|
Wajumbe wa ngazi ya juu wa nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Marekani, Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani walifanya mkutano tarehe 26 huko London wakijadili ni hatua gani zichukuliwe ili kuhimiza ufumbuzi wa suala la nyuklia la Iran. Mkutano huo ulilenga kusawazisha misimamo ya pande husika mbalimbali kabla ya baraza la usalama kujadili suala la nyuklia la Iran mwanzoni mwa mwezi ujao.
Mjumbe wa Uingereza alidokeza kuwa, nchi zote zilizohudhuria mkutano huo zimekubali kuchukua hatua kali za vikwazo dhidi ya Iran, ili kuishinikiza Iran ifuate maazimio husika ya baraza la usalama, na kuacha shughuli za kusafisha uranium. Hatua hizo huenda zitakuwa pamoja na kupiga marufuku ya kusafiri kwa watu wa Iran wanaoshiriki katika mpango wa nyuklia na mpango wa makombora, kupunguza kiasi cha bidhaa za Iran zinazosafirishwa barani Ulaya, na kuweka kikomo cha silaha zitakazosafirishwa nchini Iran. Mkutano huo pia umekubali kutunga muswada mpya wa azimio la baraza la usalama kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran.
Wakati huo huo mapambano ya kimaneno na kidiplomasia kati ya Marekani na Iran yanaendelea kupamba moto. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alisema mpango wa nyuklia ni "garimoshi lisilokuwa na breki", ambalo haliwezi kuzuiliwa. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice alisema, Iran inalazimika kuacha shughuli zake za kusafisha uranium, ama sivyo Marekani haitafanya mazungumzo nayo. Mjumbe wa mazungumzo ya nyuklia wa Iran Bwana Ali Larijani alisema, Marekani haina udhati, Iran haitafanya mazungumzo na Marekani katika hali ya kuwekewa masharti.
Kwa upande mwingine makamu wa rais wa Marekani Bw. Dick Cheney hivi majuzi alitembelea Oman inayopakana na Iran kwa mlango wa bahari wa Hormuz, ziara inayoonekana kuwa ni ishara ya Marekani kuanzisha vita dhidi ya Iran. Habari zinasema Oman imeliruhusu jeshi la angani la Marekani kutumia vituo vyake vya jeshi la anga. Wakati huo huo wachunguzi wa kijeshi wa Marekani wamesema, majeshi ya Marekani na Iraq yamekamata silaha nyingi nchini Iraq zinazodhaniwa kuwa ni za Iran. Na upande wa Iran pia umeimarisha juhudi zake za kidiplomasia, rais Ahmadinejad tarehe 26 aliitembelea Sudan na kujaribu kujipatia uungaji mkono wa nchi nyingi za kiislamu.
Jambo linalosumbua watu ni kwamba, japokuwa baraza la usalama litaiwekea vikwazo vikali Iran, lakini Iran imeeleza msimamo wake wa kutotekeleza azimio jipya litakalopitishwa na baraza la usalama, na kuendelea na mpango wake wa nyuklia. Hali hiyo imeleta changamoto kubwa kwa juhudi za amani za jumuiya ya kimataifa.
Marekani inapoweka shinikizo la kijeshi na kidiplomasia dhidi ya Iran pia inatumai kuhimiza mabadiliko ya kisiasa nchini Iran. Ufaransa inatumai kuwa Iran itakubali pendekezo la Umoja wa Ulaya ili suala lake lisishughulikiwe na baraza la usalama. China na Russia siku zote zinapendekeza suala hilo litatuliwe kwa njia ya amani. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi saba za kiislamu waliofanya mkutano mjini Islamabad walitaka suala la nyuklia la Iran litatuliwe kwa njia ya amani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon pia ameitaka Iran ibadilishe msimamo wake, na kutumai kuwa Umoja wa Ulaya utatoa mchango zaidi katika kutatua suala hilo. Hivyo bado kuna uwezekano wa suala hilo kutatuliwa kwa njia ya amani, la muhimu ni kwamba pande mbili za Marekani na Iran ziache uhasama, na zijenge uaminifu kati yao.
Idhaa ya kiswahili 2007-02-27
|