Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-05 16:47:18    
Mtaalamu wa taaluma ya riwaya ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu"

cri

"Ndoto kwenye Jumba Jekundu" ni riwaya maarufu katika fasihi ya kale nchini China. Wasomi wengi wamewahi kufanya utafiti kuhusu riwaya hiyo na mwandishi wake Cao Xueqin, na kuufanya utafiti huo kuwa taaluma. Mmoja wa watafiti hao anaitwa Zhou Ruchang.

Bw. Zhou Ruchang mwenye umri wa miaka 88 ni msomi mkubwa nchini China na katika nyanja ya kimataifa ya taaluma ya riwaya ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu", kwani kabla yake, ingawa kulikuwa na wasomi wengi waliowahi kufanya utafiti huo, lakini hakukuwa na msomi hata mmoja aliyetumia maisha yake yote katika utafiti huo na kuuendeleza utafiti huo kutoka fasihi hadi kwenye ngazi ya utafiti wa utamaduni, mafanikio aliyopata ni makubwa na yanavutia. Lakini hapo awali Bw. Zhou Ruchang alianza kufanya utafiti wa riwaya hiyo kwa bahati tu. Mwaka 1947 Bw. Zhou Ruchang aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Yanjing aligundua kitabu cha mkusanyiko wa mashairi ya Cao Xueqin ambaye ni mwandishi wa riwaya ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" katika mkataba, miongoni mwa mashairi hayo kulikuwa na mashairi sita yaliyohusu maisha ya Cao Xueqin. Bw. Zhou Ruchang aliona mashairi hayo ni muhimu sana, kwa sababu katika muda mrefu uliopita watu walikuwa na mazungumzo mengi yasiyo bayana kuhusu maisha ya Cao Xueqin. Kwa hiyo aliandika makala yake ya kwanza ya kitaaluma kuhusu riwaya hiyo. Bw. Zhou Hongchang alisema, alipoandika makala hiyo hakuwa na nia yoyote, ila kujiburudisha tu. Alisema,

"Wakati huo nilikuwa mwanafunzi, sikufikiria kuichapisha makala yangu ili nipate malipo na kujipatia umaarufu. Baada ya kuandika niliiacha na kusahau. Muda mrefu baadaye, mwalimu wangu alipotaja makala yangu alisema si vibaya kuichapisha."

Baada ya makala hiyo yenye kichwa "Makisio kuhusu hali ya Cao Xueqin alipokufa" kuchapishwa katika magazeti, mara ilimvutia Bw. Hu Shi aliyekuwa msomi maarufu wa taaluma ya riwaya ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu". Baadaye Bw. Hu Shi alimwadikia barua sita Zhou Ruchang kujadiliana naye kuhusu masuala ya taaluma. Bw. Zhou Ruchang alitiwa moyo na tokea hapo alianza kushika utafiti ambao aliufanya kwa muda wa nusu ya karne.

Mwaka 1953 kitabu cha kwanza cha kitaaluma cha "Ushahidi Mpya kuhusu Riwaya ya Ndoto kwenye Jumba Jekundu" kilichapishwa, kwenye kitabu hicho alitoa maoni mengi mapya baada ya uchunguzi wa makini. Bila kutegemea kwamba, kitabu hicho kilinunuliwa haraka mno hata kilichapwa mara tatu katika muda wa miezi mitatu, hali ambayo iliitingisha nyanja ya taaluma. Lakini Bw. Zhou Ruchang hakuridhika na mafanikio hayo, katika miaka 20 ya baadaye japokuwa masikio yake yalianza kutosikia vizuri na mwaka 1974 macho yake yalianza kutoona vizuri kutokana na kusoma sana lakini kwa nia imara alimaliza maandishi yake ya kitaaluma yenye maneno milioni kadhaa. Mafanikio hayo yalimfanya Bw. Zhou Ruchang aone kuwa ametimiza tu wajibu wake. Alisema,

"Nimepata mafanikio kiasi fulani, lakini sikufanya hayo kwa ajili ya maslahi yangu binafsi, kama ningefanya kwa ajili ya maslahi yangu binafsi ningeigusa tu taaluma hiyo na kuiacha baada ya kupata umaarufu, hali yangu ilivyo sasa ni kwamba mimi bado ni maskini, sina chochote, sijali hata kidogo hali na mali. Hisia yangu kubwa ambayo inazidi kuongezeka ni athari kutoka kusoma 'Ndoto kwenye Jumba Jekundu' na kumfahamu mwandishi wa riwaya hiyo Cao Xueqin."

Bw. Zhou Ruchang alisema, "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" ni riwaya inayong'ara kabisa katika fasihi ya kale nchini China, ndani ya riwaya hiyo kuna fikra za falsafa ya Kimashariki na utamduni wa jadi wa China. Ni jambo la kusikitisha kwamba wasomaji wengi wanaichukulia riwaya hiyo kuwa ni riwaya ya kawaida ya mapenzi, hali hiyo inamhuzunisha sana. Alisema,

"Sikusoma riwaya ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" kwa ajili ya kufurahia hadithi zake za kutokuwa na uhuru wa kuchumbiana na kupinga umwinyi, kwani huu sio undani wa riwaya hiyo, kitu alichotuachia mwandishi Cao Xueqin ni hazina kubwa ya utamaduni wa taifa la China ambao unaoneshwa wazi na kwa makini sana."

Akiwa anapenda sana riwaya hiyo na mwandishi wa riwaya hiyo Bw. Zhou Ruchang alitumia wakati wake wote maishani mwake kufanya utafiti. Jambo linalostaajabisha ni kuwa mwaka 2005, Bw. Zhou Ruchang aliyekuwa na umri wa miaka 87 alichapisha vitabu saba mfululizo kuhusu taaluma ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu". Vitabu hivyo, aliviandika kwenye karatasi kwa maneno makubwa kama mpira wa mchezo wa mezani, baadaye alimwomba binti yake kuyanukuu kwa kompyuta, amsomee mara kadhaa na asahihishe.

Mapema mwaka huu kitabu chake kingine cha "Mvuto wa usanii wa Ndoto kwenye Jumba Jekundu" kilichapishwa. Kwenye kitabu hicho alieleza sehemu zenye uhodari mkubwa wa uandishi katika mashairi, uchoraji wa picha, muziki na opera, ni kitabu kinachowafahamisha zaidi wasomaji.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-05