Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-11 18:14:17    
Rais Hu Jintao wa China amaliza ziara ya urafiki na ushirikiano barani Afrika

cri

Rais Hu Jintao wa China amemaliza ziara rasmi katika nchi 8 za Afrika, na kuondoka Shelisheli usiku wa tarehe 10 kurudi nyumbani China. Rais Hu Jintao ameeleza kufurahia mafanikio yaliyopatikana na ziara hiyo.

Katika siku 11 zilizopita rais Hu Jintao wa China alifanya ziara rasmi katika nchi 8 barani Afrika zikiwemo Cameroon, Liberia, Sudan, Zambia, Namibia, Afrika Kusini, Msumbiji na Shelisheli. Alipozungumzia ziara hiyo rais Hu Jintao alisema "Nimezuru nchi 8 za Afrika ndani ya siku 11, ambapo nilikutana na kufanya mazungumzo na wakuu na viongozi wa nchi hizo 8, tulibadilishana maoni kwa kina na kuafikiana kuhusu jinsi ya kukuza uhusiano wa pande mbili mbili, jinsi ya kutekeleza makubaliano yaliyopatikana na mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Beijing, na masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na nchi zetu. Katika ziara hiyo China na nchi hizo 8 za Afrika zilisaini nyaraka mbalimbali za ushirikiano zinazohusu sekta za uchumi na biashara, utamaduni, afya na kilimo. Aidha nilitoa hotuba kwenye chuo kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini, nikizishauri China na Afrika ziongeze mawasiliano kati ya vijana, kuimarisha urafiki uliopo na kupanua ushirikiano wa mambo halisi, ili kukuza uhusiano mpya wa kiwenzi wa kimkakati kati ya China na Afrika. Ziara hiyo imepata mafanikio makubwa."

Rais Hu Jintao wa China amefanya ziara yake ya kwanza nje ya China barani Afrika mwanzoni mwa mwaka huu. Nchi hizo 8 za Afrika alizozuru kila moja ina umaalumu wake, ina hali tofauti na utamaduni wake, hata hivyo zote zina moyo wa dhati wa kukuza urafiki kati ya China na Afrika. Katika nchi hizo rais Hu Jintao alikaribishwa kwa ukarimu mkubwa.

Katika ziara hiyo rais Hu Jintao alitangaza mlolongo wa hatua na mipango kuhusu kusamehe madeni ya nchi za Afrika, kuongeza aina za bidhaa za Afrika zinazofutiwa ushuru wa forodha na China, misaada ya kujenga shule za vijijini na vituo vya kutoa mafunzo ya ufundi wa kazi, kuanzishwa kwa kituo cha mfano cha teknolojia za kilimo, uzinduzi wa eneo la kwanza la maendeleo ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika barani Afrika, na ujenzi wa uwanja wa michezo. Hayo yote yameonesha kuwa China inatekeleza kwa makini ahadi ilizotoa kuhusu kukuza ushirikiano kati yake na Afrika.

Katika juhudi za kuhimiza hali ya uwiano wa biashara kati ya China na Afrika, rais Hu Jintao wa China aliweka bayana kuwa, serikali ya China haifurahii mbinu inayotumiwa na viwanda na kampuni za China ya kusafirisha nje kwa wingi bidhaa za China kwa lengo la kupata masoko makubwa zaidi ya nchi za kigeni. Alisema badala yake China itaongeza kununua bidhaa za Afrika, kusamehe na kupunguza kwa kiasi kikubwa ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa za Afrika ili kutatua masuala ya kibiashara yanayofuatiliwa na nchi kadhaa za Afrika.

Viongozi wa nchi hizo 8 za Afrika walitoa pongezi kwa uhusiano kati ya Afrika na China, na uhusiano kati ya nchi hizo na China, wakisema ziara hiyo ya Rais wa China "ina umuhimu mkubwa wa kihistoria", "China ni rafiki wa Afrika", "mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya nchi na nchi", na "China kufuatilia Afrika na kufanya ushirikiano na Afrika kuna maana kubwa katika kuendeleza uchumi wa Afrika."

Rais Hu Jintao alieleza maoni yake kuhusu urafiki kati ya China na Afrika. Alisema "Katika siku zilizopita, hivi sasa na siku zijazo, watu wa China na watu wa Afrika siku zote ni marafiki wakubwa wenye usawa, wanaoaminiana, na wanaotendana kwa moyo wa dhati, ni wenzi wakubwa wanaonufaishana, wanaofanya ushirikiano na wanaopata maendeleo kwa pamoja, vile vile ni ndugu wakubwa wa dhiki na faraja. Watu wa China na Afrika wanapaswa kudumisha urafiki huo kizazi baada ya kizazi, na kwa uhakika lengo hilo litatimizwa."