Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-01 14:57:16    
Mkahawa wa Starbucks ulioanzishwa ndani ya Kasri la kifalme la China wazusha mjadala

cri

Kasri la kifalme la China liitwalo Forbidden City lipo katikati ya mji mkuu wa China, Beijing. Kasri hilo lina historia ya miaka zaidi ya 600, liliwahi kutumika na wafalme wa China katika enzi za Ming na Qing, ambazo ni enzi za mwisho za kifalme katika historia ya China. Hivi sasa kasri hilo linawavutia watalii wengi sana wa China na wa ng'ambo. Hivi karibuni ulizuka mjadala mkubwa uliosababishwa na mkahawa mmoja wa kigeni kuanzishwa ndani ya kasri hilo.

Katika sehemu ya mashariki ya uwanja mbele ya mlango wa Qianqing, ndani ya kasri la kifalme, kuna safu ya nyumba za kale zenye kuta za rangi ya manjano na paa jekundu. Katika enzi za kifalme, maofisa walikuwa wanasubiri ndani ya nyumba hizo kabla ya kukutana na wafalme. Kati ya nyumba hizo, nyumba moja iliyopo kwenye magharibi ya safu hiyo, sasa ni mkahawa wa Starbucks uliosababisha kuzuka kwa mjadala. Kando ya mkahawa huo kuna duka moja linalouza vijitabu na vitu vya kumbukumbu vinavyohusu kasri la kifalme.

Hivi sasa hapa Beijing ni majira ya baridi kali. Mtalii mmoja kutoka Shanghai Dada Zhou Fang akilikuwa akinywa kahawa huku akisema  "Katika siku za baridi namna hii, tunaweza kununua kinywaji cha moto. Si mbaya."

Mkahawa huo wa Starbucks ulianzishwa mwaka 2000, wakati huo watu waliwahi kufuatilia hatua hiyo ya kuanzisha mkahawa wa kigeni ndani ya kasri la kifalme la China. Mwezi Januari mwaka huu, makala moja iliyotolewa kwenye mtandao wa internet iliwafanya watu wafuatilie suala hilo kwa mara nyingine tena. Katika kipindi cha siku 6, makala hiyo yenye kichwa cha "Starbucks iondoke kasri la kifalme la China" ilisomwa zaidi ya mara laki 5. Makala hiyo inasema Starbucks ni sehemu ya utamaduni wa chakula wa Marekani ambao si wa hali ya juu, haifai kuanzisha mkahawa ndani ya kasri la kifalme la China ambalo linaonesha utamaduni unaong'ara wenye historia ndefu wa China, kwa hiyo inafaa kwa Starbucks iondolewe kutoka kwenye kasri hilo.

Kati ya ujumbe mwingi uliojibu makala hiyo, watu wanaounga mkono maoni ya makala hiyo ni wengi zaidi kuliko watu wanaopinga. Ujumbe mmoja unasema, "tunapaswa kuhifadhi utamaduni na raslimali zetu, haturuhusu ziharibiwe." Ujumbe mwingine unasema, "Utamaduni wa chakula cha haraka wa Marekani usiingilie majengo yetu ya kale." Mabishano kuhusu tukio hilo pia yaliendelea kwenye vyombo vingine vya habari vya China.

Katika kasri la kifalme, mwandishi wetu wa habari alizungumza na watalii kadhaa wa kigeni kuhusu tukio hilo. Watalii walieleza maoni yao, wakisema Starbucks kuanzisha mkahawa ndani ya kasri la kifalme kumeharibu mazingira ya kasri hilo lenye historia ndefu.

Bw. Raul Vasquez ni Mmarekani, alisema "Naona hailingani na hali ya kasri la kifalme, labda inaweza kuanzisha mkahawa nje ya kasri hilo. Kwani kasri la kifalme ni mahala pazuri, linastahili kuheshimiwa na watu, na si mahala pa kuanzisha maduka."

