Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-21 18:08:12    
Chakula cha Kichina jiaozi

cri

   

Tarehe 18 ni sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina. Katika siku hiyo Wachina karibu wote wana desturi ya kula chakula cha jiaozi.

Jiaozi ni chakula kama sambusa ndogo yenye umbo la nusu mwezi na kinachopikwa kwa kuchemshwa ndani ya maji. Chakula hicho cha jadi kikiandaliwa nyumbani kinaashiria kujumuika kwa familia, na kikiandaliwa kuwakaribisha wageni kinaashiria ukarimu na heshima ya wenyeji kwa wageni. Kama wageni wa ng'ambo wakifika nchini China na kurudi makwao bila kuwahi kula jiaozi, watachekwa na kusemwa kuwa walikwenda bure nchini China.

Kwa kifupi, jiaozi ni chakula kama sambusa ndogo kilichotengenezwa kwa kijazo na sehemu ya nje ya unga wa ngano, na kinapikwa kwa kutoswa ndani ya maji na kuchemshwa.

Kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanyika ili kutayarisha jiaozi. Kwanza ni kutengeneza kijazo. Kwa kawaida kijazo kina mchanganyiko wa nyama na mboga, lakini wakati mwingine huwa na kijazo cha nyama peke yake au mboga peke yake. Wakati wa kutayarisha kijazo, kazi kubwa ni kukatakata nyama na mboga kwa kiasi kinachotakiwa na kuchanganya viungo. Wakati wa kukatakata, kisu kinapopigapiga mbao kinato kishindo, na kishindo hicho hubadilika kadiri kisu kinapopiga kwa nguvu tofauti. Watu hupenda kishindo hicho cha kukatakata kisikike mbali na kwa muda mrefu zaidi. Kwani kishindo hicho kikiwa cha muda mrefu zaidi kinaashiria kutayarishwa kwa jiaozi nyingi zaidi na maisha yanawawawia mema.

Baada ya kutayarisha kijazo kazi inayofuata ni kufunga kijazo, jiaozi hutengenezwa kwa umbo kama nusu mwezi, na sehemu yake ya nje hufungwa kwa vidole gumba na shahada. Katika sehemu ya vijijini nchini China, jiaozi huungwa kwa kutia alama kama mashuke ya ngano zikiashiria mavuno mazuri.

Baada ya jiaozi kuwa tayari, kazi inayofuata ni kuzitosa katika maji yanayochemka, na kukoroga koroga pole pole ili zisigandamane kwenye sufuria. Wakati inapochemka hutiwa maji baridi kidogo mara tatu na baada ya dakika ishirini hivi jiaozi zinakuwa tayari.

Kabla ya kula kwa wanafamilia wote, bakuli la kwanza hupaliliwa kwa ajili ya mababu kama ni tambiko, bakuli la pili ni kwa ajili ya miungu wanayoiamini na kuomba dua. Baada ya hapo ndipo jamaa wanapoanza kula, na baada ya kumaliza kula ni bora kubakiza jiaozi kadhaa kwa idadi shufwa ikiwa ni ishara ya ziada kila mwaka.

Katika mkesha wa mwaka mpya jiaozi ni chakula cha lazima, jamaa wanaofanya kazi katika sehemu nyingine ama wafanyabiashara au wanafunzi, wote hurudi nyumbani wanajumuika na wazazi wao. Wanatayarisha jiaozi kwa pamoja na kula pamoja, huku familia nzima ikifurahia sikukuu.

Jiaozi imekuwa sehemu ya utamaduni wa China, inaashiria furaha, baraka, kujumuika na upendo kati ya wanafamilia waliokuwa wanaishi katika sehemu tofauti.