Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-31 19:36:55    
Tukio la Uingereza kutupa takataka nchini China lafuatiliwa na kulaumiwa

cri

Hivi karibuni takataka nyingine zenye uzito wa tani laki mbili hivi zimesafirishwa na kufika nchini China kutoka Uingereza, takataka hizo zimesababisha uchafuzi kwa mazingira ya sehemu ya China. Vitendo vya Uingereza kutupa takataka zake mara kwa mara nchini China vimelaumiwa vikali na watu wa jamii ya China.

Idara za serikali za China zimeanza kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo. Sehemu ya Nanhai mjini Foshan mkoani Guangdong, kusini mwa China ambayo ni sehemu inayofahamika kwa takataka hizo ni sehemu ambayo takataka za plastiki hukusanyika kwa wingi. Serikali ya huko inafanya kazi kubwa ya kushughulikia soko la takataka za plastiki la sehemu hiyo, na kuweka vituo vya kukagua magari ya kuchukua vifaa kwenye njia muhimu mbalimbali, na takataka zinazogunduliwa zinateketezwa. Ofisa wa idara husika ya sehemu ya Nanhai mjini Foshan Bwana Wu Shaoqiu alisema:

Tumevitaka vituo mbalimbali vinavyoshughulikia takataka zilizopokewa kutoka nchi za nje visimamishe shughuli zao mara moja, na katika siku zijazo shughuli kama hizo zitapigwa marufuku.

Imefahamika kuwa kila mwaka Uingereza inatuma tani milioni 1.9 za takataka zake nchini China, nyingi kati ya hizo ni takataka za bidhaa za elektroniki, takataka hizo zimeleta uchafuzi mbaya kwa mazingira ya sehemu kadhaa mkoani Guangdong.

Vitendo hivyo vya Uingereza vimelaaniwa vikali na watu wa jamii ya China. Naibu mtafiti wa idara ya elimu ya sheria katika Taasisi ya sayansi ya jamii ya Shanghai Bwana Yang Pengfei alidhihirisha kuwa, nchi inayosafirisha takataka nje si kama tu imekiuka sheria husika ya China, bali pia imekiuka "Mkataba wa Basel" ambao ni mkataba wa kimataifa unaohusu kudhibiti takataka zisihamishwe kuvuka mipaka. Ingawa sheria husika zimekuwepo, lakini takataka zinazosafirishwa kwa China kutoka nchi za nje zinaongezeka siku hadi siku, Bwana Yang alisema sababu ni kwamba:

Hivi sasa kazi ya kushughulikia takataka ni yenye taabu kubwa, serikali na jamii za nchi nyingine pia zinakabiliwa na tatizo hilo. Kama takataka zinaweza kusafirishwa katika nchi kadhaa zinazoendelea, gharama za kushughulikia takataka hizo hakika ni ndogo kwenye nchi zilizoendelea.

Kanuni za nchi nyingi zilizoendelea zinazohusu kazi ya kushughulikia takataka ni kali sana, tena matumizi ya kazi hiyo ni makubwa sana, ndiyo maana watu fulani wanahamishia takataka zao katika nchi zinazoendelea ili kuzishughulikia. Na wahalifu fulani pia wameona thamani ya kutumia takataka fulani, hivyo wanasafirisha takataka nyingi kwenye nchi zinazoendelea bila kujali kukiuka sheria.

Lakini safari hii hali ni tofauti na ile ya safari zilizopita, kwamba takataka zilizowasilishwa nchini China hasa ni takataka za maishani na takataka za plastiki. Mkazi wa Beijing Bwana Mao Da anayeshughulikia hifadhi ya mazingira alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, takataka hizo zitaleta madhara ya muda mrefu kwa mazingira na watu nchini China. Alisema:

Wakati wa kuteketeza takataka hizo, hewa zenye vitu vingi vyenye sumu vinaweza kutolewa, ikiwemo dioxin, ambayo inaweza kuwepo kwa muda mrefu katika mazingira, dioxin inaweza kuleta madhara makubwa kwa mfumo wa kinga mwilini mwa mtu, na imethibitishwa kuwa ni kitu kinachosababisha saratani.

Tukio hilo limefuatiliwa na jumuiya maarufu duniani ya amani ya kijani, mkurugenzi wa jumuiya hiyo Bibi Yue Yihuan alisema, takataka hizo zinapaswa kurudishwa nchini Uingereza, nchi hiyo inapaswa kuwajibika na tukio hilo.