Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-02-28 20:22:57    
Serikali ya Tanzania yaingiza uganga wa asili katika mfumo rasmi wa matibabu

cri

Shirika la afya duniani limesema wataalamu wa Uganda wa asili, za kisasa na mambo ya kijamii kwa ujumla wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba watu wengi wanapata dawa salama, za uhakika, zenye sifa bora na bei rahisi ikiwa ni pamoja na kutopuuza dawa za mitishamba.

Hivi sasa nchini Tanzania uganga wa asili umeingizwa katika mfumo rasmi wa matibabu baada ya kuonekana kuwa na manufaa makubwa kiafya sambamba na tiba ya kisasa. Mwaka 2000 kikao cha 50 cha Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika kilipitisha Mkakati kwa kufikia azimio la kukuza mchango wa uganga wa asili katika mfumo unaojulikana kama `Mkakati kwa Kanda ya Afrika'. Hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa wakuu wa nchi na viongozi wa serikali za Afrika, kukitangaza kipindi cha mwaka 2001 hadi 2010 kuwa cha mwongozo wa Uganga wa asili barani Afrika.

Shirika la Afya Duniani lilisema, mitishamba ya Afrika imepatiwa nembo rasmi na uzinduzi wa nembo hiyo ulifanyika Oktoba 8 mwaka 2003. Nchini Tanzania waganga wa tiba za asili wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa uwazi kufuatia hatua ya serikali kufungua milango ya ushirikiano kati yao na waganga wa tiba za kisasa, hasa baada ya huduma ya matibabu kutambuliwa katika mfumo rasmi wa utoaji wa matibabu katika Wizara ya Afya ya Tanzania.

Mwaka 2005 serikali ya Tanzania iliunda baraza la Waganga wa uganga wa asili na tiba mbadala likalofanya kazi zake chini ya Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Asili na Chuo Kikuu kishiriki cha Sayansi ya Tiba Muhimbili Jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa baraza hilo aliyeteuliwa na Rais, Profesa Rogasian Mahunnah anasema kuundwa kwa baraza hilo kumefanikisha ushirikiano wa wataalamu wa uganga wa asili na tiba za kisasa. Alisema baraza hilo limeunganisha wataalamu wa pande zote mbili, tofauti na siku za nyuma ambapo waganga wa uganga wa asili walidharauliwa.

Amesema waganga wa tiba za asili wana umuhimu sawa na wadaktari wa tiba ya kisasa kwa kuwa lengo lao moja ambalo ni kutibu na kuponya wagonjwa hivyo ni lazima washirikiane kwa uwazi zaidi ili kufanikisha lengo hilo. Profesa Mahunnah alisema dhana iliyojengeka miongoni mwa watabibu hao wa jadi, kuwa waganga wa kisasa wana nia ya kupokonya mbinu na ugunduzi wao wa mitishamba, haina ukweli kwa kuwa nia ya serikali na wataalamu wa kisasa ni kuwajengea uwezo wa uelewa na namna ya kutibu kisasa bila kupoteza uasili wa dawa zao ili kushindana sawa na waganga wa tiba za asili wa nje ya nchi.

Anasema changamoto kubwa inayowakabili waganga wa tiba za asili wa Tanzania ni kuwa na mtazamo wa kutibu kitaifa na kimataifa ikiwa ni sehemu ya kutangaza dawa za asili hasa zitokanazo na mitishamba kama waganga wa asili wa China na Thailand, ambao dawa zao zinauzwa karibu robo tatu ya dunia.

Prof. Mahunnah amesema utafiti unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanapatiwa matibabu kwa njia ya dawa za asili hasa za mitishamba. Anasema kuna uwezekano mkubwa wa ongezeko la wastani huo, kama waganga wangejitokeza na kutambulisha dawa zao ili zifanyiwe utafiti. Anasema serikali inawatambua waganga wa tiba za asili baada ya utafiti kuonesha kuwa dawa zao ni muhimu katika kampeni yake ya kutokomeza magonjwa mbalimbali ambayo kinadharia yanaonekana kuwa sugu.

Pamoja na kuwashirikisha waganga wa tiba za asili katika siku ya Tiba ya Mwafrika, Baraza hilo pia limekuwa likiandaa makongamano ya mafunzo na kubadilishana uzoefu kati ya waganga wa tiba za asili na wataalamu wa tiba za kisasa.