ziara yake hiyo barani Afrika, rais Hu Jintao na viongozi wa nchi 8 za Afrika watabadilishana maoni kuhusu kuimarisha urafiki wa jadi na kuhimiza ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta mbalimbali, ambapo pande mbili mbili zitasaini nyaraka mbalimbali za ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Rais Hu Jintao pia atatembelea hospitali ya wanawake ya Cameroon na Uwanja wa michezo vinavyojengwa kwa msaada wa China; atashiriki sherehe ya kuzinduliwa kwa kituo cha kinga na tiba ya malaria cha China na Liberia, kuwatembelea walinzi wa amani wa China nchini Liberia, pia atashiriki kwenye sherehe ya kuzinduliwa kwa eneo la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa Zambia na China na kushiriki kwenye sherehe ya kuzinduliwa kwa kituo cha vielelezo vya ufundi wa kilimo cha China. Mtafiti wa masuala ya Afrika wa Taasisi ya sayansi ya kijamii Bibi He Wenping alisema:
Kati ya shughuli mbalimbali atakazofanya rais Hu Jintao katika ziara yake hiyo, nyingi zinahusiana na kazi ya kutekeleza kihalisi makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, hiki ni kitendo halisi cha kuhimiza mpango wa utekelezaji, na kuonesha kuwa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika siyo klabu ya kupiga soga tu.
Habari zilisema katika ziara yake nchini Sudan, rais Hu Jintao na rais Omar Al Bashir wa Sudan watazungumza kuhusu suala la Darfur linalofuatiliwa sana duniani kwa hivi sasa.
|