Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-06 15:15:29    
Barua0206

cri

Msikilizaji wetu Jendeka Godah wa Bungoma Kenya ametutumia barua pepe hivi karibuni alipongeza kwa kazi tunayofanya usiku na mchana. Kulingana na habari au ujumbe alioupata kutoka kwa Bwana Ayub Shariff Mutanda kuwa katika idhaa ya kiswahili kuna wafanyakazi wachache ili hali kazi ni nyingi mara kwa mara inatulazimu kufanya kazi mpaka usiku. Bw. Mutanda alisema yeye alishuhudia hayo mwenyewe alipokuwa Beijing mwaka jana.

Anasema angependa kutushukuru wote tuliomkaribisha Bwana

Shariff na kupata zawadi abmazo aliwafikishia wenzake. Vilevile anaiunga mkono Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa kurefusha muda wa mama Chen kustaafu. Kwa kweli anastahili hiyo heshima, yeye pamoja na wasikilizaji wengine wamefurahia uamuzi huo.

Ujumbe wmignine unatoka kwa Bwana Ayub Shariff ambaye aliwasiliana naye kwa njia ya simu kuwa kama ana uwezo wa kufungua tovuti anaweza kumtakia mama Chen heri na fanaka kwa muda ambao ameongezewa kwa sasa. Bwana Mutanda yuko na shughuli vijijini ambapo hawawezi kutembelea tovuti na wala hakuna umeme. Lakini alisema kuwa yeye alifurahia juhudi ambazo mama Chen alikutana na Bwana Mbaruok Msabah huko Dubai, Oman katika njia ya ujumbe wa CRI ya kuelekea Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Kutokana na rikodi wamesikia mama Chen akimhoji kinaga ubaga Bwana Mbarouk, wanaona wametiwa mori na kujivunia idhaa ya Kiswahili ya CRI kuwajali sana wasikilizaji wake.

Tunamshukuru sana Bibi Jendeka Goldan kwa barua yake ya kutufurahia kwamba imetuambia habari kuhusu Bwana Mtanda Ayub Shariff baada ya kurudi nyumbani, ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kwa barua, tunatumai kuwa mtaendelea kutusikiliza na kutoa maoni na mapendekezo yenu ili tuboreshe kwa pamoja matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Ramadhani Kiyungilo wa S.L.B 799 Kahama- Shinyanga nchini Tanzania ametuletea barua, kwanza kabisa akitusilimu watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio china kimataifa, anatumaini kuwa wote ni wazima tukiwa tunaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa la China. Anasema ana furaha tele kuwasiliana tena na Radio China kimataifa akiwa na ombi moja ambalo anapenda lifanyiwe kazi. Yeye anaiomba radio china kimataifa iwe inachapisha vitabu vya historia na kuwatumia wasikilizaji kwa ajili ya kuvisoma na baadaye waweze kuulizwa maswali yanatokana na vitabu hivyo.

Sababu iliyomsukuma kutoa maoni hayo, ni kutokana na yeye pamoja na wasikilizaji wengine kuwa ni wanafunzi wa bweni, hivyo inakuwa vigumu sana kwao kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa mara kwa mara. Kwani sheria za shule haziruhusu wanafunzi kusikiliza radio shuleni.

Mwisho anasema kwa vile Radio China Kimataifa inawajali wasikilizaji wake, anatumaini kuwa maoni yake yatayafanyiwa kazi, na mazingira yakiruhusu maoni yake yanaweza kutekelezwa. Anamaliza barua yake kwa kusema yeye na wanafunzi wenzake wanaipenda radio China kimataifa, na wanatutakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa heri na baraka katika kazi za kila siku.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Ramadhani Kiyungilo kwa barua yake na kutoa maoni na pendekezo lake. Tunapenda kumjulisha wewe na wasikilizaji wengine kuwa, Radio China kimataifa inafanya juhudi za kutafuta ushirikiano na Radio Tanzania Dar es Salaam na Radio Tanzania Zanzibar ili matangazo yetu yaweze kurushwa hewani moja kwa moja kwa kupitia radio hizo, tuna imani kuwa, juhudi zetu zitapata mafanikio si muda mrefu ujao, na wasikilizaji wetu hakika watapata usikivu mzuri katika wakati unaofaa. Msiwe na wasiwasi tunaendelea na juhudi.

