Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-13 15:50:19    
Barua 0213

cri

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk wa sanduku la posta 52483 Dubai United Arab Emirates ametuletea barua pepe akisema, kwanza kabisa angependa kutoa pongezi zake za dhati kwa hatua ya Radi Hu Jintao wa China ya kufunga safari kwa ziara rasmi katika mataifa 8 ya Afrika mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu wa 2007.

Ziara hiyo itakayompeleka katika mataifa ya Cameron, Liberia, Sudan, Ushelisheli, Zambia, Msumbiji, Afrika ya kusini na Namibia, kwa maoni yake ni ushahidi unaodhihirisha kwa vitendo jinsi gani mikakati na maazimio yaliyopitishwa kwenye Mkutano mkuu wa viongozi wa Barza la Ushirikiano kati ya China na Afrika yanavyoanza kufanya kazi yake chii ya dhamira, makusudio na malengo yaliyowekewa.

Bila shaka yoyote ziara ya Rais Hu Jintao itaweza kusukuma mbele gurudumu la kujenga upya maendeleo ya uchumi barani Afrika chini ya msaada wa Jamhuri ya watu wa China ili kuweza kuwapatia mamilioni ya waafrika maendeleo ya kisasa na kujikwamua katika hali duni za kiuchumi, ukosefu wa maendeleo na umaskini uliokithiri.

Anaitakia kila la kheri na mafanikio ziara hiyo ya Rais Hu Jintao na ni matumainio yake makubwa kwamba Radio China Kimataifa haitawacha kuwapasha habari wasikilizaji wake juu ya ziara hiyo.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk ambaye ni rafiki yetu mzuri wa siku nyingi kwa barua yake ya kutufurahisha na kututia moyo ambayo imeonesha jinsi gani anavyofuatilia matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Hamis Hassan anayetunziwa barua zake na shule ya sekondari ya mtakatifu Carol. S.L.B 21 Sengerema, Mwanza nchini Tanzania anaanza barua yake kwa kusema, Idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa ni idhaa ambayo urushaji wake wa matangazo unaridhisha, nchini Tanzania wanaifurahia sana kwa mchango wake katika kukieneza kiswahili kimataifa. Na Inawapa faraja sana kuwasikia wachina wakiongoza matangazo kwa lugha ya kiswahili.

Bwana Hassan anaendelea kusema, kutokana na matangazo ya Idhaa ya kiswahili kuwa ya kuridhisha hivyo angeomba eneo la kurusha matangazo liongezeke, na maoni yake ni kuwa, idhaa ya kiswahili ya CRI irushe matangazo yake kupitia vituo vya radio kubwa na maarufu katika Afrika mashariki na ukanda wa maziwa makuu, hii itawawezesha watu wengi wa Afrika ya mashariki na maziwa makuu kupata matangazo yake vizuri na kwa uhakika zaidi. Anatoa mfano wa radio maarufu za Afrika mashariki ni:

? Radio Free Afrika ikiwa jijini Mwanza nchini Tanzania

? Radio One ya jijini Dar es salaam nchini Tanzania

? Radio Tumaini ya jijini Dar es salaam nchini Tanzania

? Citizen Radio ikiwa Jijini Nairobi Nchini Kenya

? Idhaa ya kiswahili ya KBC ya nchini Kenya

? 98.1 FM ya mjini Bujumbura nchini Burundi

Kwa kutumia vituo hivi vya radio kutaifanya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ijulikane zaidi kama zilivyo idhaa nyingine za kiswahili, na sio kujulikana tu bali watu wengi watanufaika kwa kujua mambo mengi yanayohusuyo nchi ya China.

Pili, Bwana Hassan anaomba kuanzishwa vituo vidogo katika nchi zinazozungumza kiswahili kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ili iweze kuwa rahisi kwa taarifa zinazohusu mataifa hayo kutangazwa na kusikika kote Afrika ya Mashariki na kati, hii itasaidia kuongeza hamasa na wasikilizaji wengi zaidi.

Tatu, matangazo yanayohusu China yasiwe mengi sana kwani itawakinai wasikilizaji wengi, lakini bwana Hasan hana maana kuwa matangazo yanayohusu China yasitangazwe ila anapenda habari zinazohusu nchi mbalimbali hasa bara la Afrika ziongezwe, na pia kianzishwe kipindi cha habari za magazetini.

Nne, Msikilizaji wetu anasema, kipindi cha Jifunze Kichina kiboreshwe zaidi kwani kimepewa muda mfupi ambao hautoshi kwa msikilizaji kupata misimiati mingi kwa wakati. Pia uendeshwaji wa kipindi usiwe wa haraka, ili wasikilizaji waweze kwenda sambamba, na bwana Hassan anapenda siku moja aweze kuongea kichina. Na anamaliza barua yake kwa kusema, "Idhaa ya Kiswahili ya CRI inaangaza kote duniani"

Tunamshukuru sana Bw Hassan kwa maoni na mapendekezo yake. Kweli maoni yametuonesha nia yake thabiti ya kuona matangazo yetu yanasikika kwenye eneo kubwa zaidi, na pia tumetambua hata juhudi zake za kutaka kujifunza lugha ya kichina. Mapendekezo aliyotoa sasa hivi yanaendelea kufanyiwa kazi, kwa hiyo tuwe na subira.

