Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-02 15:13:46    
Madaktari wa China wanaotoa huduma kwa watanzania kwa moyo mkunjufu kwa miaka zaidi ya 40

cri

Tangu kikundi cha kwanza cha madaktari wa China kitumwe nchini Tanzania mwezi Agosti mwaka 1964 hadi sasa, vikundi mbalimbali vya madaktari wa China wameshatoa huduma za matibabu kwa moyo mkunjufu kwa watu wa Tanzania katika miaka zaidi ya 40 iliyopita. Kwenye hospitali ya Mnazi Mmoja ya Zanzibar, daktari Sui alipomaliza upasuaji wa kujifungua kwa ajili ya mwanamke mmoja, alitokwa na jasho jingi kama ameloweshwa na maji. Kutokana na hali ya hewa ya joto na hali duni ya vifaa, kwa kweli madaktari wa China wanaofanya kazi nchini Tanzania wanaogopa kufanya upasuaji, lakini wanapaswa kufanya upasuaji mara kwa mara.

Daktari Sui alisema kwa sababu katika chumba cha kujifungua hakuna kiyoyozi, na tena wanawake wanaojifungua ni wazito zaidi kuliko yeye, hivyo kila siku anatokwa jasho jingi. Daktari Sui mwenye umri wa miaka 53 amefanya kazi kisiwani Zanzibar kwa mwaka mmoja na nusu, ameokoa maisha ya wajawazito wengi waliokumbwa na shida wakati wa kujifungua, anasifiwa kuwa ni daktari No. 1 wa uzazi.

Mkuu wa kikundi cha madaktari wa China kisiwani Zanzibar Bwana Wang Peng alieleza kuwa, daktari Sui ambaye hafahamu lugha ya Kiswahili wala Kiingereza alipowasili mjini Zanzibar, mara moja alianza kazi ya kuwahudumia wagonjwa na kufanya upasuaji kwa msaada wa mkalimani. Baada ya juhudi za miezi miwili, alipata maendeleo makubwa katika kujifunza Kiswahili na Kiingereza, hata anaweza kushika zamu peke yake bila ya mkalimani. Licha ya kuwa na ustadi mzuri wa matibabu, daktari Sui pia ana moyo mkunjufu wa kuwahudumia wagonjwa, mahitaji ya wagonjwa ndiyo wajibu wake, hata akiitwa akiwa amelala usiku wa manane huwa anaamka mara moja na kukimbilia hospitalini bila ya malalamiko.

Madaktari wachina wanaofanya kazi katika nchi za Afrika karibu wote wanakumbwa na matatizo ya aina moja, kama vile mazingira magumu ya kazi, hali ngumu ya kimaisha na upweke. Lakini pia wana furaha tele wakati wa wanapofanikiwa kuokoa maisha ya wagonjwa, kama alivyosema Daktari Sui:

"Ninapowapokea wagonjwa, huwa nakuwa na wasiwasi kuhusu hali yao, lakini watoto wanapozaliwa salama baada ya juhudi zangu, huwa nasikia furaha tele moyoni, naona umuhimu wa kazi yangu hapa."

Daktari wa akyupancha wa China Bwana Liu Zhengfeng anafanya kazi katika hospitali ya Muhimbili, mjini Dar es Salaam, aliwahi kumtibu rais wa zamani wa nchi hiyo Bw Benjamin Mkapa ugonjwa wa baridi yabisi. Alipoulizwa ni wakati gani anafurahia zaidi kazi yake, jibu lake lilikuwa ni "wakati akifanya kazi". Ni kweli kwamba lengo la madaktari wa China waliotumwa nchini Tanzania ni kuwasaidia wagonjwa wa huko kuondokana na magonjwa na maumivu.

Daktari Liu alisema kwa kutoa mfano, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 12 aliugua ugonjwa wa neva wa kutoweza kusikia, mama yake alitaka kumpeleka kusoma kwenye shule ya watoto wasioweza kusikia na kuongea, daktari Liu alimshauri mama huyo mtoto wake atibiwe kwa akyupancha. Baada ya kutibiwa na akyupancha kwa miezi miwili, uwezo wa msichana huyo kusikia ulianza kurudi hatua kwa hatua, hivi sasa anaendelea kusoma katika shule aliyokuwepo.

Ingawa Tanzania inatekeleza utaratibu wa matibabu bure, lakini baadhi ya wagonjwa ni maskini wanashindwa kumudu gharama za usafiri wa kufika hospitali. Msichana mwingine aliyekuwa anaugua ugonjwa wa kutoweza kusikia kutokana na matatizo ya mishipa ya fahamu anaishi katika kijiji kilicho umbali wa kilomita zaidi ya kumi kutoka jijini Dar es Salaam, daktari Liu alipofahamu kwamba, msichana huyo hakuwa na pesa za nauli, alimpa nauli ya kurudi nyumbani na kuja tena kwa matibabu ya mara nyingine. Alisema:

"Niliwahi kufika nyumbani kwake, msichana huyo hana baba, anaishi pamoja na mama na bibi yake, nyumbani kwao hawana kipato, wanalala kwenye mkeka tu, hakuna hata kitanda. Nilipomtembelea nyumbani kwao, nilipikwa mboga tu, nataka kumsaidia mpaka apone."

Kwenye makazi ya madaktari wa China karibu kila usiku inasikika kengele ya kupelekwa kwa wagonjwa wa dharura au milio ya ving'ora vya magari ya wagonjwa, kunapokuwa na wagonjwa mahututi ndipo kunapokuwa na madaktari wa China. Naibu mkuu wa hospitali ya Mnazi Mmoja Bwana Ahmed alisema:

"Madaktari wa China wametupa msaada mkubwa, hasa wakati wa usiku wa manane na wanapokuja watu wenye magonjwa hatari sugu."

Mkuu wa idara ya upimaji ya hospitali ya Muhimbili Bwana Oudugu alisema: "Kila siku madaktari wa China wanafika kazini mapema kuliko madaktari wenyeji, na kuchelewa zaidi kuondoka, maadili yao ya kikazi yameleta athari kubwa kwa madaktari wa Tanzania."

Dereva mmoja wa Dar es Salaam alisema: "Madaktari wa China wana ustadi mzuri, hivyo tunapenda kuhudumiwa na madaktari wa China."

Naibu mkuu wa hospitali ya Muhimbili Bwana Swai alisema, alichagua kozi ya upasuaji wa kifua alipokuwa kijana kutokana na athari ya daktari Guo wa China aliyefanya kazi nchini Tanzania katika miaka ya 70 hadi 80 ya karne iliyopita, alisema Tanzania inahitaji madaktari wengi zaidi wa China.

Katibu mkuu wa wizara ya afya ya Tanzania Bwana Jidawi alisema: "Madaktari wa China wametoa mafunzo kwa madaktari wengi wenyeji, wamewatibu wagonjwa wengi na kutupatia dawa nyingi. Madaktari wa China pia ni marafiki wetu wakubwa, na wametuwezesha kufahamu mambo mengi ya China."

Madaktari wa China si kama tu wanachapa kazi nchini Tanzania, bali pia wanatoa huduma kwa watu wa Algeria, Tunisia, Sudan na nchi nyingine za Afrika. Urafiki mkubwa wa jadi kati ya China na nchi za Afrika unaimarishwa na watu kama madaktari hao.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-02