Msikilizaji wetu Mchana J. Mchana wa S.L.B 1878 Morogoro nchini Tanzania, katika barua yake leo anapenda kuungana na wasomaji wa gazeti la daraja la urafiki kutoa maoni machache anayoyafahamu kuhusu China. Anasema China ni nchi yenye sera ya usawa, na ukweli huu umejidhihirisha pale Korea ya kaskazini ilipofanya majaribio ya makombora ya nyuklia mwaka 2006. Anasema China ilitaka jumuiya ya kimataifa isiwekee vikwazo Korea ya kaskazini bali jitahada zifanywe ili tofauti zilizopo zitatuliwe, hii inaonesha wazi jinsi sera za kidiplomasia za China zilivyo na usawa.

Bwana mchana anaamini kuwa sheria 480 zilizotungwa zinatekelezeka, na ndio maana nchi za magharibi zinajaribu kupotosha ukweli wa mambo, China haiwezi wala haitarajii kuleta ukoloni mamboleo Afrika, anaendela kusema kuna usemi wa Kiswahili usemao umdhaniaye ndiyo kumbe siye.

Msikilizaji wetu huyu anaendelea kusema kuwa, Nchi za magharibi zilidhani kuwa China haiwezi, kumbe inaweza na ipo mstari wa mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika. Kwa upande wake anaiona China kama mkombozi kwa Afrika na dunia nzima, anaipongeza China kwa maamuzi yake yenye kuona mbali zaidi, na Anamaliza barua yake kwa kusema, Hongera China.

Tunamshukuru sana Mchana J. Mchana kwa barua yake, ingawa ni fupi lakini ametoa maoni ya usikivu wake kuhusu matangazo yetu, tunafurahi kuona kuwa aliyoandika yameonesha ufuatiliaji wake wa karibu wa matangazo yetu.

Bw Erickson Rumbagi wa S.L.B 277 Maswa-Shinyanga nchini Tanzania ametuletea barua akiwasalimu marafiki zake wapendwa wa Radio China Kimataifa, na kumshukuru Mungu kwa kuwazeshesha wote kuwa wazima hadi wakati huo alipokuwa anaandika barua. Msikilizaji huyu anasema, kutoka na sheria za shule ya Bupandagilia anayosoma kutoruhusu wanafunzi kusikiliza radio, inamuwia vigumu kuweza kusikiliza vipindi vya Radio China kimataifa kila siku, ni wakati wa likizo tu ndio huwa anapata fursa nzuri ya kuisikiliza idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Kwenye barua yake pia anapenda kuishauri Radio China Kimataifa irushe matangazo yake kupitia Radio Free Afrika ya Mwanza, ambayo inasikika nchi nzima ya Tanzania na nje ya nchi kwa masafa ya FM na ya kati, hatua hii anaamini itaweza kuboresha zaidi usikivu wa matangazo ya CRI.

Vilevile anaishukuru CRI kwa utoaji wake habari unaokwenda na wakati na kulenga hali halisi ya jamii. Mwisho anawatakia wafanyakazi wote wa CRI heri na baraka tele akiamini kuwa tutamuombea vyema ili aweze kufaulu katika mitihani yake ya kidato cha nne. Na pia anaamini kuwa upendo, amani, umoja na ushirikiano vitaisaidia kuboresha matangazo ya Radio China Kimataifa

Tunamshukuru msikilizaji wetu Erickson Rumbagi kwa barua yake, kama tulivyosema mwanzo juhudi zetu kuhusu kuboresha usikivu wa matangazo yetu bado zinaendelea, vilevile tunapenda kumwombea kila la heri ili aweze kupata mafanikio katika masomo yake.

