Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-08 15:33:41    
Juhudi za China kujenga jamii yenye masikilizano

cri

Katika juhudi za China kujenga jamii yenye masikilizano, suala moja kubwa ni hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa maendeleo kati ya miji na vijiji na kati ya sehemu mbalimbali. Ili kutatua suala hilo, serikali kuu ya China ilitenga fedha zaidi kwa serikali za sehemu ya magharibi iliyopo nyuma kimaendeleo, na kuweka mkazo katika kuendeleza sehemu ya magharibi na sehemu ya kaskazini mashariki ambayo ina viwanda vingi vikubwa vinavyopaswa kufanyiwa mageuzi.

Serikali pia ilitoa sera ya kuwasaidia wananchi wa China wa makabila madogomadogo wanaoishi katika sehemu za milimani zilizopo mbali na miji. Naibu mkuu wa idara ya uchumi iliyo chini ya kamati ya mambo ya kikabila ya taifa ya China Bw. Le Changhong alieleza kuwa, katika miaka mitano ijayo serikali itatenga Yuan bilioni moja, sawa na dola za kimarekani milioni 120 katika kuboresha maisha ya wananchi wa makabila madogomadogo yenye watu wasiozidi laki moja. Na serikali ina mpango wa kuongeza fedha hizo katika siku za baadaye. Alisema "Sambamba na kuimarika kwa uwezo wa taifa, tutajaribu kutenga fedha nyingi zaidi katika sehemu wanakoishi watu wa makabila madogomadogo. Vile vile tutazihamasisha sehemu zenye maendeleo ya kiuchumi zitilie mkazo zaidi kuzisaidia sehemu wanakoishi watu wa makabila madogomadogo yenye watu wachache zaidi, na kuwahamasisha wananchi wa hali mbalimbali wasaidie ndugu wa makabila hayo."

Wizara ya kilimo ya China pia iliandaa mpango kabambe wa kuendeleza vijiji vya sehemu ya magharibi ya China iliyoko nyuma kimaendeleo. Katika mpango huo serikali itavisaidia vijiji hivyo viendeleze zaidi uzalishaji wa mali unaolingana na hali halisi ya huko, ili kuharakisha maendeleo ya vijiji vya sehemu hiyo na kupunguza pengo la maendeleo kati ya sehemu ya magharibi na ya mashariki ya China.

Zaidi ya hayo serikali ya China imetoa sera na hatua mbalimbali za kuimarisha ujenzi katika mambo mengine, kwa mfano kutunga sheria zinazolinda maslahi halali ya wananchi, kukamilisha mfumo wa elimu na kuinua sifa za wananchi, kuimarisha mfumo wa utoaji huduma kwa jamii na kutilia mkazo katika shughuli za kulinda mazingira.

Mafanikio ya mwanzo yamepatikana katika utekelezaji wa sera na hatua hizo. Mzee Zhuang Yuehui anaishi katika mtaa wa makazi uitwao Lugu, mjini Beijing, ni mwanajeshi mstaafu mwenye umri wa miaka 77. Mzee huyo amenufaika na hatua hizo. Siku kadhaa zilizopita alipata kiinua mgongo ambayo imeongezeka kwa Yuan zaidi ya mia mbili. Mzee Zhuang alisema  "Nafurahi sana. Pesa za kiinua mgongo zimeongezeka, kwa hiyo tunaweza kuishi maisha mazuri zaidi ya uzeeni, na kuwa na uwezo mkubwa zaidi. Naridhika na maisha ya sasa, kila kitu ni shwari, fedha hizo za ziada zinaweza kuboresha na kuinua kiwango cha maisha ya sasa."

Kwa wakazi wa mijini, wamenufaika na ongezeko la namna hii katika mambo mbalimbali. Kwa mfano wa mji wa Beijing, kuanzia mwaka huu viwango vyote vya utoaji fedha zinazohusiana na huduma za jamii vimepanda juu, kama vile pensheni za wastaafu, mshahara wa msingi wa wafanyakazi, bima ya kukosa ajira na pensheni kwa watu waliojeruhiwa kazini.

Katika sehemu za vijijini, wakulima pia wamenufaika na juhudi za kujenga jamii yenye masikilizano. Katika mji mdogo wa Shiwei, kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani uliopo kaskazini mwa China, mzee Lina mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 na jamaa zake walipata msaada wa fedha wa serikali na kuanzisha shughuli za utalii. Katika nusu ya pili ya mwaka 2006 kipato cha familia hiyo kiliongezeka kwa Yuan elfu 50 hadi 60 kuliko mwaka 2005 kipindi kama hicho. Hivi sasa mzee Lina na jamaa zake wanaandaa shughuli za kusherehekea mwaka mpya wa jadi wa Kichina. Mzee huyo alieleza kuwa, hivi sasa maisha yanaboreshwa siku hadi siku.

Alisema "Jamii ya hivi sasa ni nzuri sana. Watoto wangu wana bahati nzuri kuishi katika jamii hii nzuri zaidi kuliko ile ya zamani."

Profesa Wu Zhongmin wa chuo cha chama cha kikomunisti cha China alisema, serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kutimiza lengo la kujenga jamii yenye masikilizano, hii inaonesha kuwa China inazingatia kuleta uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi na kulinda haki za wananchi wa hali mbalimbali. Alisema "Taifa linasisitiza kuwa wananchi wote wanastahili kunufaika na mafanikio ya mageuzi na maendeleo, hivi sasa suala la kulinda haki za wananchi wa hali mbalimbali linatiliwa mkazo zaidi. Hayo ni maendeleo yaliyopatikana nchini China."

Idhaa ya kiswahili 2007-02-08