|
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA Bwana Mohamed El Baradei tarehe 22 alilikabidhi baraza la shirika hilo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ripoti kuhusu hali ya Iran kutekeleza azimio No. 1737 la baraza la usalama. Ripoti hiyo inasema Iran haikuacha shughuli za kusafisha uranium nzito katika muda wa siku 60 zilizowekwa. Vyombo vya habari vinaona kuwa, baada ya ripoti ya Baradei kutolewa, suala la nyuklia la Iran linafuatiliwa tena na jumuiya ya kimataifa.
Ripoti ya Bw Baradei imesema, hivi sasa Iran inaendelea kazi ya kuweka zana za kusafisha uranium nzito na kuimarisha uwezo wake wa utafiti, ili kufikia kiwango cha kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya viwandani. Ripoti hiyo imedhihirisha kuwa, kutokana na kukosa ushirikiano wa Iran, wakaguzi wa nyuklia wa IAEA hadi leo bado hawawezi kupata maendeleo nchini Iran. Ripoti hiyo inasema Iran imekataa dai la kuacha shughuli za kusafisha uranium nzito, inaendelea kutekeleza mpango wake wa nyuklia, ripoti hiyo pia imesema Iran haitumii nyuklia katika mambo ya kijeshi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moom alieleza wasiwasi wake kuhusu hali ya maendeleo ya suala la Iran, akiitaka serikali ya Iran ifuate dai la baraza la usalama la kurejesha mazungumzo na jumuiya ya kimataifa ili kutatua suala hilo kwa njia ya amani.
Nchi za magharibi zinaishuku Iran kuwa inakusudia kuendeleza silaha za nyuklia kwa kisingizio cha kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia, lakini Iran inashikilia kuwa lengo la mpango wake wa nyuklia ni kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani. Katika suala la nyuklia, Iran siku zote inachukua misimamo ya aina mbili. Tangu mwezi Desemba mwaka jana, rais Ahmadinejad wa Iran anashikilia msimamo mkali, tarehe 21 Februari mwaka huu alisema kuwa na teknolojia ya nyuklia ni muhimu sana kwa maendeleo ya Iran, Iran itajitahidi kujipatia kikamilifu teknolojia ya nyuklia katika muda mfupi kadiri iwezekanavyo. Lakini maofisa wengine wa Iran wanachukua msimamo wenye unyumbufu, wakieleza mara kwa mara kuwa Iran inapenda kutatua suala la nyuklia kwa njia ya amani ya kufanya mazungumzo.
Lakini Marekani imeweka mkazo kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran katika kazi yake ya kudhibiti sehemu ya mashariki ya kati na kuzuia kutoenea kwa silaha za nyuklia. Hadi kufikia hapo Marekani imechukua hatua nyingi dhidi ya Iran isipokuwa kufanya mashamabulizi ya kijeshi na kufanya mazungumzo ya pande mbili, lakini hatua hizo hazikupata mafanikio makubwa. Waziri wa mambo ya nje ya Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 22 Feb. alisema, Marekani haina mpango wa kupambana kijeshi na Iran. Lakini rais George Bush wa Marekani mwezi uliopita alitangaza kuweka utaratibu wa makombora ya "Patriot" katika sehemu ya mashariki ya kati, na kuamrisha kuongeza manuari nyingine za kubeba ndege kwenye sehemu ya Ghuba. Hii inamaanisha kuwa, Marekani imeanza kufanya maandalizi ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.
Baraza la shirika la nishati ya atomiki duniani linapanga kujadili ripoti ya Bw Baradei kwenye mkutano unaotazamiwa kufanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Machi. Wanadiplomasia wanaona kuwa, huenda baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litaanza kufanya majadiliano kuhusu suala la nyuklia la Iran wiki ijayo, na majadiliano hayo yatakuwa magumu, na huenda yataendelea kwa wiki kadhaa. Inamaanisha kuwa kabla ya baraza la usalama kuanza kushughulikia suala la nyuklia la Iran, pande husika za suala hilo bado zina wakati wa kutosha kurejesha mazungumzo. Jumuiya ya kimataifa inatumai kuwa, hali ya kukwama kwa suala la nyuklia la Iran itaweza kubadilika.
|