Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-31 18:49:28    
China yawasaidia wafanyakazi vibarua wanaohamahama wainue uwezo wa kujikinga dhidi ya ugonjwa wa ukimwi

cri

Mradi wa ushirikiano wa kimataifa kuhusu kinga na tiba ya ukimwi kwenye viwanda na kampuni umeanzishwa tarehe 26 hapa Beijing, mradi huo unalenga kuwasaidia wafanyakazi vibarua mijini wanaohamahama kuongeza uwezo wa kujikinga dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Hivi sasa China inakabiliwa na changamoto ya ukimwi. Takwimu zinaonesha kuwa, ilipofika mwishoni mwa mwaka 2005, watu laki sita na elfu hamsini nchini China walikuwa wameambukizwa virusi vya ukimwi au walikuwa wagonjwa wa ukimwi, na idadi ya watu hao inaongezeka siku hadi siku, ambapo wafanyakazi wanaohamahama wanachukuliwa kuwa ni watu wenye hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Kutokana na hatua kubwa ya utandawazi wa miji kote nchini China, ujenzi wa miji umewavutia wakulima wengi ambao ni nguvu kazi ya ziada vijijini waingie mijini kufanya kazi za vibarua, takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya watu hao inakaribia watu milioni 200, ambao wengi kati yao ni wenye elimu ya chini, na tena hawajapata ujuzi kuhusu afya, na maisha yao ya kuhamahama yamewafanya wawe watu ambao ni rahisi zaidi kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imefanya kazi nyingi kuhusu kuwasaidia wafanyakazi wanaohamahama kuepusha kuambukizwa virusi vya ukimwi, na ili kukabiliwa na changamoto kubwa, idara husika za China pia zinafanya juhudi za kutafuta ushirikiano wa kimataifa. Mkurugenzi wa upande wa China anayeshughulikia mradi wa ushirikiano wa kimataifa ulioanzishwa tarehe 26 na Wizara ya kazi na huduma za jamii ya China, Shirika la wafanyakazi duniani na Wizara ya kazi ya Marekani Bwana Zheng Dongliang alisema:

China ikiwa nchi yenye idadi kubwa ya watu, inakabiliwa na masuala mbalimbali kuhusu kukabiliana na changamoto ya ukimwi, namna ya kutumia uzoefu duniani, pamoja na nguvu bora ya Shirika la wafanyakazi duniani katika sera na ufundi, ili kuzitumia katika viwanda na kampuni za China, hizo ni kazi muhimu sana.

Mradi huo utakaogharamiwa kwa dola za kimarekani milioni 3.5 na Wizara ya kazi ya Marekani utatelezwa kihalisi na Wizara ya kazi na huduma za jamii ya China pamoja na shirika la wafanyakazi duniani, ambapo mikoa mitatu ya Guangdong, Yunnan na Anhui imechaguliwa kuwa mikoa itakayofanya kazi za majaribio, ndani ya miaka mitatu ijayo, shughuli mbalimbali za utoaji mafunzo zitafanyika, ili kuvisaidia viwanda na kampuni, wafanyakazi na familia zao zielewe kwa usahihi zaidi ujuzi kuhusu kinga ya ukimwi; kupunguza vitendo vya hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi kwa wafanyakazi wanaohamahama mijini; na kupunguza vitendo vya kuwadhalilisha na kutowapatia watu walioambukizwa virusi vya ukimwi nafasi za ajira.

Mkoani Guangdong hivi sasa kuna wafanyakazi wanaohamahama wapatao milioni 22, ambao waliotoka mikoa mbalimbali nchini China. Ofisa wa mkoa huo anayeshughulikia mradi wa kinga ya ukimwi kwenye viwanda na kampuni Bwana Liang Manguang alisema:

Hivi sasa tunajitahidi kufanya maandalizi ili kuanzisha mradi huo kwa pande zote, tutafanya juhudi kwa kadiri tuwezavyao ili kutoa elimu kuhusu kinga ya ukimwi.

Mkurugenzi wa shirika la wafanyakazi duniani anayeshughulikia utekelezaji wa mradi huo Bwana Hao Reizhi alisema, tunapaswa kuandaa semina kwa kutoa mafunzo ili wafanyakazi wabadilishe vitendo vyao, vilevile tunatakiwa kutoa sera mbalimbali, kuwaandaa walimu kwenye viwanda na kampuni ili wawafundishe wafanyakazi na kuwapatia ujuzi sahihi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Utekelezaji wa mradi na sera hizo utaweza kuhakikisha kazi yetu ya kutimiza lengo la kujikinga dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.