|
Makamu wa rais wa Marekani Bwana Dick Cheney katika muongo wa tatu wa mwezi Februari alifanya ziara nchini Japan, Australia, Oman, Pakistan na Afghanistan. Naibu mkuu wa taasisi ya uhusiano wa kimataifa katika chuo kikuu cha umma cha China Bwana Jin Canrong alizungumzia lengo la ziara hiyo na mafanikio aliyopata. Alisema nia ya Bw. Cheney kufanya ziara nchini Japan na Australia ni kupunguza hali ya wasiwasi wa nchi hizo mbili kuhusu suala la Iraq na suala la nyuklia la peninsula ya Korea, na kupata uungaji mkono wao. Akisema "Hivi sasa Marekani inakabiliwa na changamoto ya kupunguza jeshi nchini Iraq. Uingereza ambayo ni rafiki yake mkubwa imeanza kupunguza askari wake nchini Iraq, hivi sasa Marekani inahitaji sana kupata uungaji mkono wa kisiasa kutoka kwa marafiki wengine, hivyo lengo lake la kwanza la kutembelea Japan na Australia ni kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na nchi hizo mbili, kwa jumla ziara yake hii imepata mafanikio."
Lakini alipofanya ziara nchini Japan na Australia alizungumzia nguvu ya kijeshi nchini China. Tarehe 21 alipofanya mazungumzo na waziri mkuu wa Japan walijadiliana kuhusu "kuimarika kwa jeshi la China na kuongezeka kwa athari ya China duniani". Tarehe 23 alipofanya ziara nchini Australia alieleza wasiwasi kuhusu "kuimarika kwa jeshi" la China.
Habari zinasema waziri mkuu wa Australia Bwana John Howard hakukubaliana na maoni ya Bw. Cheney, alisema katika miaka kumi iliyopita uhusiano kati ya Australia na Marekani umeimarika zaidi, na wakati huo huo Australia pia imejenga uhusiano wa kiujenzi na unaoeleweka na China. Bw. Jin Canrong alisema China ni nchi kubwa duniani, na hivi sasa inapata ongezeko kasi la uchumi, inaeleweka kwa nchi nyingine kuwa na wasiwasi kuhusu maendeleo yake makubwa, lakini mazungumzo ya Bw. Cheney yamedhihirisha vigezo viwili vya Marekani.
Bwana Cheney pia alifanya ziara ya ghafla nchini Pakistan na Afghanistan. Bw. Jin Canrong alisema hivi sasa Marekani inakabiliwa na changamoto kubwa katika medani za Iraq na Afghanistan, lakini serikali ya Bw Bush inaweka mkazo zaidi nchini Iraq, hivyo anatumai serikali za Afghanistan na Pakistan na nchi marafiki wa NATO zitabeba wajibu mkubwa zaidi nchini Afghanistan. Hivyo lengo la Bw Cheney kuzitembelea nchi hizo mbili ni kuziwekea shinikizo.
Ziara ya Cheney nchini Oman imefuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Pande hizo mbili zimejadiliana kuhusu hali ya usalama wa kikanda na suala la nyuklia la Iran. Habari zinasema Oman imeliruhusu jeshi la angani la Marekani kutumia vituo vyake vinne vya kijeshi. Bw. Jin Chanrong alisema: "Ziara ya Bw. Cheney nchini Oman ni kutokana na hadhi yake muhimu ya kijiografia. Uhusiano kati ya Marekani na Iran ni suala litakalofuatiliwa zaidi na jumuiya ya kimataifa mwaka huu, Cheney alipofanya ziara nchini Australia alisisitiza kufanya mazungumzo na Iran, lakini haiachi chaguo lingine."
Bw. Jin alisema, ziara hii ya Bw. Cheney katika nchi za Asia na Pasifiki imedokeza mambo matatu: "Shughuli hizo za kidiplomasia zimeonesha kuwa, hadhi ya Bw. Cheney katika serikali ya Bw Bush bado ni imara, na maneno yake yenye msimamo mkali yameonesha kuwa athari yake bado ipo. Wakati Bw. Cheney anapokabiliwa na shinikizo kutoka nchini na nchi za nje, anategemea zaidi uungaji mkono wa nchi marafiki wa Asia. Jambo la tatu ni kufuatilia msimamo wake kuhusu suala la nyuklia la Iran siku zijazo."
Idhaa ya kiswahili 2007-02-28
|