Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-06 15:57:55    
China yahimiza ujenzi wa nyumba ndogo na za wastani ili kutatua tatizo la nyumba kwa wakazi wenye mapato ya chini

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi wa China na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya watu, wananchi wa China wamekuwa na mahitaji makubwa ya nyumba. Lakini kwa nchi kama ya China, ambayo ina idadi kubwa ya watu na upungufu wa ardhi, mahitaji makubwa ya nyumba kwa ajili ya makazi yanazidisha upungufu wa ardhi ya kujenga nyumba kwenye miji, na kufanya familia nyingi zenye pato dogo na la wastani kushindwa kumudu gharama ya nyumba. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China ilibuni sera mpya za nyumba kwa wakazi, zikiagiza kuwa mkondo wa ujenzi wa nyumba za wakazi wa mijini katika siku za baadaye ni nyumba ndogo na za wastani chini ya mita za mraba 90 hivi kila moja. Kutokana na maelekezo ya serikali, ujenzi wa nyumba za wakazi unaelekea kuwa wa nyumba ndogo na za wastani.

Katika nyumba moja ya kwenye ghorofa, yenye kiasi cha mita za mraba 90 na vyumba vitatu za kulala, jikoni kuna sehemu mbili za kupikia na kulia chakula, na sehemu ya kulia chakula inaungana na sebule na kuifanya ionekene kuwa kubwa zaidi. Mfano huo wa nyumba ulipata tuzo la ngazi ya pili kwenye maonesho ya usanifu wa nyumba za wakazi wa mijini uliofanyika hivi karibuni mjini Beijing. Msanifu wa nyumba hiyo, ambaye ni msanifu mkuu wa taasisi ya utafiti wa usanifu wa majengo ya Beijing, Bw. Liu Xiaozhong, alipoeleza umaalumu wa nyumba za namna hiyo, alisema,

"Kwanza nilizingatia mambo mengi muhimu, ili nafasi za nyumba hiyo zitumike kwa ufanisi zaidi. Pili, nilizingatia matumizi na mambo ambayo wakazi wanayapenda ili kutimiza mahitaji yao."

Nyumba za wastani na ndogo zinatiliwa mkazo katika sekta ya usanifu wa majengo nchini China. Sababu yake ni kuwa, kutokana na agizo la serikali ya China, kuanzia tarehe 1 mwezi Juni mwaka 2006, nyumba zenye mita za mraba chini ya 90 kila moja inatakiwa kuchukua nafasi ya zaidi ya 70% ya mahali inapojengwa.

China ni nchi yenye idadi kubwa ya watu na upungufu wa ardhi, wastani wa ardhi kwa kila mtu ni kiasi cha theluthi moja ya wastani wa ardhi wa kila mtu duniani. Pamoja na kuharakishwa kwa ujenzi wa miji, mahitaji ya nyumba kwa wakazi wa mijini yanaongezeka kwa mfululizo, lakini nyumba kubwa zinazotumia ardhi kubwa, vifaa vya chuma cha pua, maji na nishati nyingi haziambatani na kanuni za maendeleo endelevu. Naibu Kiongozi wa jumuiya ya soko la nyumba na viwanja vya nyumba, Bw. Zhu Zhongyi alisema, kuweka mkazo katika ujenzi wa nyumba za wastani na ndogo kunaambatana na kiwango halisi cha idadi ya watu, rasilimali na maendeleo ya uchumi na jamii ya China ya hivi sasa, kunachangia utatuzi wa tatizo la nyumba za kuishi kwa wakazi wa mijini na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya wakazi wa mijini. Alisema,

"Sababu ya serikali ya China kutoa wito wa kujenga nyumba nyingi zaidi za wastani na ndogo, kwanza ni kuwa kuna upungufu mkubwa wa nyumba za aina hiyo, pili ni kufikiria upungufu wa rasilimali ya ardhi nchini China, na tatu, tunajifunza uzoefu wa baadhi ya nchi zenye upungufu wa rasilimali ya ardhi, zikiwemo Japan na Korea ya Kusini, ambazo zimetunga sheria ya kudhibiti ukubwa wa nyumba za wakazi."

