Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-05 19:37:57    
Kazi ya kuwamba jumba la kuogelea kwa plastiki maalum yamalizika

cri

Hivi karibuni jumba la kuogelea lililojengwa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 mjini Beijing limemalizika kuwambwa kwa plastiki maalum. Baada ya kuwambwa, jumba hilo linanawiri kwa sura yake kama mapovu ya maji yenye rangi ya buluu. Hivi sasa kazi iliyobaki ni kukamilisha ndani.

Jumba la kuogelea inajengwa kwa gharama ya yuan bilioni 1.2 ambazo zote zilitolewa na wakazi wa Hong Kong, Macau na Taiwan na Wachina waishio katika nchi za nje. Jumba hilo linakabiliana na jengo la uwanja wa michezo lenye sura ya "kiota". Majengo hayo mawili yamekuwa alama za kuvutia zaidi katika upande wa kaskazini wa mji wa Beijing.

Awali msanifu wa jumba hilo alikuwa na wazo la kulifanya jumba hilo liwe na sura inayohusiana na maji kutokana na kazi yake ya kuogelea, mwishowe amefanikiwa kutimiza wazo lake. Msanifu wa jumba hilo Bi. Wang Min alieleza,

"Hapo awali tulikuwa na tumaini la kulifanya jumba hilo liwe na sura inayohusiana na maji. Mwishowe tumeamua kuwamba jumba hilo liwambwe kwa vipande vya plastiki ambavyo baada ya kutunishwa vinaonekana kama mapovu ya maji."

Ujenzi wa jumba la kuogelea na uwanja wa taifa wa riadha ulizinduliwa kwa pamoja mwishoni mwa mwaka 2003. Baada ya miaka mitatu, ujenzi wa jumba la kuogelea umekamilika kwa muundo wa chuma na kuanzia majira ya joto ya mwaka jana lilianza kuwamba kwa vipande vya plastiki maalum. Tunaposema plastiki maalum tuna maana plastiki hiyo inadumu sana na inaweza kuhimili uzito mkubwa, kwa mujibu wa majaribio, plastiki hiyo ambayo ina unene kama karatasi tu, hata gari linaweza kupita kwenye plastiki hiyo na isipasuke.

Sifa nyingine ya plastiki hiyo ni kuweza kujisafisha. Msimamizi wa ujenzi wa jumba hilo Bw. Han Tao alieleza,

"Plastiki hiyo hainyonyi kabisa maji, maana maji yakipita hayaachi alama yoyote juu yake, kwa hiyo mavumbi na uchafu mwingine utaondolewa pamoja na maji ya mvua."

Kutokana na plastiki kutonyonya maji, jumba hilo limesanifiwa pamoja na mfumo wa kuvuna maji ya mvua. Paa la jumba hilo lina eneo la mita za mraba elfu 30, linaweza kuvuna maji ya mvua tani elfu 10 kwa mwaka na mengi ya maji hayo yanaingia kwenye mfumo wa huduma za maji. Ili kulinda "koti" la jumba hilo lenye rangi ya samawati msanifu amechukua hatua ya kulilinda. Bi. Wang Min alisema,

"Ingawa hatutaki jumba hilo liwe mbali na watu, lakini pia hatutaki watu waliliguse, kwa hiyo tumechukua hatua ya kuchimba mfereji wenye upana wa mita minne pembezoni mwa jumba hilo ili kuzuia watu wasilikaribie, na mfereji huo pia umepamba mandhari ya maji."

Baada ya kukamilisha kazi ya kuwamba plastiki maalum nje ya jumba hilo, kazi ya kukamilisha ndani inaendelea. Kazi muhimu ya ndani ni bwawa na jukwaa la kupiga mbizi la waogeleaji. Bwawa hilo pia limebuniwa kwa kuzingatia mazingira bora kwa waogeleaji. Mhandisi wa ujenzi wa jumba hilo Bw. Sun Hongzhuang alisema,

"Kina cha maji ni mita tatu ambacho ni ongezeko la nusu mita kuliko kina cha kawaida. Kina hicho kinasaidia kupunguza mawimbi yanayoathiri waogeleaji na kinafaa kwa waogeleaji kufanya vitedo vya aina mbalimbali."

Katika siku za michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 mjini Beijing, jumba la kuogelea litakuwa na michezo ya kuogelea, kupiga mbizi, mpira wa maji na kuogelea kwa vitando mbalimbali, waogeleaji watagombea medali za 46 za dhahabu. Jumba hilo linaweza kukaliwa na watazamaji 17,000, kati ya hao watu 11,000 watakaa kwenye viti vya muda, yaani baada ya mashindano kumalizika, viti hivyo vya muda vitaondolewa, na jumba hilo litabadilishwa kuwa jumba la wazi kwa umma na linaweza kufanya michezo ya aina nyingi ya majini, licha ya kuweza kuandaa mashindano ya kimataifa pia linaweza kukidhi mahitaji ya burudani kwa watu wa kawaida. Meneja mkuu wa jumba hilo la kuogelea Bw. Kang Wei alieleza,

"Tutaligawa jumba hilo katika sehemu tofauti, kwa mfano bwawa, hakika tutawawezesha watu wa kawaida kuingia na kumudu kiingilio."

Jumba hilo la kuogelea litakamilika mwishoni mwa mwaka 2007, na mwezi Februari mwaka 2008 mashindano ya kuogelea ya China yatafanyika katika jumba hilo. Kadhalika kabla ya kufanyika kwa michezo ya Olimpiki mjini Beijing, jumba hilo litaandaa mashindano ya kupiga mbizi na kuogelea kwa vitendo vya aina mbalimbali kwa ajili ya kuchagua wachezaji watakaoshiriki kwenye mashindano ya dunia.

Idhaa ya Kiswahili 2007-02-05