Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-12 15:40:32    
Filamu za kibiashara na za kisanaa zote zaongoza katika soko la filamu nchini China

cri

Filamu ya "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" iliyopigwa chini ya uelekezaji wa Zhang Yimou, mwongoza filamu maarufu wa China, imepata mapato makubwa katika mwezi mmoja tokea ianze kuoneshwa nchini China na nchi za nje, na filamu nyingine za kuonesha maisha halisi ya wakazi wa China ingawa bado hazijapata mafanikio kama filamu ya "Deraya" lakini pia zinasifiwa sana na watazamaji. Filamu za kibiashara na za kisanaa zote zimekuwa zinaongoza katika soko la filamu nchini China.

Filamu za kibiashara zimeanza kuwepo nchini China katika miaka ya karibuni tu. filamu hizo zinatengenezwa kwa lengo la kupata mapato makubwa kutokana na kushirikisha waigizaji mashuhuri, waongoza filamu wakubwa, fedha nyingi na teknolojia ya kisasa. Filamu za aina nyingine ni za kisanaa.

Filamu ya "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" ni filamu ya kibiashara kabisa. Hadithi iliyobuniwa kwa ajili ya filamu hiyo ilitokea kwenye ukoo wa kifalme. Filamu hiyo inawafanya watazamaji wawe na hofu kutokana na hali ya utukufu wa kifalme na vita kabambe. Filamu hiyo ambayo ilitengenezwa kwa gharama kubwa, tokea ilipoanza kuoneshwa mjini Beijing tarehe 14 Desemba mwaka 2006 mapato ya tikiti kwa wiki moja yalifikia yuan milioni 200, mpaka sasa majumba yote ya filamu yanaendelea kuonesha filamu hiyo, ni filamu ambayo inapata watazamaji wengi zaidi kuliko filamu nyingine. Watazamaji wanaona, filamu hii ni nzuri ya kibiashara nchini China. Mmoja wa watazamaji alisema,

"Naona wasanii wameigiza vizuri sana, na mandhari ya vita inavutia roho yangu."

Mtazamaji mwingine alisema,

"Kama nikiambiwa nitaje dosari yake, ningesema naona filamu hiyo ingekuwa na muda mrefu zaidi ili kueleza hadithi vya kutosha zaidi na waigizaji wawe na wakati wa kutosha kuigiza. Hata hivyo kwa ujumla naridhika nayo."

Katika miaka ya karibuni filamu kama ya "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" zinazidi kuwavutia watazamaji. Kabla ya hapo, filamu za kibiashara nchini China karibu zote zilikuwa ni za kutoka nchi za nje. Waongoza filamu Zhang Yimou na Chen Kaige walitumia fedha nyingi katika matengenezo ya filamu za kibiahsara na wanatanguliza matangazo ya filamu zao kabla hazijaanza kuoneshwa, na filamu hizo licha ya kuoneshwa nchini China pia zinaoneshwa nchi za nje.

Sambamba na kuoneshwa kwa filamu za kibiashara kama "Askari Wenye Deraya Kote Mjini" na "Karamu ya Usiku", filamu za kisanaa ambazo hazikuwa na uwekezaji mkubwa pia zinasifiwa, kati ya filamu hizo filamu ya "Raia Wema katika Sehemu ya Magenge Matatu ya Mto wa Changjiang" na filamu ya "Hadithi ya Jade" zinavutia zaidi. Filamu ya "Raiaa Wema katika Sehemu ya Magenge Matatu ya Mto wa Changjiang" iliyoongozwa na Jia Zhangke mwenye umri wa miaka 36 ilipata tuzo ya Tamasha la Filamu la Venice la mwaka 2006. Filamu hiyo ikiwa na mazingira ya ujenzi wa boma la maji katika sehemu ya magenge matatu ya mto wa Changjiang inaeleza hadithi mbili za mapenzi kati ya wavulana na wasichana. Filamu ya "Hadithi ya Jade" iliyoongozwa na Ning Hao mwenye umri wa miaka 29 inaeleza hadithi moja ya kuchekesha, mapato yake ya tikti yamezidi gharama za utengenezaji kwa mara kumi. Prof. Zhang Huijun wa Chuo Kikuu cha Filamu alisema, filamu za kisanaa pia zimeanza kuimarika katika soko la filamu nchini China. Alisema,

"Filamu hiyo inamaanisha mambo mengi, yaani filamu hiyo ni mfano wa filamu iliyowekezwa fedha chache na kupata mapato makubwa, filamu hiyo inalingana na nia ya vijana kuhusu matatizo ya kijamii, na filamu hiyo imetengenezwa kwa uzoefu unaofaa wa kimagharibi."

Tokea China ijiunge na Shirika la Biashara Duniani WTO filamu zilizotengenezwa kwa fedha zisizo za kiserikali zimeongezeka, na fedha hizo nyingi zimewekezwa kwenye filamu za kibiashara zilizoongozwa na waongoza filamu mashuhuri, na fedha zilizowekezwa kwenye matengenezo ya filamu za kisanaa ni chache. Hata hivyo katika mwaka 2006 kati ya filamu 330 zilizotengenezwa nchini China, theluthi moja ni filamu za kisanaa, na filamu kadhaa zilipata tuzo katika matamasha ya kimataifa ya filamu, kwa mfano filamu ya "Korti kwenye Mgongo wa Farasi".

Filamu ya "Korti kwenye Mgongo wa Farasi" iliyoongozwa na Liu Jie inaeleza hali ngumu ya mahakimu wakiwajibika katika sehemu za mbali. Filamu hiyo ilisababisha serikali kutilia maanani kuboresha hali ya utekelezaji wa sheria katika sehemu hizo. Mwongoza filamu hiyo Liu Jie alisema, soko la filamu nchini China linahitaji filamu za kibiashara na pia linahitaji filamu za kiutamaduni. Alisema,

"Watu wengi wanasema filamu za kisanaa ni nyongeza tu ya filamu za kibiashara, lakini naona sivyo. Kama filamu zote zikiwa ni za kibiashara, filamu hizo hazitakwenda mbali, watazamaji watazichoka."

Naibu mkuu wa Idara Kuu ya Filamu ya China Bw. Zhang Pimin alipozungumza na waandishi wa habari alisema, ingawa katika soko la filamu nchini China filamu za kibiashara zinapata mapato makubwa lakini filamu za kisanaa pia haziwezi kukosekana. Alisema,

"Filamu za kibiashara zinavutia watazamaji wengi kutokana na upigaji wake wa kisasa, kwa hiyo filamu ya 'Askari Wenye Deraya Kote Mjini' inaendelea kuoneshwa moto moto, lakini watazamaji wana hamu tofauti, na pia ni lazima filamu ziwe na aina tofauti, ili kuwavutia watu wengi kuingia kwenye majumba ya filamu na kila mmoja aone anachopenda."

Bw. Zhang Pimin alisema, kuanzia mwaka huu serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia waongoza filamu vijana wenye uwezo mkubwa na kutoa sera za kusaidia filamu ambazo hazitatumia fedha nyingi katika matengenezo. Anaamini kwamba soko la filamu nchini China hakika litastawi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-12