Tarehe 14 watu elfu kumi kadhaa walikusanyika kwenye sehemu ya katikati ya mji wa Beirut kukumbuka miaka miwili tokea waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Rafiq Hariri auawe.
Waziri mkuu Fuad Siniora na Saad al-Hariri ambaye pia ni kiongozi anayewakilisha kundi kubwa ndani ya bunge na mtoto wa Bw. Hariri, walihudhuria mkutano huo. Kwenye mkutano huo Bw. Saad al-Hariri aliwataka watu wa Lebanon waimarishe mshikamano na kufanya mazungumzo kati ya makundi tofauti. Alisisitiza kwamba kuanzisha mahakama ya kimataifa na kushughulikia tukio la kuuawa kwa Bw. Rafiq Hariri ni njia pekee ya kuondoa msukosuko wa kisiasa wa Lebanon. Mkutano huo ulikuwa salama kutokana na askari na polisi kuchukua hatua za kuimarisha usalama.
Tarehe 14 Februari, mwaka 2005, waziri mkuu wa zamani Bw. Rafiq Hariri aliuawa mjini Beirut, kundi linaloipinga Syria mara moja lilishutumu Syria kuhusika na tukio hilo, na kusababisha kutokea kwa makundi mawili, moja likiunga mkono Syria na lingine likiipinga Syria. Katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwaka huo, kundi linalopinga Syria lilipata ushindi na kuunda serikali. Chama cha Hezbollah na Chama cha Movement Amal ambavyo vinaunga mkono Syria vimekuwa vyama vya upinzani. Katika miaka miwili iliyopita makundi hayo mawili yalipambana vikali kuhusu uchunguzi na tukio la kuuawa kwa Bw. Hariri, Lebanon imetumbukia katika hali ya wasiwasi.
Wachambuzi wanaona kuwa mkutano wa halaiki ulioandaliwa na kundi la watu wengi kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka miwili tokea Bw. Hariri auawe, unataka kuonesha kuunga mkono kuanzishwa kwa mahakama ya kimataifa, na lengo lingine ni kuonesha nia ya kutaka serikali ya sasa ivunjwe. Kutokana na hali ilivyo sasa mgogoro wa kisiasa kati ya makundi hayo mawili hauwezi kutatuliwa katika muda mfupi.
Kwanza, kundi kubwa na kundi dogo hayawezi kuafikiana kuhusu kugawana madaraka. Tokea mgogoro kati ya Lebanon na Israel ulipotokea katika majira ya joto mwaka jana, mapambano kati ya makundi hayo mawili yamekuwa makali. Kundi la upinzani linataka serikali iundwe upya na kutaka theluthi moja ya mawaziri serikalini ili liwe na haki katika maamuzi muhimu ya serikali, lakini kundi kubwa linakataa kabisa. Kutokana na hayo mawaziri sita wa vyama vya upinzani walijiuzulu mwezi Novemba mwaka jana na kuifanya serikali ya sasa isiwe halali. Isitoshe, tokea tarehe mosi Desemba mwaka jana maandamano yanayotaka serikali ivunjwe yamekuwa yanaendelea kufanyika hadi leo katika sehemu ya katikati ya mji wa Beirut.
Pili, kuhusu suala la kuanzisha mahakama ya kimataifa ya kushughulikia tukio la kuuawa kwa Bw. Hariri, maoni tofauti kati ya makundi mawili yanaendelea. Hivi sasa serikali na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimeidhinisha kwa kuanzishwa kwa mahakama hiyo, lakini vyama vya upinzani vinasema uamuzi huo wa serikali sio wa haki, rais Emile Lahoud hataki kusaini uamuzi huo na spika ambaye ni kiongozi wa chama cha Movement Amal hataki kuwasilisha waraka huo kwenye bunge na kuufanya uamuzi huo usiwe na nguvu ya kisheria.
Tatu, mgongano kati ya makundi hayo mawili unasababisha mapambano ya ubabe kati ya watu wanaounga mkono makundi hayo mawili, na kusababisha hali kuwa mbaya siku hadi siku. Mwaka huu tu mapambano hayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 10 na kiasi cha watu mia moja kujeruhiwa. Na tukio lililo baya zaidi ni kuwa katika siku kabla ya siku ya kumbukumbu ya miaka miwili ya kifo cha Bw. Hariri, mashambulizi mawili ya kigaidi yalitokea ndani ya mabasi na kusababisha watu wengi kupoteza maisha na kujeruhiwa.
Kwa hiyo, msukosuko wa kisiasa uliosababishwa na migongano kati ya makundi mawili umehatarisha usalama na utulivu wa nchi ya Lebanon. Watu wanatumai kuwa makundi yote yatatanguliza mbele maslahi ya taifa na kuifanya Lebanon ifuate njia ya kuelekea kwenye utulivu na maendeleo kwa njia ya mazungumzo.
Idhaa ya kiswahili 2007-02-15
|