Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-26 19:36:33    
Watibet wazungumzia filamu inayoonesha hali halisi ya zamani ya Tibet

cri

Hivi karibuni filamu inayoonesha hali halisi ya zamani ya Tibet imekuwa ikioneshwa mjini Beijing. Filamu hiyo inaonesha hali ilivyokuwa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kabla ya mkoa wa Tibet kufanyiwa mageuzi ya kidemokrasia mwaka 1959. Filamu hiyo ilisababisha hisia kali miongoni mwa Watibet.

Mtibet Bw. Tashi Wangdu mwenye umri wa miaka 73 ni mpigaji filamu hiyo, alikuwa mkoani Tibet wakati mageuzi ya kidemokrasia yalipotokea huko. Miaka ya 50 ya karne iliyopita, hali ya ndani na ya nje ya mashamba ya makabaila inaweza kuelezwa kwa neno "pepo" na "jahanamu". Bw. Tashi Wangdu alisema, alipopiga filamu hiyo hali ya fahari na anasa ndani ya mashamba ya makabaila, ilimpiga bumbuazi yeye aliyekuwa maskini.

"Wakati tulipopiga picha za filamu katika shamba la Phalha, mmiliki wa shamba hilo Phalha Wangchug na mkewe walikuwa wamekwenda India. Mtumishi wa shamba hilo alikuja na mfuko mzima wa funguo alitufungulia mlango mmoja baada ya mwingine ili tupige filamu. Mali za shamba hilo zilikuwa nyingi, mvinyo na vyakula vilijaa chumba kizima, pombe za kimagharibi zilikuwa nyingi pamoja na maboksi ya peremende za Ulaya."

Mwaka jana Bw. Tashi Wangdu na wenzake walikwenda tena kwenye shamba hilo. Tashi Wangdu alisema, zamani katika shamba hilo kulikuwa na ngozi nyingi zenye thamani, vitu vya anasa vya Ulaya na nyumba za starehe. Wamiliki wa shamba hilo mara kwa mara walisafiri kwenda nchi za nje, na vipodozi walivyotumia wanawake vyote vilikuwa ni vya chapa maarufu kutoka Ulaya. Lakini nje ya shamba hilo 95% ya Watibet walikuwa ni watumwa wanaoishi maisha ya kunyanyaswa.

Kabla ya mageuzi ya kidemokrasia ya mwaka 1959, Tibet ilikuwa chini ya mfumo wa utumwa, maofisa wa serikali, wahudumu wa dini na mabwanyenye waliitawala Tibet, hali hiyo ilifanana na mfumo wa Ulaya vijijini katika zama za katikati. Watawala walikuwa na haki mahsusi zote na watumwa walikuwa hawana haki yoyote, na walinyanyaswa ovyo. Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa elimu kuhusu Tibet Bw. Lhagpa Phuntshogs alisema, sheria za Tibet kabla ya mageuzi ya demokrasia ziliwagawa Watibet katika matabaka, na sheria hizo zinawanufaisha tu watawala. Alisema,

"Hapo zamani sheria za Tibet ziliwagawa watu katika matabaka matatu na ngazi tisa, kila tabaka liligawanywa katika ngazi tatu yaani ngazi ya juu, ngazi ya kati na ngazi ya chini. Thamani ya mtu inapimwa kwa mujibu wa tabaka na ngazi aliyokuwa nayo, mtu wa ngazi ya juu akiuawa thamani ya uhai wake ilipimwa kwa uzito wa dhahabu unaolingana na uzito wa mwili wake, mtu duni akiuawa thamani ya uhai wake sawa na kamba."

Bw. Lhagpa Phuntshogs alisema, kwa mujibu wa sheria, watumwa wanaweza kuuzwa na kubadilishwa kati ya makabaila, kama watumwa wakioana walitakiwa kulipa kiasi fulani cha fedha, na watoto wao pia ni warithi wa utumwa. Watumwa wakiathiri vibaya maslahi ya mabwana wao waliuawa au kutiwa gerezani. Hizo ni zama giza ambazo hakukuwa na usawa na demokrasia.

Filamu hiyo ilionesha maisha halisi ya watumwa na ombaomba kabla ya kuwepo kwa mageuzi ya demokrasia. Baada ya mageuzi ya demokrasia katika mwaka 1959, maisha yao yalikuwa na mabadiliko makubwa, mfumo wa utumwa ulifutiliwa mbali na kila Mtibet ana haki sawa, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu, hali ambayo ilikuwa haipo kabisa kwa watumwa.

Mtibet Bw. Sherab Nyima aliyezaliwa mwaka 1955 ni naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Makabila cha Beijing na pia ni mtaalamu wa sheria na historia ya Tibet. Neno "sherab" maana yake ni "akili" na neno "nyima" maana yake ni "jua" kwa lugha ya Kitibet, wazazi wake walipompatia jina hilo wakiwa na matumaini kuwa atakuwa na mustakbali mzuri. Baada ya mageuzi ya demokrasia kutokea mkoani Tibet alianza kusoma na baadaye kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Baada ya kutazama filamu hiyo alikuwa na mawazo mengi, alisema elimu ilibadilisha maisha yake na hivi sasa watoto mkoani Tibet wana fursa nyingi zaidi za maendeleo. Alisema,

"Hapo zamani mkoani Tibet hakukuwa na shule, lakini sasa shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu vipo. Tokea Chuo Kikuu cha Makabila cha Beijing kianzishwe katika miaka ya 50 ya karne iliyopita kimekuwa kinapokea wanafunzi wa Tibet toka mwanzo, wanafunzi hao wanatoka kutoka sehemu mbalimbali na wote wanasoma kwa bidii. Baada ya kuhitimu, wanafunzi hao wanaweza kuendelea zaidi na masomo na kupata shahada ya pili na ya tatu."

Wataalamu wa Tibet walisema, mtu yeyote hawezi kukana maendeleo makubwa yaliyokana na mageuzi ya demokrasia mkoani Tibet. Mtaalamu wa utafiti wa maendeleo ya dini ya Buddha ya Kitibet Bw. Ta Tenzin alisema, mfumo wa kisiasa unaotekelezwa sasa mkoani Tibet umewaletea Watibet haki sawa, ikiwemo haki ya uhuru wa kuamini dini. Alisema,

"Watibet wana uhuru kamili wa kuamini dini. Hivi sasa waumini wa dini ya Buddha ya Kitibet ni wengi kama zamani, sehemu zote za kufanyia ibada ni wazi kwa wote, kwa hiyo waumini wanaweza kuomba dua na kufanya ibada kila siku."

Mtaalamu huyo aliongeza kuwa, watu waliowahi kuishi katika miaka 50 iliyopita mkoani Tibet, kama wakitazama filamu hiyo hakika watakumbushwa maisha yao ya kuhuzunisha, na watu wanaotaka kufahamu hali ya maendeleo mkoani humo, filamu hiyo pia ni filamu nzuri ya kuwaonesha maendeleo makubwa yaliyopatikana kutokana na juhudi za serikali.

Idhaa ya Kiswahili 2007-02-26