Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-06 14:50:15    
Rais Hu Jintao wa China afanya ziara nchini Namibia

cri

Kutokana na mwaliko wa rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia, rais wa China Hu Jintao tarehe 5 alifika Windhoek, mji mkuu wa Namibia kuanza ziara yake ya kiserikali nchini humo.

Namibia ni nchi iliyoko kusini magharibi mwa Afrika, ni nchi yenye historia ndefu, lakini ni nchi ya mwisho kabisa kupata uhuru barani Afrika, kwa hiyo pia ni nchi changa kabisa barani humo.

Rais Hu Jintao alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Windhoek alikaribishwa na wenyeji kwa shangwe kubwa.

Ingawa China na Namibia zinatengana kwa masafa marefu, lakini nyoyo za watu wa nchi mbili zinaungana. Siku ya pili tu baada ya Namibia kupata uhuru yaani tarehe 22 Machi mwaka 1990, China na Namibia zilianzisha uhusiano wa kibalozi. Kwenye tafrija ya kumkaribisha rais Hu Jintao iliyoandaliwa na raia Pohamba, rais Hu Jintao alisifu sana urafiki kati ya nchi hizo mbili. Alisema,

"Katika kipindi wakati Namibia ilipopigania uhuru, China na Namibia zilikuwa ni marafiki wa kivita, na katika miaka wakati Namibia inapojenga taifa baada ya kupata uhuru, China na Namibia ni wenzi wa ushirikiano. Katika miaka 17 iliyopita tokea uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili uanzishwe, mwaka hadi mwaka nchi hizo mbili zimekuwa zikipanua ushirikiano katika sekta za uchumi, biashara, elimu, afya na utamaduni, urafiki na maelewano kati ya watu wa nchi mbili yanazidi kuwa makubwa. Katika mambo ya kimataifa, pande mbili zinazidi kuaminiana na kuungana mkono. Namibia inatekeleza sera ya kuwepo kwa China moja na kuunga mkono juhudi za China kuunganisha taifa. Daima hatutasahau kwamba kila China ilipohitaji uungaji mkono wa Namibia, serikali na watu wa Namibia walijitokeza kutuunga mkono bila wasiwasi. China inaona kuwa Namibia ni rafiki anayeaminika kabisa."

Mwezi Novemba mwaka jana, mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mjini Beijing na ulipata mafanikio makubwa. Rais Hu Jintao alisema dhamira ya ziara yake ni kujadiliana na viongozi wa Namibia namna ya kutekeleza mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo. Ili kuisaidia Namibia iendeleze uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, rais Hu Jintao alitangaza hatua kadhaa za serikali ya China kuisaidia nchi hiyo, alisema,

"Serikali ya China imeamua kuipatia Namibia msaada wa kifedha na mikopo isiyo na riba na katika muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2007 hadi 2009, serikali ya China itaipatia Namibia mkopo wenye masharti nafuu wa yuan bilioni moja na mkopo wa bidhaa wenye thamani ya dola za kimarekani milioni mia moja."

Pamoja na hatua hizo, serikali ya China itaendelea kuhamasisha makampuni ya China yenye uwezo mkubwa kuwekeza nchini Namibia na kushirikiana na makampuni ya Namibia katika sekta za biashara, miundombinu na kilimo, na kuchukua hatua za kuzidi kununua bidhaa za Namibia ili kusawazisha urali wa kibiashara. Serikali ya China itaisaidia Namibia kuanzisha kituo cha kutoa mafunzo ya kazi, kujenga hospitali, kutuma watu wanaojitolea na kuisaidia Namibia katika sekta ya teknolojia ya mawasiliano ya habari.

Rais Hifikepunye Pohamba alisema, watu wa Namibia hawatasahau kwamba serikali na watu wa China siku zote walisimama pamoja na watu wa Namibia katika miaka ya kupigania uhuru na wako pamoja katika miaka ya kuendeleza uchumi. Watu wa Namibia wanathamini urafiki kati ya Namibia na China na kutaka kuendeleza kwa kina zaidi ushirikiano unaonufaisha pande mbili. Alisisitiza,

"Serikali ya Namibia inaunga mkono sera ya China moja tu, na Taiwan ni sehemu isiyoweza kutengeka ya China, serikali ya Namibia inaunga mkono juhudi za China kwa ajili ya kulinda mamlaka ya taifa na ukamilifu wa ardhi, na kuunga mkono juhudi za umoja wa taifa la China."

Idhaa ya kiswahili 2007-02-06