Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-15 15:01:31    
Mafundi wa kabila la Wahezhe waendeleza ufundi wa jadi

cri

Mliosikia ni wimbo unaojulikana miongoni mwa watu wa kabila la Wahezhe, uitwao kaka aliyekwenda kuwinda amerudi nyumbani. Hapo awali Wahezhe walikuwa wanajishughulisha na uvuvi na uwindaji, walikuwa hodari katika mambo ya uvuvi na uwindaji, kama vile kutengeneza mashua kwa magamba ya miti na kutengeneza nguo kwa kutumia ngozi ya samaki. Hivi sasa baadhi ya Wahezhe wameanza kujishughulisha na kilimo au viwanda. Je, ufundi wa jadi wa kabila hilo unaendelea vipi?

Kabila la Wahezhe lina watu wasiozidi elfu 5, ambao wanaishi kando ya Mto Wusuli, kaskazini mashariki mwa China. Wahezhe ni wavuvi hodari na wanajulikana kutokana na ufundi wa kutengeneza mashua za aina mbalimbali, zikiwemo mashua zilizotengenezwa kwa magamba ya miti aina ya white birch. Mashua moja ya namna hii imehifadhiwa katika wilaya ya Sipai, mkoani Heilongjiang wanakoishi Wahezhe, mashua hiyo ilitengenezwa na Bw. Fu Zhanxiang, fundi anayejulikana miongoni mwa Wahezhe. Fundi huyo aliyeishi kando ya Mto Wusuli tangu utotoni mwake, alieleza kuwa kwake kusafiri mtoni kwa kutumia mashua ya namna hii ni kama jambo lililotokea jana. Alisema"Tunapotengeneza mashua hii, kwanza tunatengeneza mkuku kwa kutumia fito tulizopata kando ya mto, halafu tunaufunika mkuku kwa magamba ya mti wa white birch. Sehemu ya chini ya mashua ni gamba moja la mti. Tunafunika sehemu ya ndani ya mashua kwa magamba mengine ya mti, na kuunganisha magamba hayo ya miti kabla ya kukamilisha utengenezaji."

Bw. Fu Zhanxiang aliongeza kuwa, Wahezhe hawawezi kuishi bila ya miti ya white birch. Magamba ya miti hiyo yanaweza kukinga maji, na si rahisi kuoza. Zaidi ya hayo, magamba hayo ya miti ni rahisi kukatwa, na vyombo vinavyotengenezwa kwa magamba hayo ya miti ni vyepesi na rahisi kubeba, na si rahisi kuvunjika. Mashua zilizotengenezwa kwa magamba hayo ya miti ni nyepesi, na zinafaa kwa uvuvi katika sehemu za mto zenye kina kifupi.

Mbali na kutengeneza mashua kwa magamba ya miti ya white birch, watu wa kabila la Wahezhe pia wanatengeneza vitu mbalimbali kwa kutumia magamba hayo, kama vile masanduku na mabakuli. Zaidi ya hayo, Wahezhe wanachora na kuchonga picha mbalimbali kwenye vitu hivyo, na kuvifanya viwe mapambo mazuri.

Hivi sasa kutokana na mabadiliko ya maisha, Wahezhe wengi wamesahau ufundi wa kutengeneza vitu kwa kutumia magambao ya miti ya white birch. Bw. Fu Zhanxiang mmoja ni kati ya mafundi wachache ambao bado wanaendelea kutumia ufundi huo wa jadi. Kwa maoni yake, ufundi huo ni utamaduni wa kabila la Wahezhe, ni lazima usipotee, kama ukipotea kabila hilo litakosa umaalumu wake. Katika miaka mingi iliyopita, Bw. Fu Zhanxiang alikuwa anashikilia ufundi huo na kuwafundisha vijana ili waweze kurithi ufundi huo.

You Juntao mwenye umri wa miaka zaidi ya 20 ni mwanafunzi anayeridhika sana na mwalimu wake, Bw. Fu Zhanxiang. Kijana huyo anatengeneza visanduku vya kuhifadhi vito kwa kutumia magamba ya miti ya white birch. Visanduku hivyo vinapendwa sana na wanawake. Vile vile anachora picha kwenye magamba hayo. Alisema alikuwa akijifunza kutoka kwa mwalimu wake kwa miaka mitatu, sasa anaweza kuhitimu. Alisema "Hivi sasa sina kazi nyingine, bali natengeneza vitu mbalimbali kwa kutumia magamba ya miti ya white birch. Watu wa vizazi kadhaa vya familia yangu wamepokezana ufundi huo, babu yangu, mjomba wangu, na sasa ni mimi. Najifunza ufundi huo ili nistahili jina la kabila la Wahezhe."

You Juntao alipomaliza masomo ya sekondari ya juu, aliwahi kutafuta ajira lakini alishindwa kupata nafasi ya kujiendeleza, kwa hiyo alirudi kwenye maskani yake na kuanza kujifunza ufundi huo wa jadi kutoka kwa fundi Fu. Kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii katika maskani yake, You Juntao aliona watalii wengi wanavutiwa na vitu vinavyotengenezwa kwa magamba ya miti ya white birch. Kwa hiyo alifanya bidii zaidi katika kubuni na kutengeneza vitu hivyo na kuanzisha duka moja la kuuza vitu alivyotengeneza. Vile vile alianzisha duka lingine kwenye mtandao wa Internet. Kijana huyo alieleza mpango wake kuwa, atajenga kiwanda cha kutengeneza vitu vinavyotengenezwa kwa ngozi za miti ya white birch kwa wingi.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-15