Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-20 19:07:55    
Mazungumzo kati ya pande tatu za Marekani, Israel na Palestina hayajapata maendeleo

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice ambaye yuko ziarani katika sehemu ya mashariki ya kati, waziri mkuu wa Israel Bw Ehud Olmert na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmoud Abbas tarehe 19 Februari huko Jerusalem walifanya mazungumzo, hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kufanya mazungumzo ya pamoja, lakini mazungumzo hayo hayajapata maendeleo katika kuhimiza mchakato wa amani ya Palestina na Israel.

Siku hiyo baada ya kumalizika kwa mazungumzo, Bi. Condoleezza Rice alitoa taarifa fupi akisema, wamejadili kuhusu kuunda serikali mpya ya Palestina na masuala mengineyo, mazungumzo hayo yanazitaka Palestina na Israeli ziheshimu makubaliano ya kusimamisha vita yaliyofikiwa mwezi Novemba mwaka jana, na kuhimiza utekelezaji wa mpango wa amani ya mashariki ya kati. Bi. Rice aliongeza kusema kuwa, Bw. Olmert na Bw. Abbas wameamua kukutana tena hivi karibuni, na wameutaka upande wa Marekani ushiriki tena kwenye mazungumzo hayo, hivyo Bi Rice alisema, atarudi mashariki ya kati siku chache zijazo. Lakini hakudokeza tarehe ya mkutano ujao kati ya viongozi wa Palestina na Israeli na tarehe gani atarudi tena katika sehemu ya mashariki ya kati.

Habari zinasema mbali na mtafsiri wa kiarabu wa Bi. Rice, wasaidizi wowote wa viongozi hao watatu hawakushiriki kwenye mazungumzo ya siku hiyo.Na baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, Bwana Olmert na Bwana Abbas waliondoka mara moja, na hawakukutana na waandishi wa habari. Dalili zinaonesha kuwa, mazungumzo kati ya viongozi hao watatu hayakupata maendeleo halisi. Vyombo vya habari vinasema, hali hii inatokana na migongano mikubwa kati ya pande hizo tatu kuhusu kuunda serikali mpya ya Palestina.

Marekani inashikilia kuwa, serikali mpya ya Palestina inapaswa kutatua kanuni tatu zilizotolewa na jumuiya ya kimataifa, yaani kuitambua Israel, kuacha matumzizi ya nguvu za kimabavu na kufuata makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Palestina na Israel. Katika taarifa aliyotoa siku hiyo Bi. Rice pia amesisitiza kanuni hizo. Tarehe 18 kwa nyakati tofauti, Bi. Rice alikuwa na mazungumzo na Bwana Abbas na Bwana Olmert, akijaribu kusuluhisha misimamo ya pande zote kuhusu serikali mpya ya Palestina.Baada ya kufanya mazungumzo na Bwana Abbs, Bi. Rice alisema, Marekani itasubiri na kutoa uamuzi wake baada ya kuanzishwa kwa serikali mpya ya Palestina. Lakini hali ilivyo ya sasa imeonesha kuwa, msingi wa serikali mpya ya Palestina si rahisi kukidhi matakwa ya jumuiya ya kimataifa.

Kadiri msimamo wa Marekani unavyoonekana wazi siku hadi siku, ndivyo Israeli inavyoshikilia zaidi msimamo wake imara. Bwana Olmert tarehe 19 alisema, Israel haitatambua serikali yoyote ya Palestina ambayo haikubali masharti matatu yaliyotolewa na jumuiya ya kimataifa, tena haitafanya mawasiliano na waziri yeyote wa serikali hiyo. Lakini alisema Israel itadumisha mawasiliano na Bwana Abbas.

Na Bwana Abbas ameulalamikia sana misimamo ya Marekani na Israel. Habari kutoka upande wa Palestina zinasema, Bwana Abbas alikasirika sana baada ya kuambiwa kuwa Marekani itasusia serikali mpya ya Palestina. Bwana Abbas alisisitiza kuwa ataendelea kuwajibika na mazungumzo kati ya Palestina na Israel, lakini siyo suala la kuhusu serikali mpya inayoundwa.

Wachambuzi wanaona kuwa Bi. Rice amesema atarudi tena hivi karibuni kwenye mashariki ya kati, hii imeonesha kuwa Marekani imeanza kutilia maanani tena suala la Palestina na Israel, Marekani ikiwa nguvu kuu ya kuathiri hali ya mashariki ya kati, ushiriki wake kwenye mazungumzo hakika utasaidia kuhimiza mchakato wa amani ya mashariki ya kati.