Milipuko miwili ya mabomu yaliyotegwa kwenye mabasi ilitokea karibu na mji wa Beirut nchini Lebanon, na kusababisha vifo vya watu watatu, na wengine 23 kujeruhiwa. Wachambuzi wanaona kuwa milipuko hiyo iliyotokea siku moja kabla ya kutimiza miaka miwili tangu kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Rafiq Hariri imeonesha kuendelea kuwepo kwa hali ya wasiwasi nchini Lebanon, na migongano kati ya vyama vinavyopingana na mgogoro kati ya makundi ya kidini umezidi kuwa mkubwa siku hadi siku.
Polisi wa Lebanon walisema milipuko hiyo ilitokea katika sehemu ya milimani ambako wanaishi waumini wengi wa dini ya kikristo, na sehemu hiyo iko karibu na mji wa Bikfaya ambao ni makwao ya rais wa zamani wa Lebanon ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Phalange Bw. Amin Gemayal. Mtoto wa Bw. Amin ambaye ni waziri wa zamani wa viwanda wa Lebanon Bw. Pierre Gemayal alikuwa mwanasiasa maarufu, aliuawa na watu wenye silaha mjini Beirut tarehe 21 mwezi Septemba mwaka jana. Polisi walisema mabomu hayo yalitegwa chini ya viti vya mabasi, na mlipuko ulitokea kwenye basi la pili dakika kadhaa tu baada ya mlipuko kutokea kwenye basi la kwanza. Ingawa mpaka sasa bado hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na milipuko hiyo, lakini watu wengi wanaona kuwa milipuko hiyo inahusiana na utimiaji wa miaka miwili tangu kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Rafiq Hariri.
Tarehe 14 mwezi Septemba mwaka 2005, waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Rafiq Hariri aliuawa kutokana na mlipuko wa mabomu yaliyotegwa kwenye gari mjini Beirut. Tukio hilo lilisababisha mfarakano wa kisiasa na hali ya wasiwasi wa usalama nchini Lebanon. Kwa upande mmoja, Syria ililaumiwa kuhusika na tukio hilo na kulazimishwa kuondoa jeshi lake kutoka Lebanon; shirikisho la vyama vinavyoipinga Syria lilitumia fursa hiyo na kushinda kwenye uchaguzi wa bunge na kuunda serikali mpya, na mkwaruzano kati ya vyama vinavyoiunga mkono Syria na vyama vinavyoipinga Syria nchini Lebanon ulikuwa mkubwa zaidi. Kwa upande mwigine, kutokana na kupamba moto kwa mgogoro kati ya vyama vinavyopingana, mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wanasiasa wanaoipinga Syria na waandishi wa habari yalitokea mara kwa mara, hali ya usalama ilizidi kuwa mbaya. Baada ya mgogoro kutokea kati ya Lebanon na Israel mwaka jana, mgogoro kati ya vyama vinavyopingana nchini Lebanon pia umekuwa mkali zaidi.
Chama cha Hezbollah cha madhehebu ya Shia, Chama cha harakati za Amal na Chama cha Uhuru na Uzalendo cha wakristo vinavyoiunga mkono Syria ambavyo vina viti vichache kwenye bunge vilitoa madai hadharini ya kugawana madaraka. Vyama hivyo vinataka kuunda serikali mpya ya muungano, na vyama hivyo vitapata theluthi moja ya viti kwenye baraza la mawaziri ili viwe na nguvu ya kuamua sera muhimu za serikali.
Lakini shirikisho la vyama vinavyoipinga Syria ambalo linachukua viti vingi kwenye Bunge linapinga kithabiti madai hayo, na migongano kati ya pande hizo mbili inaongezeka siku hadi siku. Kuanzia tarehe mosi Mwezi Desemba mpaka sasa, watu wanaounga mkono vyama vinavyoipinga Syria wanafanya maandamano mara kwa mara mjini Beirut wakiitaka serikali ya hivi sasa ijiuzulu.
Milipuko ya mabomu yaliyotegwa kwenye mabasi iliyotokea tarehe 13 huenda itasababisha hali ya usalama nchini Lebanon kuwa ya wasi wasi zaidi. Ili kuzuia hali ya hivi sasa iszidi kuwa mbaya, vyama vya Lebanon vinapolaani tukio hilo la kigaidi, vimetoa mwito wa kusimamisha mgogoro na mashambulizi ya kigadi.
Maoni ya raia yanaonesha kuwa vyama vinavyopingana kufanya juhudi pamoja ili kuondoa hali ya wasiwasi ya kisiasa ni njia muafaka ya kutatua mgogoro nchini humo. Vyama hivyo vinatakiwa kufanya mazungumzo kwa amani na kujizuia kugombea madaraka. Ama sivyo hali ya Lebanon huenda itazidi kuwa mbaya.
|