Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-29 18:00:51    
Mkutano wa mwaka wa baraza la uchumi duniani wafungwa

cri

Mkutano wa mwaka wa 37 wa baraza la uchumi duniani ulifungwa tarehe 28 mjini Davos, Uswisi. Kwenye mkutano huo wa siku tano viongozi wa sekta za siasa, biashara, utamaduni na jamii duniani walijadili kwa kina masuala kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya uchumi duniani, mabadiliko ya hali ya hewa, hali ya Mashariki ya Kati, na mazungumzo ya raundi ya Doha.

Kuhusu uchumi wa dunia, viongozi waliohudhuria mkutano huo walitoa matarajio ya kufurahisha. Wanaona kuwa ingawa ongezeko la uchumi wa Marekani huenda litapungua, lakini uchumi wa Umoja wa Ulaya na Japan utaendelea kuongezeka, nchi zinazojitokeza kiuchumi ambazo ni pamoja na China, India, Russia na Brazil zimepata ongezeko kubwa la uchumi. Wataalam walidhihirisha kuwa ongezeko la uchumi wa nchi zinazojitokeza kiuchumi limekuwa uhakikisho muhimu kwa maendeleo ya uchumi duniani, tena matumizi ya bidhaa ya nchini China, India na nchi nyingine yanaongezeka, na ongezeko la mahitaji ya nchini si kama tu litapunguza hali ya kutegemea mauzo ya nje ya bidhaa, bali pia litahimiza uchumi uendelee kwa mwelekeo mzuri zaidi. Viongozi hao pia wanaona kuwa hivi sasa maendeleo ya uchumi duniani yameelekea kwenye kiini cha sehemu mbalimbali kutoka kiini kimoja cha Marekani na Ulaya kama ilivyokuwa zamani, utaratibu wa kuwa na ncha nyingi duniani unaanza kuonekana siku hadi siku.

Suala kuhusu kubadilika kwa hali ya hewa duniani kuwa joto zaidi, ni mada nyingine iliyofuatiliwa sana na viongozi hao kwenye mkutano huo. Matokeo ya utafiti mpya wa sayansi yaliyotolewa kwenye mkutano huo yanaonesha kuwa, mwelekeo wa hali ya hewa duniani kubadilika kuwa joto mwaka hadi mwaka umeleta changamoto kubwa kwa binadamu siku zijazo, hivyo suala hilo linatakiwa kutatuliwa haraka. Chansela wa Ujerumani ambayo ni nchi mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya Bi. Angela Merkel alipohutubia kwenye sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo aliihimiza sana Marekani ipunguze utoaji wa hewa ya Carbon Dioxide na kufuata msimamo wa kuwajibika kwa mazingira ya dunia nzima. China, India na nchi nyingine zinazoendelea zilifahamisha hali ya nchi hizo ya kuchukua hatua za kupunguza utoaji wa hewa ya Carbon Dioxide na sera zao kuhusu nishati mpya, ambapo zimezitaka nchi zilizoendelea zizipatie nchi zinazoendelea uzoefu na teknolojia husika.

Hali ya vurugu za kisiasa imekuwa tatizo kubwa kabisa linaloathiri maendeleo ya uchumi duniani. Hivyo hali ya Mashariki ya Kati, mgogoro nchini Iraq na suala la nyuklia la Iran pia yamekuwa masuala yaliyofuatiliwa sana kwenye mkutano huo. Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw Mahmud Abbas na waziri wa mambo ya nje wa Israel Bi Tzipi Livni walihudhuria kongamano kuhusu suala la Mashariki ya Kati na kufanya mazungumzo, wakitoa mwito wa kuanzisha upya mazungumzo kati ya Palestina na Israel. Makamu wawili wa rais na naibu waziri mkuu wa Iraq, pia walihudhuria mkutano huo na kueleza matakwa yao ya kutuliza mgogoro nchini Iraq mapema iwezekanavyo na kufanya ukarabati baada ya vita. Kuhusu suala la nyuklia la Iran, mkurugenzi mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani IAEA, Bw Mohamed Baradei na katibu mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu Bw Amr Moussa wote walieleza kuwa inapaswa kuepusha kutumia nguvu dhidi ya Iran na ni sahihi kufuata njia ya kidiplomasia kutatua tatizo hilo.

Kuhimiza utandawazi wa uchumi duniani ni wajibu mkuu wa baraza la uchumi duniani. Lakini mchakato wa biashara huru unaendelea huku kukiwa na vikwazo, na mazungumzo ya Doha yamesimamishwa kwa nusu mwaka. Tofauti kati ya pande mbalimbali kwenye mazungumzo hayo iko katika biashara ya mazao ya kilimo. Kwa kuwa Marekani inashikilia kutoa ruzuku kubwa kwa mazao yao ya kilimo yanayosafirishwa kwa nje na Umoja wa Ulaya unashikilia kutoza ushuru mkubwa wa forodha kwa kuagiza mazao ya kilimo, hivyo mazungumzo ya Doha yamekwama. Baada ya mkutano huo, mkurugenzi mkuu wa WTO Pascal Lamy alizihimiza nchi muhimu wanachama za WTO zifuate njia mpya kufanya mazungumzo na kupata maendeleo, ama sivyo mazungumzo hayo yatakabiliwa na hatari ya kushindwa.