Msikilizaji wetu Gabriel Simiyu Wekesa anayetunziwa barua zake na Mutanda Ayub wa S.L.B 292 Kimilili nchini Kenya. Anawasalimu sana watangazaji na wafanyakazi wote wa radio China kimataifa, binafsi amefurahishwa sana kujumuishwa katika shindano la chemsha bongo la "mimi na radio china kimataifa". Anaomba kwamba asisahauliwe katika shindano lolote katika siku za usoni, vijana wa kijini kilimahewa ni wapenzi sana wa CRI, na ukifika muda wa matangazo ya CRI wote huisikiliza na tayari wameanzisha club yao ya "mimi na Radio China Kimataifa" kijijini kilimahewa, pia wanapenda sana kujinfunza kichina na kutuma card za salamu.

Ombi lake ni kuwa, radio china kimataifa iwe inawatembelea wasikilizaji wa nchini Kenya ili kuzidi kudumisha zaidi uhusiano na urafiki, na yeye anapenda sana kuitembelea China, na kabla ya kukamilisha barua yake, anasema angependa kuwakumbuka wafuatao:

? Winnie Kakila simiyu akiwa Bungoma nchini Kenya

? Boaz, Norah, Lydia, Magdalena, na Lameck wote wakiwa huko Kilimahewa, Bungoma nchini Kenya

? Papa Johnstone Wanelongo na mama Zinah Mutoro wakiwa Kilimahewa, Bungoma nchini Kenya

? Ayub Mutanda na mke wake wakiwa Bungoma nchini Kenya

? Mjomba Ifraim Sisungo akiwa Naitiri-Bungoma nchini Kenya

? Mwibandi Mukwama wa shule ya sekondari Kibabi, Bungoma nchini Kenya

? Wamtu Musamil akiwa Siknana nchini Uganda

? Babu yake Muichwana na nyanya zake Nafula, Joina na Zaina wakiwa Shule ya msingi Misimo,, hakuwasahau pia bibi zake wengine, Webuye, Lukusi, zusi Nanjala na Eliza waote kwa pamoja wakiwa Bungoma nchini Kenya

? Pia anawakumbuka Anthony,Jeremia, Libanisa, Amosi, Peter, Aizaki na Juma Wekesa wakiwa Kitale nchini Kenya

? Na mwisho anawasalimu Caral Okoyo, Luichuna na Ezra Simiyu wa Kitale nchini Kenya

Wote hawa anawataka wasikilize Radio China Kimataifa ili wafahamu mengi kuhusu uchumi, kilimo na mambo ya afya nchini China.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabaha wa S.L.B 52483 Dubai Falme za Kiarabu ametuletea barua akipenda kuchukua fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa marafiki zake wa Jamhuri ya watu wa China kwa kuharakisha maandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008. Anasema bila shaka kipindi hiki kifupi kilichobaki kabla ya michezo hiyo kufanyika ni kipindi cha harakati na shamrashamra nyingi katika miji mbalimbali ya China, ili kujiandaa kuikaribisha michezo ya Olimpiki na hasa katika mji wa Beijing.

Yeye kama msikilizaji wa Radio China kimataifa na rafiki mkubwa wa Jamhuri ya watu wa china anaona fahari kubwa kwa juhudi zinazochokuliwa na serikali ya China katika maandalizi ya Tamasha kubwa kabisa la michezo ya Olimpiki. Ni matumaini yake makubwa kuwa radio china kimataifa haitawaacha nyuma wasiklizaji wake kwa kuandaa chemsha bongo inayohusu michezo ya Olimpiki na washindi wake waweze kupata nafasi ya kushuhudia michezo hiyo jijini Beijing.

Tunamshukuru sana Bw Mbarouk kwa barua yake nzuri, n kweli maandalizi ya michezo ya Olimpiki yanaendelea kama kawaida, ujenzi wa viwanja uko katika hatua za mwisho mwisho. Na kuhusu shindalo la Chemsha bongo, litaendelea kuwepo kila mwaka kama kawaida, tunawakumbusha wasikilizaji wasisahau kushiriki.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-06