Rais Hu Jintao wa China amemaliza ziara rasmi katika nchi 8 za Afrika. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ziara hiyo barani Afrika ni ziara ya urafiki na ushirikiano, ni tukio kubwa linalohusu uhusiano kati ya China na Afrika kufuatia kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika huko Beijing. Alisema ziara hiyo itahimiza uhusiano kati ya China na Afrika uendelezwe zaidi.
Rais Hu Jintao wa China alizizuru nchi 8 zilizoko sehemu mbalimbali barani Afrika. Nchi hizo zinatofautiana katika ukubwa na hali ya maendeleo. Na ziara hiyo ni ya kwanza aliyofanya rais wa China katika nchi 6 kati ya nchi hizo 8. Katika ziara hiyo ya siku 11, rais Hu Jintao alisafiri umbali wa kilomita karibu elfu 40, kufanya mazungumzo na viongozi zaidi ya 20 wa nchi za Afrika, kukutana na watu mashuhuri mia kadhaa wa Afrika, kuhudhuria shughuli zaidi ya 90 na kutoa hotuba zaidi ya 30. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alisema ziara hiyo imepata mafanikio katika maeneo mbalimbali, hii ni ziara ya urafiki na ushirikiano.
Kuimarisha urafiki uliopo kati ya watu wa China na Afrika na kudumisha urafiki huo kizazi baada ya kizazi ni lengo moja la ziara hiyo ya rais wa China. Katika kipindi cha nusu karne iliyopita, watu wa China na Afrika walijenga urafiki mkubwa katika mapambano ya kupigania uhuru wa taifa na juhudi za kujiendeleza kiuchumi. Katika ziara hiyo, kwenye mazungumzo na watu wa hali mbalimbali wa Afrika, rais Hu Jintao alikuwa anasisitiza kuwa, watu wa China ni marafiki, wenzi na ndugu wakubwa wa watu wa Afrika, China kamwe hailazimishi nchi nyingine zikubali itikadi zake, mfumo wake wa jamii na wa maendeleo. Alisema China kamwe haifanyi jambo lolote linaloharibu nchi za Afrika na watu wa Afrika.
Lengo lingine la ziara hiyo ya rais wa China ni kutekeleza hatua 8 zilizotolewa na serikali ya China kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika huko Beijing mwezi Novemba mwaka jana, hatua hizo zikilenga kuimarisha ushirikiano wa mambo halisi kati ya China na Afrika na kuunga mkono nchi za Afrika katika juhudi za kujiendeleza. Katika ziara hiyo China na nchi hizo 8 za Afrika zilisaini nyaraka zaidi ya 50 za ushirikiano ambazo nyingine zinahusiana na utekelezaji wa makubaliano yaliyopatikana na mkutano wa Beijing. Zaidi ya hayo rais Hu Jintao wa China alitoa mapendekezo yanayolenga kupanua ushirikiano unaonufaishana kati ya China na Afrika, akisisitiza kuwa China itajitahidi kuboresha biashara na Afrika, kuongeza uwekezaji wa vitega uchumi barani Afrika, kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi wa kikazi, na kuzisaidia nchi za Afrika ili ziwe na nguvu kubwa zaidi za kujiendeleza.
Viongozi wa nchi za Afrika walieleza kuwa, China ni mwenzi mwenye uaminifu, Afrika inatarajia kuimarisha ushirikiano na China katika sekta za biashara, uwekezaji wa vitega uchumi na ujenzi wa miundombinu.
Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alisema katika zaira hiyo, China na nchi za Afrika ziliafikiana kuhusu kuimarisha urafiki na ushirikiano wa sekta zote na kuendeleza uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Afrika. Katika ziara hiyo rais Hu Jintao wa China alikuwa anarudia kwamba, China inapenda kushirikiana na Afrika, kutekeleza kwa makini makubaliano yaliyopatikana na mkutano wa Beijing, kuimarisha uaminifu wa kisiasa, kupanua wigo wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kuongeza maingiliano ya utamaduni, kuimarisha ushirikiano katika mambo ya kimataifa ili kuendeleza zaidi uhusiano kati ya pande hizo mbili. Rais wa China alipendekeza kuwa China na Afrika zinatakiwa kuimarisha mawasiliano na kufundishana, kuhimiza maendeleo ya pamoja, kusimama kwenye mstari mmoja katika kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea, na kutoa mchango katika juhudi za kujenga dunia yenye masikilizano, amani ya kudumu na ustawi wa pamoja. Viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika walieleza kufurahia mapendekezo aliyotoa rais Hu Jintao wa China kuhusu jinsi ya kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika, walisema kuimarisha uhusiano na China ni chaguo la kimkakati la nchi za Afrika ambalo linalingana na hali ya hivi sasa na maslahi ya msingi ya watu wa Afrika.
Katika ziara hiyo rais Hu Jintao wa China pia alirudia msimamo wa China kuhusu masuala yanayofuatiliwa na jumuiya ya kimataifa, likiwemo suala la Darfur ya Sudan. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alisema hii inaonesha kuwa China ina moyo wa dhati na imechukua hatua halisi katika kuunga mkono juhudi za kuleta amani na utulivu barani humo, pia China inaunga mkono juhudi za nchi za Afrika za kulinda mshikamano, kufufua Afrika na kuleta amani ya kuduma na maendeleo endelevu.
Bw. Li Zhaoxing alisema ziara hiyo inaonesha kuwa, China inayo jiendeleza kwa kufuata njia ya amani, yenye masikilizano na kisayansi ni nguvu muhimu ya kuhimiza amani na maendeleo duniani, na watu wa China watatoa mchango mpya kwa ajili ya ustaarabu na maendeleo ya binadamu.
|