Utaratibu wa ugawaji nyumba uliokuwepo nchini China tokea miaka mingi iliyopita, wakazi wa China ama walikosa nyumba za kuishi au walikuwa na nyumba ndogo kupita kiasi. Mwaka 1978 wastani wa eneo la nyumba kwa kila mkazi wa mijini ulikuwa mita za mraba 7.2 tu. Katika mwisho wa karne iliyopita, serikali ya China ilianza kutekeleza utaratibu mpya wa nyumba, badala ya kuwapatia wakazi nyumba, ilitaka wanunue nyumba wao wenyewe kwenye soko la nyumba zikiwa ni pamoja na bidhaa za nyumba, nyumba za bei nafuu na nyumba za kupangisha kwa gharama ndogo kufuatana na tofauti za makundi ya watu. Njia hiyo si kama tu imestawisha soko la nyumba, bali pia inaharakisha maendeleo ya ujenzi wa nyumba za wakazi. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, wastani wa eneo la nyumba kwa kila mkazi wa mijini ulifikia mita za mraba 26.

Hata hivyo, bado kuna hali ya kukosa uwiano katika nyumba za wakazi, ambapo baadhi ya matajiri wana nyumba kubwa na anasa, wakati wakazi wengi wenye pato dogo na wastani wanashidwa hata kununua nyumba kutokana na bei ya nyumba kupanda kwa mfululizo. Bw. Zhu alisema, katika hali ya namna hiyo, serikali inatakiwa kuunga mkono ujenzi mwafaka wa nyumba, wenye uwiano na kuokoa raslimali.

"Ukubwa wa nyumba unahusiana na ugawaji wa rasilimali za umma, matajiri wasipanue bila kikomo ukubwa wa nyumba zao, na watu wenye matatizo ya kiuchumi nao pia wapate nyumba. Gharama za nyumba za wastani na ndogo, ni ndogo kuliko nyumba kubwa, hivyo ni nafuu kwa wakazi wenye pato dogo kuzinunua."

Takwimu husika zinaonesha kuwa, hivi sasa nyumba zinazohitajiwa zaidi na wakazi wa mijini, ni nyumba za wastani na ndogo. Katika miji mikubwa na ya wastani, kiasi cha nusu ya familia zinazofikiria kununua nyumba, zinataka kununua nyumba zenye ukubwa wa chini ya mita za mraba 90. Lakini tatizo lililopo hivi sasa kwenye soko la nyumba ni kuwa nyumba za wastani na ndogo ni chache sana. Kwa upande mmoja, watu wenye pato dogo wanashindwa kununua nyumba; kwa upande mwingine nyumba kubwa za hali ya juu zimekuwa nyingi kuliko mahitaji.

Bw. Yu Qiping alimaliza masomo ya chuo kikuu miaka miwili iliyopita, hivi sasa anafanya kazi katika kampuni moja ya teknolojia ya mawasiliano ya habari mjini Beijing. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, ameshindwa kabisa kununua nyumba anayoweza kumudu. Alisema,

"Nyumba zilizoko mjini Beijing, nyingi ni kubwa, na nyumba zilizo ndogo ni chache sana, hata nyumba moja yenye vyumba viwili vya kulala iliyoko kwenye ghorofa ni yenye mita za mraba zaidi ya 100. Bei ya nyumba katika mji wa Beijing inapanda mwaka hadi mwaka, acha nyumba zile zilizoko katikati ya mji, hata bei ya nyumba zilizoko katika viunga vilivyoko mbali na mji imefikia Yuan elfu 7 au 8 kwa mita 1 ya mraba, mtu kama mimi anayepata mshahara Yuan elfu 3 au 4 hivi, kabisa hana uwezo wa kununua nyumba."

Kuna watu wengi kama Bw. Yu Qiping, ambao wana shida ya kununua nyumba. Lakini katika siku za baadaye serikali ya China itatoa sera husika za kutoza malipo kwa wakazi wenye nyumba kubwa. Hivi sasa wizara ya ujenzi inabuni kigezo cha usanifu wa nyumba zenye ukubwa wa chini ya mita za mraba 90, kuongeza ufanisi wa matumizi ya nyumba za aina hiyo ili kufanya wakazi wa nyumba hizo waone raha na wasipatwe na matatizo katika maisha yao.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-06