Eneo la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ambalo ni la kwanza kuanzishwa na China barani Afrika limezinduliwa tarehe 4, Januari huko Lusaka, mji mkuu wa Zambia. Rais Hu Jintao wa China ambaye yupo nchini Zambia kwa ziara na rais Levy Mwanawasa wa Zambia walihudhuria uzinduzi huo.
Kwenye uzinduzi huo, rais Hu Jintao alisema "Eneo hilo la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ni sehemu ya matunda yaliyopatikana kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Kuanzishwa kwa eneo hilo ni jambo muhimu katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Zambia, na vilevile ni ishara kwamba ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika umepiga hatua mpya."
Rais Hu Jintao aliongeza kuwa, China siku zote inafanya juhudi kuendeleza ushirikiano na nchi za Afrika katika fani mbalimbali. Katika ushirikiano huo, China inafuata kanuni ya urafiki wa dhati, kuwa na usawa na kunufaishana, mshikamano na ushirikiano na kupata maendeleo ya pamoja. Alisema ushirikiano huo umewaletea watu wa China na Afrika maslahi halisi. Mwezi Novemba mwaka jana kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, rais Hu Jintao kwa niaba ya serikali ya China, alitangaza kuwa China itaanzisha maeneo kati ya matatu na matano ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara barani Afrika katika miaka mitatu ijayo. Kwa mujibu wa mpango husika, eneo hilo lililoanzishwa nchini Zambia ni la kwanza. Hadi kufikia mwaka 2010 wakati ambapo ujenzi wa eneo hilo utakapokamilika, viwanda 60 kutoka China na nchi nyingine vitajengwa katika eneo hilo na kuleta uwekezaji wa vitega uchumi vyenye thamani ya dola milioni 800 za kimarekani, na kutoa nafasi za ajira elfu 6.
Rais Hu Jintao wa China alisema "Safari hii nimekuja barani Afrika kwa lengo la kuimarisha urafiki uliopo kati ya China na Afrika, kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kupanua wigo wa ushirikiano wa mambo halisi na kuhimiza maendeleo ya pamoja."
Kuhusu Zambia rais Hu Jintao alisema "Zambia ni nchi muhimu katika sehemu ya kusini mwa Afrika, pia ni nchi ya kwanza iliyoanzisha uhusiano wa kibalozi na China miongoni mwa nchi za kusini mwa Afrika. Hivi sasa uchumi wa Zambia unaendelea vizuri, na mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa siku hadi siku. Serikali ya China inahamasisha na kuunga mkono viwanda vyenye nguvu vya China kuwekeza kwenye eneo hilo la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na kutoa mchango kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya Zambia."
Rais Levy Mwanawasa wa Zambia alipongeza kuanzishwa kwa eneo hilo, akisema "Kuanzishwa kwa eneo hilo ni kutekeleza ahadi aliyotoa rais Hu Jintao kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Watu wa Zambia watanufaika na eneo hilo, hususan katika mambo ya ajira, teknolojia na mafunzo kwa watu. Kuanzishwa kwa eneo hilo pia kutaboresha maisha ya watu wa nchi jirani na kuendeleza uchumi wa Zambia. Tunatumai viwanda vingi vya China vitawekeza eneo hilo, jambo ambalo litatuletea ujuzi, teknolojia na uzoefu wa usimamizi, pia kuleta nafasi za kujiendeleza kwa viwanda vya China, vya kigeni na vya Zambia."
Idhaa ya kiswahili 2007-02-05
|