|
Waziri mkuu wa Uingereza Bwana Tony Blair tarehe 21 Februari alitangaza kwenye baraza la chini la bunge la Uingereza kuwa, serikali ya Uingereza imeamua kupunguza idadi ya askari wake nchini Iraq kufikia 5500 kutoka 7100 ya hivi sasa katika miezi kadhaa ijayo.
Bw. Blair alifanya uamuzi huo kabla ya kutimia miaka minne tangu Uingereza na Marekani zitume wanajeshi nchini Iraq. Bw. Blair alisema, hivi sasa hali ya sehemu zilizo karibu na Basra, kusini mwa Iraq kimsingi imetulia. Tarehe 20 jeshi la Uingereza nchini Iraq lilikabidhi utawala wa Basra kwa jeshi la Iraq, hivi sasa jeshi la Iraq linaweza kushughulikia usalama wa huko, hivyo Uingereza inaweza kupunguza idadi ya askari wake. Bw. Blair alisema jambo hilo linalenga kuwaoneshea wananchi wa Iraq kuwa, Uingereza na nchi nyingine kwenye jeshi la nchi nyingi hazitaki kuweka askari wao nchini Iraq kwa muda zaidi ya uliowekwa. Lakini aliongeza kuwa, askari wa Uingereza wataendelea kuweko nchini Iraq hadi mwaka 2008, ili kusaidia kutoa mafunzo kwa askari wa Iraq, kuwaunga mkono na kulinda njia za uchukuzi na mpaka wa Iraq.
Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, akiwa rafiki mkubwa wa Marekani Bw. Blair alifanya uamuzi wa kupunguza askari nchini Iraq kutokana na mashinikizo mawili. Kwanza Bw. Blair siku zote anakosolewa na vyombo vya habari vya Uingereza kuhusu sera yake ya kuunga mkono Marekani katika suala la Iraq, na ameathirika sana kisiasa. Tangu Marekani na Uingereza zianzishe vita ya Iraq mwaka 2003, Bw. Blair siku zote analaumiwa na wanasiasa wa vyama mbalimbali na wananchi wa Uingereza, watu wanaomwunga mkono wamepungua kwa kiwango kikubwa, hata ameshurutishwa kujiuzulu mara kadhaa na chama chake cha leba. Uchunguzi wa maoni ya raia uliofanywa hivi karibuni umeonesha kuwa, hivi sasa chama cha wahafidhina cha Uingereza kinapata asilimia 40 ya uungaji mkono, ambapo kiasi hicho kwa chama cha leba kinachoongozwa na Bw. Blair ni asilimia 31 tu. Mwezi Mei mwaka huu Uingereza itafanya uchaguzi wa mikoa, Bw. Blair ataondoka madarakani mwaka huu. Hivyo lengo la Blair la kutangaza mpango wa kupunguza askari nchini Iraq ni kwa ajili ya kubadilisha hali mbaya ya chama cha leba. Uamuzi huo utaleta matokeo mazuri si kama tu kwenye uchaguzi wa mikoa unaotazamiwa kufanyika baada ya miezi mitatu, bali pia kwa yeye mwenyewe ambaye ameshika madaraka ya waziri mkuu kwa miaka kumi.
Pili, kutokana na kwamba jeshi la Uingereza limewekwa katika nchi mbili za Iraq na Afghanistan, hivi sasa linakabiliwa na kufifia kwa uwezo wake katika mapigano ya kijeshi na upungufu wa vifaa vya kijeshi. Tangu Bw Blair ashike wadhifa wa waziri mkuu, siku zote anafuata mkakati wa dunia wa Marekani, na kutuma kwa mfululizo askari kushiriki katika harakati za kijeshi nchini Afghanistan na Iraq, hayo yamezidi kwa kiwango kikubwa uwezo wa jeshi la Uingereza. Hivyo uamuzi wa Bw Blair wa kupunguza askari nchini Iraq umeonesha kuwa Bw. Blair anajitahidi kulikwamua jeshi la Uingereza kutoka kwenye matope ya vita ya Iraq.
Alipozungumzia mpango wa Uingereza wa kupunguza askari nchini Iraq, msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema mpango huo umeonesha kuwa jeshi la Uingereza limemaliza baadhi ya majukumu yake katika sehemu ya kusini mwa Iraq. Naye kiongozi wa chama cha wahafidhina cha Uingereza Bw. David Cameron alisema, chama chake kinakaribisha uamuzi wa chama cha leba wa kupunguza askari wa Uingereza nchini Iraq.
|