Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-09 16:06:07    
Uhimizaji wa makampuni binafsi ya China kuwekeza katika nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo za Afrika

cri

Ni rahisi zaidi kwa makampuni binafsi ya China kuwekeza vitega uchumi kwenye nchi za Afrika zisizokuwa na rasilimali nyingi na soko ndogo, kuliko makampuni makubwa na ya wastani ya kitaifa kutokana na kuwa makampuni binafsi yana utaratibu wenye unyumbufu zaidi, wanakampuni binafsi wanaweza kufanya uamuzi haraka, na kutumia mitaji yao kama wanavyopenda. Hivyo makampuni hayo yanaweza kutoa mchango mkubwa zaidi katika kutekeleza "sera ya kuanzisha shughuli" katika nchi hizo za Afrika.

Lesotho ni nchi ndogo iliyoko kwenye uwanda wa juu katika sehemu ya ndani ya kusini mwa Afrika, ina idadi ya watu milioni mbili na eneo kilomita za mraba elfu 30, haina rasilimali nyingi za nishati na madini na soko lake ni ndogo. Hivi sasa makampuni mengi ya China yanayowekeza nchini Lesotho ni makampuni binafsi, ambayo yanashughulikia utengenezaji wa bidhaa kutokana na chuma cha pua, usagaji wa mawe yaliyofaa kwa tarazo, ufumaji wa nguo, utengenezaji wa vyombo vya karatasi, vyombo vya plastiki, na samani. Kiwango cha uwekezaji wa makampuni hayo ni kidogo, lakini yana ufanisi mzuri.

Ili kustawisha sekta ya uzalishaji bidhaa na kuongeza nafasi za ajira, serikali ya Lesotho inahitaji sana uwekezaji kutoka China. Wizara ya biashara ya China imechukua hatua nyingi kuhimiza makampuni ya China kuwekeza nchini Lesotho, kama vile kushirikiana na upande wa Lesotho kufanya shughuli za kuwavutia wafanyabiashara wa China kuwekeza nchini Lesotho, kuwahamasisha wanakampuni wa China kufanya ukaguzi wa kibiashara na kuwekeza nchini Lesotho, lakini si rahisi kuyashawishi makampuni makubwa na wastani ya kitaifa ya China kuwekeza nchini Lesotho kutokana na soko dogo na upungufu wa rasilimali.

Kuwekeza vitega uchumi kwenye sekta za maliasili ni kazi kubwa katika ushirikiano kati ya China na Afrika. Ingawa nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo za Afrika hazina raslimali nyingi zilizo muhimu duniani, lakini bado zina fursa nyingine za uwekezaji katika uendelezaji wa maliasili za sekta hiyo, tena uwekezaji wa aina hiyo hauhitaji fedha nyingi katika hatua ya mwanzo, hivyo ni chaguo zuri la uwekezaji kwa makampuni binafsi ya China. Kwa mfano Lesotho ina mawe mengi yanayofaa kwa tarazo, mawe yenyewe hayana thamani kubwa, lakini baada ya kampuni moja ya China kupeleka zana zilizotengenezwa nchini China zenye teknolojia ya juu, kuyasaga na kuyasugua mawe hayo kuwa tarazo zinazotumiwa katika ujenzi wa nyumba, mawe hayo yaliongezwa thamani. Bidhaa zinazotengenezwa kutokana na mawe hayo zinauzwa na kupendwa sana katika nchi mbalimbali za jumuiya ya soko la pamoja la nchi za kusini mwa Afrika COMESA.

Uwekezaji wa makampuni binafsi ya China katika nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo unatakiwa kufuata mahitaji ya soko, na kuzingatia lengo la kunufaishana ili kuhakikisha maendeleo endelevu. Kwa kawaida, uwekezaji huwa unafanyika zaidi kwenye sekta zenye faida kubwa, Kuwekeza katika nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo urahisi ni kupata kibali cha kuanzisha miradi, hakuna kikomo cha kiasi cha mitaji inayowekezwa, kuna hatari ndogo na ufanisi mzuri, hivyo inafaa zaidi kwa makampuni madogo binafsi kuwekeza katika nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo za Afrika.

Wanakampuni binafsi wa China wanaowekeza katika nchi za nje wanaweza kulimbikiza mitaji huku wakiendesha shughuli, baada ya kufahamu sera na utaratibu husika na kuzoea mazingira ya uwekezaji ya nchi wanazokuwepo, wanajua namna ya kutumia fursa nzuri ya kibiashara na kuongeza uwekezaji hatua kwa hatua. Miradi mingi yenye mafanikio iliyowekezwa na wanakampuni wa China nchini Lesotho ni wachina binafsi waishio nchini humo, japokuwa mwanzoni wanakuwa hawana fedha nyingi, lakini miradi yao yote inafanikiwa, baadhi ya makampuni ya China yamekuwa na mali zisizohamishika ambazo thamani yake ni kubwa.

Kwa ujumla kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi ndogo na zilizo nyuma kimaendeleo za Afrika ni mahitaji ya sera ya kidiplomasia ya China na mkakati wa kiuchumi wa China.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-09