Tarehe 30 msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bi. Jiang Yu alitangaza kuwa baada ya kufanyika kwa majadiliano, mkutano wa kipindi cha tatu wa duru la tano la mazungumzo ya pande sita utaanza kufanyika tena tarehe 8 Februari mjini Beijing, pande husika zimeonesha msimamo wa kuukaribisha mkutano huo.
Bi. Jiang Yu alisema katika siku ambapo mazungumzo yalikwamwa, pande husika zilijadiliana kuhusu namna ya kuendelea na mazungumzo na kutekeleza taarifa ya pamoja, majadiliano hayo yameweka msingi wa kurejesha mapema mazungumzo hayo. Bi. Jiang Yu alisema China itashirikiana na pande husika ili kuyafanya mazungumzo yapate mafanikio, na alitumai kuwa pande husika zitafanya juhudi kuimarisha mazungumzo na imani ili kutekeleza taarifa ya pamoja na kuhakikisha kuwa peninsula ya Korea haina silaha za nyuklia.
Naibu msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Tom Casey tarehe 30 alisema Marekani inatumai kuwa mazungumzo ya pande sita yatapata maendeleo halisi kuhusu "taarifa ya pamoja ya 19 Septemba". Lakini mkuu wa ujumbe wa Marekani kwenye mazungumzo ya pande sita ambaye pia ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw.Christopher Hill alisema, huenda mazungumzo hayo yakafikia makubaliano mapya ambayo yatafanana na "makubaliano ya Geneva kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani mwaka 1994", na hayo ni matarajio tu pengine makubaliano yenyewe yatakwenda mbali zaidi.
Wizara ya mambo ya nje na biashara ya Korea ya Kusini ilitoa taarifa ikitumai kuwa mazungumzo hayo yatapata makubaliano halisi kuhusu namna ya kuanza hatua za kutekeleza taarifa ya pamoja.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Russia ambaye ni mkuu wa ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo ya pande sita Bw. Alexander Lusyukov alisema kurejesha mazungumzo kumeonesha mabadiliko ya misimamo ya pande husika, anaonesha matumaini yenye tahadhari.
Naibu katibu mkuu wa baraza la mawaziri la Japan Bw. Suzuki Seiji kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, Japan itashirikiana na Marekani na China ili kuifanya Korea ya Kaskazini ichukue hatua halisi katika kuacha silaha za nyuklia, na waziri mkuu wa Japan Bw. Shinzo Abe alionya kuwa kama mazungumzo hayo hatayapata maendeleo yoyote, jumuyia ya kimataifa itazidi kuishinikiza Korea ya Kaskazini na kuifanya ikabiliwe na hali ngumu zaidi.
Pamoja na hayo pande husika zilifanya majadiliano kuhusu mazungumzo hayo. Waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini tarehe 30 alibadilishana maoni na waziri wa mambo ya nje wa Russia kwa njia ya simu na kukubaliana kusukuma mbele mazungumzo hayo. Mkuu wa ujumbe wa Korea ya Kusini katika mazungumzo ya pande sita Bw. Chun Yung Woo tarehe 31 atakwenda nchini Russia na kufanya mazungumzo na mkuu wa ujumbe wa Russia katika mazungumzo ya pande sita Bw. Sergey Lavrov. Aidha, mkuu wa ujumbe wa Marekani katika mazungumzo ya pande sita Bw. Christopher Hill atazuru Korea ya Kusini na Japan ili kusawazisha misimamo kuhusu mazungumzo hayo ya pande sita.
Vyombo vya habari vimegundua kwamba baada ya kutangaza tarehe ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya pande sita, Marekani na Korea ya Kaskazini tarehe 30 zilifanya majadiliano mjini Beijing. Mwakilishi wa Marekani Bw. Daniel Glaser alisema, pande mbili zilibadilishana maoni kuhusu suala la mambo ya fedha na kuamua kuwa zitaendelea zaidi na mazungumzo hayo. Baadhi ya wataalamu wanasema, hapo kabla Korea ya Kaskazini ilikuwa inaunganisha utatuzi wa tatizo la mambo ya fedha na suala la silaha, na Marekani ilikuwa inapinga kuunganisha masuala hayo mawili. Lakini kutokana na hali ilivyo sasa, misimamo ya pande mbili imebadilika kwa kiasi fulani, na mabadiliko hayo yatasaidia kuondoa vikwazo vya maendeleo ya mazungumzo.
Idhaa ya kiswahili 2007-01-31
|