Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-16 14:44:38    
Mahmoud Abbas amteua rasmi Ismail Haniyeh kuunda serikali mpya

cri

Serikali ya kundi la Hamas iliyodumu kwa miezi 11, tarehe 15 ilitangaza kujiuzulu, kisha mwenyekiti wa mamlaka la utawala wa Palestina Bw. Abbas amemteua rasmi waziri mkuu wa muda Bw. Ismail Haniyeh aunde serikali mpya ya muungano. Hii inamaanisha kuwa Palestina imepiga hatua ya kuelekea kwenye maafikiano ya kitaifa na kujinasua kutoka kwenye vikwazo vya kiuchumi vya kimataifa.

Shughuli fupi ya uteuzi huo ilifanyika mjini Gaza. Kwenye shughuli hiyo kwa niaba ya mawaziri wote, Bw. Ismail Haniyeh alimkabidhi Bw. Abbas ombi la kujiuzulu. Baada ya kupokea ombi hilo Bw. Abbas akamteua rasmi Bw. Ismail Haniyeh aunde serikali mpya. Kwenye shughuli hiyo Bw. Abbas aliitaka serikali mpya iheshimu maazimio husika ya kimataifa ya Palestina na mikataba kati ya Palestina na Israel. Bw. Ismail Haniyeh aliahidi kuwa ataunda serikali mpya kwa mujibu wa maagizo yaliyoandikwa kwenye waraka wa uteuzi. Kwa mujibu wa sheria ya Palestina, Bw. Ismail Haniyeh ataunda serikali mpya ndani ya wiki tano, na katika muda huo Bw. Ismail Haniyeh ataendelea kuwa waziri mkuu.

Kujiuzulu kwa serikali ya Hamas na kumteua Bw. Ismail Haniyeh ni hatua moja muhimu katika njia ya kuunda serikali ya muungano ya makundi mbalimbali. Katika mwaka mmoja uliopita, Palestina iliingia katika hali mbaya ya kifedha na migongano ya kisiasa, na juhudi za kuunda serikali mpya pia zilikumbwa na matatizo mengi. Baada ya mazungumzo mengi na migongano mingi, makundi ya Hamas na Fatah mwishowe yamekubaliana kuunda serikali ya muungano. Hii imeleta matumaini katika kukomesha migogoro ndani ya Palestina na kupata tena misaada ya kiuchumi ya kimataifa.

Hata hivyo, makundi ya Hamas na Fatah pia yanakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwanza, ni wagombea wa nafasi muhimu za uwaziri. Hivi sasa pande mbili bado zinahitalifiana kuhusu nafasi za naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani. Kwa mujibu wa habari, Fatah ilimpendekeza mkuu wa jeshi la usalama la Palestina Bw. Mohammed Dahlan awe naibu waziri mkuu, lakini pendekezo hilo linapingwa na Hamas. Bw. Dahlan ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika eneo la Gaza na anachukuliwa kama ni mrithi wa Bw. Abbas, lakini ana tofauti kubwa na Hamas. Kwa hiyo Hamas inataka Fatah imteue afisa mmoja wa ukingo wa magharibi wa mto Jorda kwenye wadhifa huo. Kuhusu nafasi ya waziri wa mambo ya ndani, Hamas ilitoa orodha ya watu wawili kwa Bw. Abbas, lakini Bw. Abbas hakujibu lolote.

Pili, pande mbili zinahitaji kukubaliana kuhusu suala la namna ya kushughulikia vikosi vya Hamas. Katika mapambano yaliyofanywa katika miezi kadhaa iliyopita dhidi ya Fatah, vikosi hivyo vilishiriki kwenye vitendo vingi vya Hamas na kupigana kisilaha na jeshi la usalama linalodhibitiwa na Bw. Abbas. Hivi sasa pande mbili zinaendelea na mvutano kuhusu namna ya kushughulikia vikosi hivyo, na shughuli za kuwateua wasimamizi wa vikosi hivyo iliyopangwa kufanyika tarehe 14 pia imeahirishwa. Tarehe 15 maofisa wa Bw. Abbas na Hamas walifanya mazungumzo kuhusu suala hilo lakini pande mbili hazikuafikiana.

Zaidi ya hayo, Bw. Abbas na Bw. Ismail Haniyeh wanakabiliwa na matakwa ya kimataifa ya kuitaka serikali mpya itambue Israel. Watu wa Palestina wanatumai kuwa jumuyia ya kimataifa itaweza kuikubali serikali mpya na kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa Palestina. Lakini tarehe 15 ofisa wa Marekani alisema, serikali mpya ya Palestina ni lazima iitambue Israel na kutangaza kuacha vitendo vya kimabavu na kutambua mikataba yote iliyosainiwa hapo kabla kati ya Palestina na Israel, ama sivyo serikali ya Marekani itaendelea kutoikubali serikali hiyo na kutowasiliana na mawaziri wowote wa serikali hiyo. Hali kadhalika, Israel pia inasisitiza kuwa serikali yoyote ya Palestina ni lazima ikubali masharti matatu ya jumuyia ya kimataifa. Lakini serikali ya muda inayotawaliwa na Hamas inashikilia kutoitambua Israel. Kwa hiyo kutokana na suala hilo mikwaruzano kati ya Bw. Abbas na Hamas haitaepukika.

Tarehe 21 waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Rice atafanya mazungunzo na Bw. Abbas na waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert, kwenye mazungumzo hayo msimamo wa serikali mpya ya Palestina hakika utakuwa mada muhimu. Imefahamika kwamba Bw. Abbas anatumai kuwa serikali mpya itaudwa kabla mazungumzo hayo. Lakini hadi sasa Hamas na Fatah bado hazijaafikiana kuhusu mawaziri na mpango wa kisiasa wa serikali mpya, itakuwa vigumu kukamilisha kazi ya kuunda serikali mpya kabla ya mazungumzo hayo. Kwa hiyo sio rahisi kupata maendeleo kwa mazungumzo hayo ya pande tatu.

Idhaa ya kiswahili 2007-02-16