Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-15 14:46:46    
Kheri ya mwaka mpya wa Kichina!

cri

Sikukuu ya Spring ambayo ni mwaka mpya wa jadi kwa kalenda ya kilimo ya China inakaribia. Sikukuu hiyo kubwa kuliko nyingine katika jamii ya Wachina itaanza tarehe 18, Februari mwaka huu. Hivi sasa nchini China, ama vijijini au mijini, watu wana pilikapilika nyingi wakifanya maandalizi kwa ajili ya sikukuu hiyo ya jadi.

Katika vijiji vya China inaonekana kuwa shamrashamra za sikukuu ya spring zinakuja mapema zaidi kuliko sehemu za mijini, kwani hivi sasa ni majira ya siku za baridi, hakuna shughuli nyingi za kilimo, na wakulima wa China wanafanya maandalizi ya sikukuu hiyo kwa furaha.

Ukitembelea kijiji cha Sanzhao kilichopo kwenye kitongoji cha mji wa Xian, magharibi mwa China, utakuta furaha ya sikukuu ya spring imeenea kote kijijini, ambapo jozi za kandili zimetundikwa kwenye milango ya familia moja moja, na watoto wanacheza kwa pamoja. Kijiji hicho kinajulikana kwa kuwa na historia zaidi ya miaka elfu 2 ya utengenezaji wa kandili. Watu wanatengeneza kandili kwa kutumia vipande vya mianzi, na kuifunika kwa karatasi zilizochapishwa nembo mbalimbali za baraka.

Huyan Jianyi mwenye umri wa miaka zaidi ya 40 ni fundi hodari wa kutengeneza kandili. Kwenye ua wa nyumba yake, kuna kandili za aina mbalimbali. Bwana huyo alisema "Natengeneza kandili za aina mbalimbali, kubwa na ndogo, nyingi ni za mitindo ya katuni. Hivi karibuni nilitengeneza kandili za mtindo wa maua ya yungiyungi kwa ajili ya sikukuu ya spring."

Wakati wa sikukuu ya spring, kandili zinanunuliwa sana na wateja nchini China, kwa hiyo Bw. Huyan na jamaa zake hawawezi kusimamisha kazi ya kutengeneza kandili mpaka mkesha wa sikukuu. Hata hivyo bwana huyo alieleza kufurahia kuwapa wengine furaha ya sikukuu.

Mkoani Henan, katikati ya China, wakulima pia wana pilikapilika nyingi za kufanya maandalizi kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China. Katika mwaka uliopita, wakulima wa China walipata manufaa makubwa kutokana na sera za serikali za kufuta kodi ya kilimo na kuwapa wakulima ruzuku za zana za kilimo na mbegu.

Nyumbani kwa mama Zhang Xiangyun, jamaa wa familia hiyo wanaandaa vitafunwa vya Jiaozi ambavyo ni aina ya chakula cha jadi cha China. Mama Zhang alisema "Tumewahi sana kukamilisha maandalizi ya sikukuu ya spring. Wanafamilia wote wamepata nguo mpya, vyakula vya aina mbalimbali vimenunuliwa. Sasa tuna matarajio na kuwadia kwa sikukuu ya spring, tutaisherehekea kwa furaha."

Kwenye mlango wa nyumba ya mama Zhang, zimetundikwa kandili mbili nyekundu. Na nyumbani peremende na keki mbalimbali zimewekwa mezani. Mama huyo alisema, baada ya kufutwa kwa kodi ya kilimo na kupewa ruzuku za aina mbalimbali, mapato ya wanakijiji yameongezeka kwa Yuan elfu kadhaa kwa shamba la hekta moja kwa mwaka, wamekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kununua vitu vingi kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China.

Wakulima waliokwenda mijini kufanya kazi pia walianza kurudi nyumbani kukutana na jamaa zao. Katika miaka ya hivi karibuni, katika kipindi cha sikukuu ya spring, wizara ya reli ya China imeandaa magarimoshi yatakayowahudumia wakulima hao. Usiku wa tarehe 5 Februari, kwenye garimoshi moja la namna hii lililokuwa linaondoka kutoka Beijing, mkulima Li Meixiang aliyefanya kazi mjini Beijing alisema "Maskani yangu ni Shiyan, mkoani Hubei, nimewakumbuka sana jamaa zangu. Zamani ilinibidi mimi mwenyewe ninunue tiketi, mwaka huu bosi wetu alitusaidia kuagiza tiketi na alilipa nusu ya gharama ya tiketi."

Dada huyo aliongeza kuwa, mwaka huu kwenye garimoshi hilo linalowahudumia wakulima waliofanya kazi mijini, hata walipata zawadi ya matunda, maji na vyakula vyingi vidogo vidogo.

Katika miji ya China watu wanaendelea kufanya kazi, lakini furaha ya mwaka mpya wa jadi wa China pia inaonekana kuongezeka siku hadi siku. Dada Han Rui ni mkazi wa Beijing, alieleza jinsi jamaa zake wanavyosherehekea sikukuu ya spring. Alisema "Wakati wa sikukuu ya spring, tunakutana kwenye nyumba ya wazee, ambapo jamaa ambao hawakuonana kwa miaka mingi wanaweza kukutana. Kwenye mkesha wa sikukuu, tunakula chakula cha jioni kwa pamoja, ambapo hakika tunakula vitafunwa vya Jiaozi, kwani kwa Wachina chakula cha Jiaozi kinamaanisha kujumuika. Kula vitafunwa vya Jiaozi kwenye mkesha wa sikukuu ya spring kunamaanisha kutakiana neema na furaha katika mwaka mpya utakaokuja."

Idhaa ya kiswahili 2007-02-15