Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-01 16:28:41    
Shirika la ufumaji la wanawake mjini Hanzhou

cri

Kwa watu wengi ufumaji unaofanywa kwa mikono ni jambo la kupitishia muda, lakini katika baadhi ya sehemu nchini China, ufumaji unaofanywa kwa mikono ni chanzo muhimu cha mapato ya baadhi ya familia. Shirika la ufumaji la wanawake la mji wa Hangzhou, mkoani Zhejiang, mashariki mwa China limewasaidia wafanyakazi wanawake wengi wasiokuwa na ajira kupata ajira tena.

Shirika hilo lilianzishwa mwezi Machi mwaka 2002, hivi sasa lina wafanyakazi wanawake zaidi ya 500. Bibi Xu Qiming ni mkuu wa shirika hilo, alisema kazi nyingi za shirika hilo ni kazi za sanaa za ufumaji na ushonaji wa mikono, kama vile nguo na kofia za wanasesere, na vitu vya sanaa za mikono. Shirika hilo linawalipa wafanyakazi wake kutokana na kazi wanazofanya, wale hodari wanaweza kupata Yuan zaidi ya 2000 kwa mwezi. Bi. Xu Qiming alisema:

"Tunawasimamia wafanyakazi wetu kwa kufuata utaratibu wenye unyumbufu, kama wanashikilia kufanya kazi kwenye shirika letu, mapato yao kwa mwezi yanaweza kuwa zaidi ya Yuan 1000. Baadhi yao kama wanalazimika kubaki nyumbani kuwatunza wazee na watoto, wanaweza kwenda na kazi nyumbani."

Shirika hilo la ufumaji ni la utoaji hisani, kwenye mtaa lilipo shirika hilo, kuna wafanyakazi wanawake wengi wasiokuwa na ajira, kwa sababu umri wao ni mkubwa kiasi, hawakupata elimu nzuri, tena hawana ustadi maalum wa kazi, hivyo ni vigumu kwao kupata ajira tena. Ili kuwasaidia wafanyakazi hao wanawake wapate ajira tena, makada wa mtaa huo wameanzisha shirika la ufumaji. Mwanzoni shirika hilo lilikodisha chumba kimoja na kuwa na wafanyakazi wachache tu. Hatua kwa hatua shirika hilo limepanuka, kazi za sanaa za mikono zinazotengenezwa na shirika hilo zinapendwa na watalii.

Bi. Cai Lingqiong mwenye umri wa miaka 48 ni mlemavu, mwaka 2003 alipunguzwa kazi kiwandani. Mume wake pia ni mlemavu, pato lake la mwezi ni Yuan 1000 hivi, mwanao anasoma shule ya sekondari. Hivyo familia yake inaishi maisha magumu. Bi. Cai alisema, sifa kubwa ya shirika la ufumaji la wanawake ni kufuata utaratibu wenye unyumbufu, wafanyakazi wake wanaruhusiwa kwenda na kazi nyumbani. Akisema:

"Nikichukua kazi za kufanyia nyumbani naweza kumtunza shangazi yangu ambaye ni mzee na mgonjwa. Ikiwa kila siku nalazimika kufanya kazi kwenye shirika la ufumaji, nitashindwa kumtunza mgonjwa nyumbani."

Mkuu wa shirika la ufumaji la wanawake Bi. Xu Qiming alisema, kwa wafanyakazi wanawake wengi wa shirika hilo, si kama tu wameajiriwa tena, bali pia wamerejeshewa imani yao. Kazi za ufumaji na ushonaji ni rahisi kujifunza hata kwa wale wasiokuwa na ustadi wowote. Chumba cha shirika la ufumaji la wanawake kilikodiwa na mtaa, kazi za sanaa za mikono baada ya kuuzwa, faida zote zinatumiwa kulipa mishahara licha ya kulipia maji na umeme, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwa kiwango kikubwa mapato ya wafanyakazi wanawake hao. Hivi sasa shirika la ufumaji la wanawake linajulikana, wanawake kutoka mitaa mingine pia wameomba kujiunga na shirika hilo. Na baada ya juhudi za wafanyakazi wanawake, shughuli za shirika hilo zinapanuka siku hadi siku. Bi. Xu Qiming alisema:

"Mwanzoni tulifanya kazi za sanaa za mikono zenye thamani ya Yuan elfu kadhaa tu kwa mwaka, ilipofika mwaka jana mishahara iliyotolewa na shirika ilikuwa zaidi ya Yuan laki saba. Hivi sasa tunapokea kazi nyingi kutoka nje, baadhi ya kazi zinahitaji wafanyakazi 700 hadi 800."

Kutokana na sifa bora za kazi na kumaliza kazi kwa wakati, shirika la ufumaji la wanawake limepata imani kubwa ya makampuni. Makampuni mengi maarufu ya mkoani Zhejiang yamesaini mikataba ya muda mrefu na shirika hilo. vitu vya sanaa vinatengenezwa na shirika hilo pia vimeuzwa katika nchi za nje.

Kutokana na kuongezeka kwa shughuli za shirika hilo, wafanyakazi wanawake zaidi ya 20 wamekwenda kwenye sehemu nyingine karibu na mji wa Hangzhou kuwashirikisha wanawake wa vijijini, na kuwanufaisha wanawake wengi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-01