Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-09 21:02:43    
Mahojiano na rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin Mkapa

cri

Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alifanya mahojiano na rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin Mkapa aliyekuwa nchini China kuhudhulia mkutano wa kituo cha kusini kinachohimiza uhusiano kati ya nchi za kusini.

Alipozungumzia uhusiano kati ya China na nchi za Afrika mheshimiwa Mkapa alisema, uhusiano uliopo kati ya China na Afrika ni mzuri sana na mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana mwezi Novemba uliangalia namna uhusiano huo unavyoweza kuimarishwa. Katika mkutano huo, wakuu wa nchi za Afrika na China hawakuangalia ushirikiano wa kisiasa tu bali pia waliangalia jinsi biashara na uwekezaji unavyoweza kuongezwa zaidi kati ya pande mbili, na pia ulitoa tamko muhimu linaloashiria kasi kubwa ya uwekezaji na biashara kati ya pande hizi mbili, vilevile upeo mkubwa zaidi wa uwekezaji kati ya makampuni ya China na ya nchi za Afrika.

Mh Mkapa pia alikuwa na maoni yake kuhusu tuhuma zinazotolewa na nchi za magharibi kuwa China inaendeleza ukoloni mamboleo barani Afrika, Mh Mkapa alisema, "kama kuna ukoloni mamboleo hivi sasa barani Afrika basi ni ukoloni mamboleo wa nchi za magharibi na sio wa China. Kwa sababu ni nchi za magharibi ambazo zilikuwa wakoloni wa nchi za Afrika, ndizo zilizotawala na kutengeneza mfumo wa kiuchumi kati ya nchi zao na nchi za kiafrika kwa muda mrefu na waliandaa na kudhibiti uhusiano huo bila ya kujali uhuru wa nchi za Afrika, uhuru wa waafrika na bila kujali haki za msingi za waafrika. Sasa nchi za kiafrika zimekuwa huru na zinaamua kutafuta mahusiano na nchi ambazo hazikuwatawala huko nyuma ikiwemo China, hivyo nchi za magharibi zinaona kama fursa zilizokuwa nazo za kupata rasilimali za kiafrika zinatishiwa, na huo ni utiaji chumvi wa uhusiano katika ya Afrika na China".

Akiongelea kuhusu tatizo la uwekezaji wa China barani Afrika hasa katika sekta ya mafuta na madini, Mheshimiwa Mkapa alisema, tatizo analoliona yeye ni kuwa, nchi za kiafrika bado hazijawa na utayari wa kuingia ubia na wawekezaji wa China, ndio maana nchi nyingi za Afrika zinafikiri kuwa zinavamiwa, Mheshimiwa Mkapa aliongeza kuwa, ni lazima nchi za kiafrika ziwe na wataalamu na wajasiriamali wanaoweza kufanya mazungumzo ya dhati na wajasiriamali wa China ili kuweza kuwa na makampuni ya ubia. Kwa hiyo changamoto ni kwa nchi za Afrika sasa kufungua mlango wa ujasiriamali katika mahusiano ya kiuchumi na dunia hii mpya ya sasa ya utawandazi.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya kati ya China na Tanzania na hasa katika tiba ya jadi ya kichina, Mheshimiwa Mkapa alieleza kufurahiswa kwake na ushirikiano huo na hasa China inavyojitahidi kushirikiana na Tanzania ili kuweza kuona kama Tanzania inaweza kuwa na medani mpya ya matumizi ya dawa za asili. Katika tamko la mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, serikali ya China ilisema haitaleta wataalam tu bali pia watasaidia ujenzi wa hospitali kama za rufaa katika maeneo mbalimbali kama vile ya magharibi, mashariki, na kusini mwa Afrika wakishirikiana na nchi husika. Kwa hivyo kwa upande wa dawa, tiba na udhamini wa wanafunzi wa kiafrika kuja kusoma nchini China, serikali ya China inazisaidia sana nchi za Afrika. Mheshimiwa Mkapa alisema,

"mimi mwenyewe nilishawahi kupata tiba ya kichina wakati naugua ugonjwa wa baridi yabisi, na kwa kweli tiba hiyo ilinisaidia sana kabla sijaenda kufanyiwa operesheni barani Ulaya"

Akieleza kuhusu mkutano wa mahusiano kati ya nchi za kusini ambao kwa mara ya kwanza umefanyika nchini China, Mheshimiwa Mkapa aliishukuru China kwa kuandaa mkutano huo. Alisema "mapato ya kituo cha kusini yanatokana na michango ya wanachama wa nchi zilizoko kusini pamoja na China, kituo hicho bado ni kichanga na hakijajijenga kiasi cha kutosha. Kwa hiyo gharama za mikutano yake ni kubwa, licha ya kuwasafirsha wajumbe wa bodi yake kutoka mabara mbalimbali ya Asia, Afrika na Latin Amerika, na gharama za kufanyia mikutano pale Geneva ni kubwa. Ili kuthibitisha uungaji mkono wa shughuli za kituo cha kusini, serikali ya China ilitualika kuja kufanyia mkutano kwa maana ya kupunguza gharama".

Idhaa ya Kiswahili 2007-02-09