Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-22 19:12:18    
Bw. Essa Han na kampuni yake ya kutengeneza mavazi na vifaa vya kiislamu

cri

Huko Xining, mkoani Qinghai kaskazini magharibi mwa China, kuna kampuni inayoitwa Yijia inayoshughulikia utengenezaji na biashara ya mavazi na vifaa vya kiislamu.

Katika karakana za kisasa za kiwanda hicho, wafanyakazi walikuwa wanatumia mitambo kwa ustadi wakitengeneza mavazi mbalimbali ya kiislamu, kama vile skafu, vishikizo vya skafu, shali, vitambaa vilivyotariziwa kwa herufi za kiarabu na mablanketi ya mtindo wa kiarabu. Mkuu wa karanaka moja Bw. Sun Zheng alieleza kuwa, mavazi na vifaa vinavyotengenezwa na kiwanda hicho vinaweza kukidhi mahitaji ya waislamu. Alisema "Bidhaa zetu zinatengenezwa kwa kufuata mila na desturi za waislamu. Bidhaa hizo zinanunuliwa sana."

   

Imefahamika kuwa bidhaa nyingi za kampuni ya Yijia zinauzwa nje ya China, na zinajulikana katika dunia ya waislamu. Hivi sasa kampuni hiyo ina mali zisizohamishika zenye thamani ya Yuan milioni 270, sawa na dola za kimarekani milioni 33, na wafanyakazi zaidi ya elfu 5, ambayo inajulikana katika sehemu ya kaskazini magharibi mwa China.

Lakini miaka kadhaa iliyopita, kampuni hiyo ilikuwa ni karakana ndogo iliyoweza kutengeneza tu skafu na vishikizo vya skafu, na ilikuwa na wafanyakazi kadhaa. Je, kampuni ya Yijia iliwezaje kupata mafanikio makubwa namna hii?

Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Essa Han ni mwanzilishi wa kampuni hiyo. Bwana huyo wa kabila la Wasala alikumbusha kuwa, katika miaka zaidi ya 10 iliyopita alipokuwa anasoma nchini Pakistan, aliona kuna aina mbalimbali za mavazi ya waislamu, hasa kofia za wanaume. Lakini waislamu wa China walikuwa wanavaa kofia nyeupe za aina moja tu.

Bw. Essa Han alisema "China ina waislamu zaidi ya milioni 20, huenda watafurahia bidhaa hizo ambazo hazipo kwenye soko la China. Kwa hiyo wakati huo nilipata wazo la kuuza kofia za waislamu zilizotengenezwa nchini Bangladesh, Pakistan na Saudi Arabia nchini China."

Bwana huyo alichuma pesa kutokana na mauzo ya kofia hizo, halafu alianza kujiuliza, je kwa nini hatutengenezi bidhaa hizi sisi wenyewe? Kwani kuna waislamu zaidi ya bilioni moja duniani kote, hili ni soko kubwa zaidi. Bw. Essa Han alisema "Nikishauza bidhaa hizo za kigeni nchini China kwa miaka miwili, nilipata soko kubwa la China. Kutokana na msingi huu, nilianza kufikiri kusafirisha bidhaa za China kwenye nchi nyingine, nikaanza kuchukua hatua za kukuza kiwanda hicho."

Mwanzoni mwa mwaka 1998 Bw. Essa Han alitumia akiba yake yote ya Yuan elfu 30 kuanzisha kiwanda kimoja katika mkoa wa Qinghai, ambayo ni maskani yake. Kutokana na kutokuwa na mtaji wa kutosha, aliwaajiri wafanyakazi watano tu ambao walikuwa wanatengeneza skafu, vishikizo vya skafu na mablanketi kwa mikono. Wakati huo mfanyakazi hodari alikuwa anaweza kutengeneza kofia 20 tu.

Ili kuongeza uzalishaji na kuinua sifa za bidhaa, Bw. Essa Han alitembelea nchi kadhaa za kiarabu, akichunguza na kujifunza ufundi wa jadi wa kutengeneza kofia. Katika matembezi hayo aliona katika nchi hizo, mavazi ya waislamu yanatengenezwa kwa mikono katika karakana ndogo mbalimbali. Alisema "Bidhaa zinazotengenezwa kwa mikono zinauzwa kwa bei kubwa. Naona ili kutimiza lengo la kuinua sifa za bidhaa na kupunguza gharama za uzalishaji, inapaswa kutumia teknolojia mpya ya kubuni bidhaa kwa kompyuta."

Bw. Essa Han alitembelea sehemu mbalimbali za China ili kutafuta viwanda vinavyoweza kutengeneza mitambo ya kisasa ya kutengeneza nguo. Mwishoni mwa mwaka 2000, kampuni ya Yijia ikishirikiana na kampuni nyingine mbili zilizopo Beijing na Qingdao, zilifanikiwa kutengeneza mitambo ya kwanza ya kutarizi kwa kutumia kompyuta.

Mbali na kofia, kampuni hiyo pia ilibuni mitambo mingine ya kutengeneza mavazi mbalimbali ya waislamu, mapambo na mablanketi. Hivi sasa waislamu wanaoishi mkoani Qinghai wakienda kuhiji huko Mecca, wananunua bidhaa za kampuni ya Yijia kama zawadi kwa jamaa na marafiki wa huko, na zawadi hizo zinapendwa sana na waislamu wa nchi nyingine.