Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-19 19:50:02    
Wachina waishio nchini Kenya washerehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China

cri

Tarehe 18 Februari ilikuwa Tarehe 1 Januari ya mwaka mpya wa jadi wa China kwa kalenda ya kilimo ya China, siku hiyo shamrashamra zilionekana kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa huko Nairobi Kenya, ambapo wachina wanaoishi nchini Kenya walishiriki kwenye shughuli kubwa ili kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China.

Siku hiyo uwanja wa kituo cha mikutano ya kimataifa cha Kenya ulipambwa kwa mtindo dhahiri wa kichina, ambapo vijana wa China waliovaa mavazi ya jadi ya China walichezesha dragon na simba wa bandia kwa kufuata midundo ya furaha ya muziki, wakiwavutia watazamaji wengi na kupigiwa makofi ya furaha.

Shughuli hizo zilizoandaliwa na ubalozi wa China nchini Kenya na Shirikisho la wachina wanaoishi nchini Kenya ziliwashirikisha wachina na wakazi wa Kenya zaidi ya elfu moja, ambapo balozi wa China nchini Kenya Bwana Zhang Ming aliwatakia heri na baraka wachina wanaoshi nchini Kenya na wakazi wa Kenya. Alisema

"China na Kenya ziko mbali, lakini mawasiliano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili yalianzia tangu enzi na dahari. Katika miaka ya hivi karibuni, mawasiliano hayo yameongezeka zaidi, ambapo idadi ya wachina wanaoishi nchini Kenya pia inaongezeka dhahiri. Wachina wanaoishi nchini Kenya wanaenzi mila na maadili ya taifa la China, wanafanya juhudi bila kuogopa taabu katika kuendeleza shughuli zao, ambao wanaishi pamoja na wananchi wa Kenya katika hali ya masikilizano, na wametoa mchango wao kwa ajili ya maendeleo ya uchumi na jamii ya Kenya. Nina matumaini kuwa katika mwaka mpya, shughuli za wachina wanaoishi nchini Kenya zitaendelezwa zaidi, na muhimu zaidi ni kuwa wachina hao wanatakiwa kuishi pamoja na wakazi wa Kenya katika hali ya mshikamano na masikilizano, ili kutafuta maendeleo ya pamoja.

Shughuli za kusherehekea sikukuu ziliwavutia watazamaji wengi kwa maonesho ya michezo ya Gongfu na maonesho ya mavazi ya jadi ya China, ambapo wimbo wa Kenya uitwao Jambo ulioimbwa na mke wa balozi wa China nchini Kenya Bibi Cai Shaoli na wafanyakazi wa ubalozi wa China nchini Kenya uliwafurahisha wakazi wa Kenya, ambapo wengi wao waliimba kwa hiari pamoja nao, sherehe ilifika kileleni.

Kwenye maonesho ya maandiko ya Kichina na michoro ya kichina na vitu vya sanaa vya China, pia kulikuwa na watazamaji wengi wenyeji wa Kenya na watu kutoka nchi nyingine duniani, na mabanda mbalimbali ya vitoweo vya kichina yaliwavutia watu wengi hata kuwafanya wang'ang'anie huko kwa muda mrefu. Wachina wanaoishi nchini Kenya waliona kama wako nyumbani, na wakenya na watalii kutoka nchi nyingine duniani walijionea mila na desturi za China katika shughuli hizo za kusherehekea mwaka mpya wa jadi wa China.

Hii ni mara ya kwanza kwa wachina wanaoishi nchini Kenya na wananchi wa Kenya kusherehekea pamoja sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China. Bwana Wang Zhijia ambaye amefanya kazi kwa miaka mingi nchini Kenya alisema:

"Naona shughuli hizo zina umuhimu wa kufungua ukurasa mpya, ambazo zimeonesha ustawi na neema ya China. Nchi yetu imekuwa na nguvu na ustawi, hivyo inaweza kufanya shughuli kubwa kama hizo. Aidha shughuli hizo zimewashirikisha wachina wanaoishi nchini Kenya, pia zimeonesha sura mpya ya wachina katika zama mpya, mimi ninafurahi sana".

Mkuu wa Shirikisho la wachina wanaoishi nchini Kenya Bwana Han Jun alisema, ana matumaini kuwa shughuli hizo zitaongeza zaidi maelewano kati ya wananchi wa China na Kenya, kuenzi utamaduni wa taifa la China na kuongeza mshikamano kati ya wachina wanaoishi ng'ambo.

Idhaa ya Kiswahili 2007-02-19