Baada ya kufanya kwa makini majadiliano ya siku 6, mkutano wa kipindi cha tatu cha Duru la tano la mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea umefungwa tarehe 13. Waraka wa pamoja kuhusu "Hatua ya mwanzo ya kutekeleza taarifa ya pamoja" umetolewa kwenye mkutano huo, ambapo pande zote 6 zimekubali kufuata kanuni za "vitendo kwa vitendo", kuchukua hatua za pamoja zinazolingana ili kutekeleza kipindi hadi kipindi taarifa ya pamoja. Kwenye sherehe ya kufungwa kwa mkutano huo, kiongozi wa ujumbe wa China ambaye pia ni naibu waziri wa mambo ya nje Bwana Wu Dawei alipotoa risala alisema:
Kutokana na juhudi za pande mbalimbali, mkutano huo umefikia maoni muhimu ya pamoja kuhusu hatua ya mwanzo ya kutekeleza taarifa ya pamoja, mkutano huo umepata mafanikio mema, ambayo yameonesha kuwa hatua kubwa na imara imepigwa katika mazungumzo ya pande 6 na kutimiza lengo la kuifanya sehemu ya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na silaha za nyuklia. Hali hii si kama tu inasaidia amani, utulivu na maendeleo ya peninsula na sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki, na kusaidia nchi husika kuboresha na kuendeleza uhusiano kati yao, hali kadhalika inasaidia kujenga mazingira mapya yenye masikilizano kwenye sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki.
Waraka wa pamoja kuhusu "Hatua ya mwanzo ya kutekeleza taarifa ya pamoja" uliopitishwa siku hiyo ni waraka mwingine unaonesha matokeo makubwa yaliyopatikana kutokana na juhudi za pamoja kwa kufuata Taarifa ya pamoja ya tarehe 19 Septemba. Waraka huo umeweka hatua ya mwanzo ya pande hizo 6 kuhusu upande wa Korea ya kaskazini kufunga majengo ya nyuklia ya Yongbyon kwa lengo la kuacha kabisa mpango wa nyuklia; Korea ya kaskazini kuwaalika wakaguzi wa shirika la nishati ya atomiki duniani warudi nchini humo kufanya kazi zote za lazima za usimamizi na uthibitishaji zinazokubaliwa na shirika hilo na upande wa Korea ya kaskazini; na pande mbalimbali zinazohusika zimekubali kutoa misaada ya dharura ya nishati kwa Korea ya kaskazini, misaada hiyo itaanza kutolewa ndani ya siku 60. Mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Taasisi y a sayansi ya jamii ya China Bwana Gao Hong amesifu sana waraka huo akisema:
Waraka huo wa pamoja umetuwezesha tuone mambo mengi halisi kama vile Korea ya kaskazini kuacha majengo ya nyuklia, ushirikiano wa kiuchumi kati ya jumuia ya kimataifa na Korea ya kaskazini, aidha kuhusu usalama wa kijeshi, ambapo Marekani na Korea ya kaskazini zitafanya juhudi za kuelekea kuanzisha uhusiano wa kibalozi, na Japan na Korea ya kaskazini zitafanya juhudi za kuufanya uhusiano kati yao uwe wa kawaida.
Bwana Gao Hong pia anaona kuwa, wakati pande mbalimbali zinapofurahia maendeleo yaliyopatikana katika mazungumzo hayo, pande hizo pia zinapaswa kutambua zaidi kuwa, kutimiza lengo la kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia ni mchakato wa muda mrefu na wenye utatanishi. Alisema:
Hali ya peninsula ya Korea na sehemu nzima ya Asia ya kaskazini mashariki bado ina utatanishi mwingi. Baada ya kufanya juhudi za pamoja, maendeleo makubwa yamepatikana, lakini baada ya kupiga hatua hiyo kubwa, huenda baadaye kutakuwa na vizuizi vingine kadha wa kadha. Hivyo pande zinazohusika zinapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi ili mchakato mzima wa amani uendelee kwa mwelekeo wa kujenga utaratibu wa kudumisha amani ya kudumu.
|