Ofisa wa Palestina tarehe 12 alitangaza kuwa serikali ya sasa ya Palestina inayoongozwa na kundi la Hamas itavunjwa katika siku za karibuni na kuundwa kwa serikali mpya. Viongozi wa Hamas na Fatah watajadiliana kuhusu kuundwa kwa serikali mpya. Lakini wachambuzi wanasema kuna matatizo kadhaa ambayo yanatakiwa kutatuliwa na pande mbili kabla ya kuunda serikali mpya.
Maofisa wa Fatah na Hamas waliofanya mazungumzo mjini Mecca tarehe 12 wameanza kurudi nchini Palestina. Jioni katika siku hiyo waziri mkuu wa Palestina Bw. Ismail Haniyeh alitoa hotuba kwa njia ya televisheni akiwafahamisha watu wa Palestina makubaliano ya Mecca. Alisema mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Abbas atarudi ukanda wa Gaza na kufanya majadiliano ya mwisho na Hamas kuhusu kuundwa kwa serikali mpya ya muungano. Kwa mujibu wa makubaliano ya Mecca, baada ya serikali ya Hamas kuvunjwa Bw. Abbas atamwidhinisha rasmi Bw. Ismail Haniyeh kushughulika na kuunda serikali mpya, Bw. Ismail Haniyeh atapewa muda wa wiki tano kuunda serikali hiyo.
Wachambuzi wanaona kuwa ingawa makubaliano ya Mecca yameweka msingi wa kuundwa kwa serikali mpya ya muungano, lakini shughuli za kuunda serikali hiyo zitakumbwa na matatizo kadhaa.
Kwanza, uchaguzi wa mawaziri. Makubaliano ya Mecca yameweka kanuni za kugawa idadi ya mawaziri kwa upande wa Hamas na upande wa Fatah, lakini hivi sasa kila upande haujabainisha watu wake, na tatizo muhimu ni uchaguzi wa waziri wa mambo ya ndani. Kwa mujibu wa makubaliano ya Mecca, Hamas itatoa mtu huru atakayekuwa waziri wa mambo ya ndani na akubaliwe na Bw. Abbas. Hamas imetangaza kuwa imemkabidhi Bw. Abbas orodha ya wagombea wawili, lakini bado haijapata majibu kutoka kwa Bw. Abbas. Kwa kuwa wizara ya mambo ya ndani inadhibiti jeshi la usalama la Palestina, kwa hiyo uongozi wa wizara hiyo huwa unagombewa sana.
Pili, ni tatizo la kubaki au kuendelea kwa vikosi vya Hamas. Ili kupambana na jeshi la usalama la Palestina, mwaka jana Hamas iliunda vikosi vyake vyenye askari elfu tatu bila kujali upinzani kjutoka kwa Bw. Abbas na idadi ya askari wa vikosi hivyo inaongezeka kutokana na migongano ya ndani kuongezeka. Katika mapambano ya miezi kadhaa kati ya Hamas na Fatah vikosi vya Hamas vilipambana mara nyingi na kikosi cha kulinda Bw. Abbas. Makubaliano ya Mecca hayakutaja namna ya kushughulikia vikosi hivyo.
Tatu, tatizo kubwa ni namna ya kuifanya serikali mpya ikubaliwe na jumuyia ya kimataifa. Makubaliano ya Mecca yanasema serikali mpya "itaheshimu" mikataba ya zamani kati ya Palestina na Israel, lakini hayasemi kama nchi za Israel na Marekani zinavyotaka, yaani serikali mpya iitambue Israel na kuacha matumizi ya mabavu. Baada ya makubaliano hayo kusainiwa msemaji wa Hamas alisema serikali mpya haitaitambua Israel. Hivi sasa nchi nyingi za magharibi zinachukua tahadhari kuhusu makubaliano ya Mecca, Umoja wa Ulaya tarehe 12 ulisema, hautarudisha misaada yake kwa Palestina. Waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel tarehe 12 pia alisema kuwa hawezi kusema lolote kabla ya kuundwa kwa serikali mpya ya Palestina. Na kusema kwamba hivi sasa Bw. Abbas na Hamas wamekuwa katika serikali moja, kama serikali mpya haitatambua Israel, inamaanisha kwamba Bw. Abbas atakuwa amebadilisha msimamo wake. Israel inamchukulia Bw. Abbas kuwa kama ni mwakilishi wa msimamo wa upole na inawasiliana naye toka mwanzo. Ofisa wa Israel alidokeza kuwa ikiwa serikali mpya haiwezi kukidhi matakwa yaliyotolewa na jumuyia ya kimataifa, Israel itakata mawasiliano na Bw. Abbas wakati wowote, kama hivyo ndivyo Bw. Abbas atakabiliwa na shinikizo kubwa.
Habari zinasema, tarehe 14 Bw. Abbas atakwenda Gaza kufanya mzungumzo na Hamas kuhusu kuundwa kwa serikali mpya. Watu wa Palestina wanatumai serikali hiyo iundwe ili Palestina iondokane na hali mbaya ya sasa.
Idhaa ya kiswahili 2007-02-13
|