Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-23 19:35:38    
Mchina aliyeteuliwa kuwa chifu nchini Nigeria

cri

Chifu ni kiongozi wa jadi katika nchi za Afrika. Zamani nchi mbalimbali za Afrika zilikuwa na utaratibu kamili wa uchifu, chifu mkuu ndiye aliyekuwa mfalme wa nchi, na mwenye madaraka ya juu kabisa. Ili kudumisha utulivu wa kijamii, baada ya kujipatia uhuru, nchi nyingi za Afrika ziliendelea na utaratibu wa uchifu. Ingawa chifu wa leo hana madaraka makubwa kama ilivyokuwa zamani, lakini bado anachukua hadhi muhimu katika jamii na kupewa madaraka fulani. Mwaka 2001 Chifu mkuu wa Nigeria alimteua Bwana Hu Jieguo anayeishi nchini Nigeria kuwa chifu, yeye ni mchina wa kwanza na mchina pekee kuteuliwa kuwa chifu barani Afrika.

Baba yake Hu Jieguo alikwenda nchini Nigeria kutafuta njia ya kujiendeleza, na kufanya kazi nyingi katika kuhimiza ujenzi wa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Nigeria. Bwana Hu Jieguo alizaliwa mjini Shanghai mwaka 1948, mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita aliruhusiwa kwenda Nigeria kumsaidia baba yake. Baba yake alikuwa anamiliki kiwanda cha nguo, lakini Bw. Hu Jieguo hakupenda kufuata nyayo za baba yake, badala yake alipenda kufanya kazi za kutoa huduma. Hivyo alikwenda nchini Canada kusomea taaluma ya usimamizi wa hoteli. Baada ya kuhitimu masomo alirudi nchini Nigeria na kuanza kufanya kazi ya huduma katika hoteli ya Shangri-La, ambayo ni hoteli nzuri kabisa mjini Lagos. Kutokana na juhudi na werevu wake, Bw. Hu Jieguo alipata maendeleo haraka, na kupandishwa cheo hadi kuwa meneja mkuu wa hoteli hiyo, na kumiliki hisa.

Katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, nchi za magharibi ziliiwekea Nigeria vikwazo vya kiuchumi kwa kisingizio cha haki za binadamu, wawekezaji wengi wa nchi za nje waliondoka nchini Nigeria, lakini Bwana Hu Jieguo alibaki huko, ambapo aliwekeza dola za kimarekani milioni tano kwa ujenzi wa hoteli ya Jinmen mjini Lagos. Kwenye sherehe ya uzinduzi wa hoteli hiyo, waziri wa utalii na utamaduni wa Nigeria alisema: "Hoteli ya Jinmen si kama tu imetuletea utamaduni wa chakula wa China, bali pia imezidisha urafiki wa dhati kati ya watu wa China na Nigeria na hali ya kutafuta mustakabali mzuri wa siku zijazo."

Alipozungumza ni kwa nini alichagua kuwekeza katika hoteli Bw. Hu Jieguo alisema: "Wakati huo nchi nyingi za magharibi zilikuwa zikichimba mafuta nchini Nigeria, na China ilikuwa imeanza kutekeleza sera ya kuelekea nchi za nje, ambapo makampuni mengi ya China pia yalituma ujumbe kwenda barani Afrika, lakini Nigeria ilikuwa na upungufu mkubwa wa hoteli."

Katika maisha yake ya miaka zaidi ya 30 nchini Nigeria, Bw. Hu Jieguo amewahi kukumbwa na matatizo ya aina mbalimbali. Alisema:

"Shida kubwa ya kuishi nchini Nigeria ni utulivu wa kisiasa. Uasi umewahi kutokea mara nyingi nchini Nigeria, watu wengi wa nchi za magharibi waliondoka kutokana na tatizo la usalama, lakini mimi niliamua kubaki."

Vitendo vyake viliungwa mkono na serikali ya huko na watu wa fani mbalimbali, yeye mwenyewe anapendwa na wakazi wenyeji, hivyo shughuli zake zinaendelea vizuri. Mwaka 1999 Bw. Hu Jieguo alitumia dola za kimarekani zaidi ya milioni 40 kujenga shule 4 kwenye mitaa ya wakazi maskini wa Lagos, kila shule inaweza kuwa na wanafunzi zaidi ya 3000 kwa wakati mmoja. Alisema:

"Nilipokuwa nchini China niliwahi kuwa mwalimu, hivyo nafahamu umuhimu wa elimu. Nadhani wanafunzi wanaosoma katika shule hizo watakumbuka daima kuwa walipata elimu katika shule zilizojengwa na wachina, yaani kupanda mzizi wa urafiki mioyoni mwao."

Katika miaka 30 iliyopita, Bw. Hu Jieguo alionesha hisani, urafiki na upendo kwa watu wa Nigeria kwa vitendo halisi, hivyo alijulikana sana nchini humo na kupewa sifa kubwa. Alisema sababu muhimu ya kuteuliwa kwake kuwa chifu ni kuinuka kwa hadhi ya China duniani, yeye si kama tu ni chifu, bali pia ni mshauri wa rais, na pia ni mshauri wa uendelezaji wa makampuni ya wastani na madogo. Watu wa Nigeria wamefahamu kuwa, njia ya kujiendeleza ya China inawafaa sana, wanataka kujifunza uzoefu wa China, kuingiza teknolojia ya China na kuvutia uwekezaji wa China.

Baada ya kuteuliwa kuwa chifu Bw. Hu Jieguo amekuwa na shughuli nyingi zaidi kuliko zamani, anapaswa kuhudhuria mikutano ya aina mbalimbali, kuisaidia serikali ya huko kushughulikia mambo ya wachina waishio huko, hata hana wakati wa kushughulikia biashara zake mwenyewe. Wachina zaidi ya elfu 50 waishio nchini Nigeria wote wanamfahamu Bw. Hu Jieguo ambaye ni mkarimu na anayependa kuwasaidia watu.

Bwana Hu Jieguo siku zote anasaidia mawasiliano kati ya China na Nigeria, si kama tu amejenga daraja kwa wafanyabiashara wa China kuanzisha shughuli zao nchini Nigeria, kuusaidia ubalozi wa China nchini Nigeria kushughulikia mikwaruzano ya aina mbalimbali, bali pia amechangia shughuli za muungano wa amani wa taifa la China. Anatumaini kuwa wachina waishio katika nchi za nje wanaweza kushikamana ili kuonesha sura nzuri ya China, na kuchangia maendeleo ya China. Ataendelea kuishi nchini Nigeria, kufanya mchango wake kwa urafiki kati ya watu wa China na Nigeria na mawasiliano ya kirafiki kati ya China na nchi mbalimbali za Afrika.