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067, Kahama, Shinyanga nchini Tanzania kwenye barua aliyotuandikia ameanza kwa salamu na pongezi kwa wafanyakazi na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Pia anasema anapenda kutumia fursa hii kuipongeza Jamhuri ya watu wa China kwa kuadhimisha miaka 57 tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya watu wa China, na anaipongeza zaidi kwa kuendelea na uhusiano na nchi za Afrika na ulimwengu kwa ujumla.

Vilevile anasema anapenda kuwapongeza wasikilizaji wenzake Ras Franzi Manko Ngogo wa Tarime, Mara nchini Tanzania na Bw Mutanda Ayub Sharif wa Bungoma nchini Kenya kwa kupata ushindi wa tuzo maalum ya kuitembelea China katika maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa radio China Kimataifa. Pia anawaomba wasikilizaji wenzake wote popote walipo ambao hawakubahatika kuchaguliwa katika ushindi wa nafasi maalum wasife moyo kwani radio China kimataifa inaendelea kuwaletea chemsha bongo kila mwaka. Mwisho anawatakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kazi njema na yenye mafanikio mema katika mwaka huu mpya wa 2007, na urafiki kati yake na Radio China Kimataifa uendelee.Tunamshukuru sana kwa barua yake na ni matumaini yetu kuwa tutadumisha urafiki kati yetu.

Msikilizaji wetu Noel Mshauri wa Seminari ya Mtakatifu Patrick Dun'gunyi, S.L.P 275 Singida nchini Tanzania, ametuletea barua akitoa salamu kwa wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa, pia anasema anapenda kutoa pongezi zake nyingi kwa CRI kutimiza miaka 65. Lakini msikilizaji wetu anapenda kutujulisha kuwa, ingawa hana klabu ya wasiklizaji huko aliko, lakini alifanya sherehe pamoja na CRI kwa yeye kuadhimisha miaka minane (8) ya uanachama hai wa CRI pamoja na matatizo ya hapa na pale ya usikivu.

Aidha msikilizaji wetu huyu anasikitika kutopata ushindi kwenye shindano la chemsha bongo, kwani alitaka asherekee miaka yake nane ya uanachama wa Radio China kimataifa akiwa nchini China. Pia radio anayotumia sasa si nzuri sana kwa usikivu, hivyo anaomba kufahamishwa gharama ya radio hapa Beijing ili atume pesa za manunuzi na CRI imtumie radio hiyo. Pamoja na hayo, bwana Mshauri ametunga shairi ili kuonesha hisia zake juu ya Radio China Kimataifa, shairi lake linasema:-

1. safari ni safari, safari nasimulia

wasikilizaji safari, si kwa meli wala punda

Si safari ya kilevya, ipumbazayo ubongo

Safari toa habari, moja mpaka sita tano

2. Ilianza ka' utani tena chini ya mapango

Ni kwa moyo kujitoa. Ka'nza huyo mjapan

Askari pinga vita, kutangaza hili lile

Mradi kufahamisha, yale yote matukio

3. Jikongoja kama jua, asubuhi kuchomoza

Shika bango kaza buti, neema ikashamiri

Fika hatua murua, hata jina badilisha

Asili ikawa China, Radio Kimataifa

4. Yote hayo yalitokea, miaka ile tano ziro,

Enzi hizo tu viziwi, jui hili wala lile

Fika mwaka tisa nane, natoka usingizini

Sasa mengi yameshajiri, taifa zaidi kukua.

5. Muda zaidi songa mbele, maboresho enda juu

waanzisha mashindano, wasikizi tu tayari

Tufahamu china nzima, vipengele mbalimbali

Pata nafasi muhimu, wenda tembelea China

6. Mbili ziro ziro moja, waanzisha matangazo,

Kwa njia ya mtandao, yaani China Online

Ukifungua utaona habari, nyingi kedekede

Anzia za pale China, pia za kimataifa

7. Ilipofika mbili sita, mwezi machi mbili tisa

Pia fungua kituo tisa moja doti tisa

Kituo cha FM, pale Nairobi Kenya

Huduma imesogezwa, Afrika mashariki

8. Hongereni viongozi, tangu mwanzo hadi sasa

Juhudi mlizofanya, wazi tunashuhudia

Pongezi watangazaji, mama Chen dada Mei

Liumba naye Mpunji, kwa bidii mtamboni

9. Narudi kwa viongozi, bidii hima dumisha

Msibweteke kwa hayo, bado mengi twahitaji

Ielezeeni China, igagadueni dunia

Ipangeni safu yenu, za kweli toa habari

10. Wasikilizaji kazi kwetu, kuchangamkia tenda

Radio tusikilize, na tovuti tufungue

Tupate habari moto, tuwe wakwanza wajanja

Tutumeni na maoni, hoja bora tuwambie

11. Malengo yenu pangeni, malengo yenu ni heri

kama simu za mkono, zitatoa matangazo

viganja vitageuka,vituo vya matangazo

CRI itapaa, itafika kileleni

12. Nami nawapongeza, kwa wenu ushirika

miaka nane mpo nami, ado ado tunasonga

Tudumishe ushirika, mimi nanyi siku zote

Munkali ukinipanda, kimbilio ni Cri

13. Safari meshika kasi,kweli mmetuthamini,

wahenga walishanena, neno tunanena tena

Pema pale japo pema, ukipema sio pema

Msumari nagongea, China radio ni pendwa

14.Nimechoka nimechoka, kuyauma maneno

Nisiwachoshe masikio, yaje leta maumivu

Nasi hatuna muwasho, twasubiri tu taarifa

Sote sisi tuungane, Radio China idumu