|
Makamu wa rais wa Marekani Bwana Dick Cheney tarehe 20 alasiri alifika Tokyo kuanza ziara yake ya siku mbili nchini Japan. Wakati wa ziara yake Bwana Cheney atafanya mazungumzo na viongozi wa Japan kuhusu usalama wa Bara la Asia na mapambano dhidi ya ugaidi kote duniani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bwana Cheney kufanya ziara nchini Japan katika miaka mitatu iliyopita, ambapo itakuwa mara ya kwanza kwake kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Japan Bw Shinzo Abe. Kutokana na mpango uliowekwa, tarehe 21 Bwana Cheney atakutana na kufanya mazungumzo na mfalme wa Japan Akihito, waziri mkuu Shinzo Abe na waziri wa mambo ya nje Taro Aso, ambapo watabadilishana maoni kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea, suala la nyuklia la Iran na hali ya Iraq. Aidha, Bwana Cheney atakagua kituo cha jeshi la baharini cha jeshi la Marekani huko Yokosuga, Japan, pia atasikiliza taarifa ya maofisa wa jeshi la Marekani nchini Japan na maofisa wa kikosi cha kujilinda cha Japan kuhusu suala la ulinzi.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, jukumu kuu la Bwana Cheney katika ziara yake hiyo nchini Japan ni kutoa ufafanuzi wa sera mpya ya Marekani kwa Iraq aliyotangaza rais Bush katikati ya mwezi Januari mwaka huu, kuhusu kuongeza askari zaidi ya elfu 20 wa jeshi la Marekani nchini Iraq, na kutafuta uelewa na ushirikiano wa upande wa Japan kwa Marekani. Tokea vita vya Iraq ianze mwaka 2003, Japan ikiwa nchi mshirika muhimu wa Marekani barani Asia, siku zote inaiunga mkono Marekani, si kama tu ilitunga sheria husika kutuma kikosi cha kujilinda nchini Iran, bali pia imeahidi kutoa misaada ya fedha na miradi ya msaada kwa Iraq. Lakini nchini Japan, watu wa makundi tofauti ya kisiasa wana maoni tofauti juu ya sera hiyo ya serikali ya Japan kuhusu Iraq. Wapinzani wanasema, kutuma kikosi cha kujilinda nchini Iraq kunashutumiwa kukiuka katiba ya amani ya Japan, na pia wanahofia kuwa utandawazi wa kijeshi utafanyika kati ya Japan na Marekani.
Siku chache kabla ya Bwana Cheney kufanya ziara nchini Japan, waziri wa ulinzi wa Japan Fumio Kyuma na waziri wa mambo ya nje wa Japan Taro Aso kwa nyakati tofauti waliikosoa sera ya Marekani kuhusu Iraq, ni dhahiri kuwa hii imekuwa athari mbaya kwa ziara hiyo ya Bwana Cheney. Waziri wa ulinzi wa Japan Fumio Kyuma tarehe 24 Januari aliwaambia waandishi wa habari kuwa, rais Bush alianzisha vita kwa kisingizio kuwa Iraq inamiliki silaha za nyuklia, lakini naona huu ni uchambuzi wa makosa. Ingawa baadaye waziri mkuu wa Japan Bw Shinzo Abe alisema maoni ya Bw Fumio Kyuma ni maoni yake binafsi, na baraza la mawaziri la Japan lina maoni ya pamoja kuhusu vita vya Iraq, lakini hayo hayakuifurahisha Marekani, hata baada ya hapo Marekani iliilaani serikali ya Japan kwa njia ya kidiplomasia, na kulalamikia maneno aliyosema Bwana Kyuma. Lakini kwa kweli hii siyo mara ya kwanza kwa Bwana Kyuma kuilaani Marekani. Mapema mwezi Desemba wa mwaka jana, Bwana Kyuma aliwahi kusema hadharani kuwa, serikali ya Japan haikuunga mkono rasmi vita vya Iraq. Maneno aliyosema yaliikasirisha sana serikali ya Rais Bush, hata ofisa wa serikali ya Marekani alisema kama Bwana Kyuma Fumio hatafuta maneno hayo, Marekani itafuta mazungumzo kati ya maofisa waandamizi wa wizara za mambo ya nje na wizara za ulinzi za Marekani na Japan. Katika ziara yake hiyo, Bwana Cheney hatakutana na Bwana Kyuma, bali atakutana moja kwa moja na makamanda wa kikosi cha kujilinda cha Japan. Ni dhahiri kwamba hii imeonesha malalamiko makali ya Marekani kwa Bw Kyuma.
|