Bw. Joerg Schmitz anatoka Ujerumani, alisema "Hili ni jambo zuri, kwani hapa ni sehemu ya utamaduni, lakini Starbucks inashughulikia biashara, inatakiwa kufanya biashara yake nje ya kasri la kifalme."

Imefahamika kuwa, jumba la makumbusho la kasri la kifalme ambalo ni idara inayoshughulikia hifadhi ya kasri la kifalme, lilipoandaa mpango wake kati ya mwaka 2004 na 2005, lilijadili suala la makahawa wa Starbucks. Mwaka 2005 Starbucks ilibadilisha mapambo ya nje ya nyumba ya mkahawa huo, hivi sasa hakuna nembo yoyote inayolingana na Starbucks ionekane nje ya mkahawa huo. Baada ya mabadiliko hayo, baadhi ya watu walikubali kuwepo kwa mkahawa huo, wakisema mkahawa huo unaweza kuwahudumia watalii wanaotaka kinywaji bila kuharibu mazingira ya kasri la kifalme.

Mtalii Mchina Bibi Wang Ping alisema "Tunaweza kununua vinywaji, mkahawa huo unatoa huduma. Tena unachukua sehemu ndogo tu, hapa huwezi kuona utamaduni wa kimagharibi unaotiliwa mkazo."

Lakini mtalii mmoja wa Marekani Bw. Rob Mullin alisema, atafurahia zaidi kupata vinywaji vya Kichina anapotembelea kasri la kifalme la China. Alisema  "Natarajia zaidi kunywa chai ya Kichina hapa."

Kasri la kifalme ni jamii ya majengo ya kifalme yenye eneo kubwa kabisa duniani, eneo lake ni hekta zaidi ya 70. Watalii wakitembelea kasri kubwa kama hilo, wanasikia uchovu na kiu, kwa hiyo haifai kutoruhusu kuanzishwa kwa mkahawa ndani ya kasri hilo. Mkurugenzi wa ofisi ya jumba la makumbusho la kasri ya kifalme Bw. Feng Naien alimwambia mwandishi wa habari kuwa, watalii karibu milioni 10 wanatembelea kasri hilo kila mwaka, mbali na kuhifadhi kasri hilo, pia inapaswa kuwapatia watalii huduma bora, zikiwemo huduma za chakula na vinywaji.

Bw. Feng Naien aliongeza kuwa, kama linatokea tatizo kati ya biashara ya mkahawa wa Starbucks na shughuli za kuhifadhi kasri la kifalme, kwa uhakika upande wa kasri la kifalme utashikilia kanuni ya kuhifadhi kasri. Hivi sasa upande wa kasri hilo unajadiliana na Starbucks kuhusu hatma ya mkahawa huo, matokeo yanatarajiwa kupatikana kabla ya mwezi Juni mwaka huu. Pamoja na hayo, upande wa kasri la kifalme pia unatafuta mbinu mpya za usimamizi na kujiendeleza.

Bw. Feng Naien alisema "Tulishapata kampuni moja ya kutoa ushauri kwa njia ya zabuni. Kampuni hiyo itatusaidia kupanga shughuli za kujiendeleza. Mpango wetu utakapokamilishwa, suala kama la Starbucks hakika litatatuliwa."

Bw. Feng pia alieleza kuwa, hivi sasa kwa kupitia njia ya zabuni, wamepata kampuni itakayotoa huduma za chakula, na wanajadili masuala mbalimbali, kama vile bidhaa gani zinastahili kuuzwa kwenye kasri la kifalme, jinsi bidhaa hizo zinavyoweza kuonesha umaalumu wa kasri la kifalme na namna ya kukidhi mahitaji ya watalii. Bw. Feng Naien aliongeza kuwa, mpango husika utatangazwa hadharani katika nusu ya kwanza ya mwaka huu. Kwa mujibu wa mpango huo mpya, inapaswa mahala pa kuanzishwa mikahawa palingane na mazingira ya kasri la kifalme, pia mikahawa hiyo itawahudumia vizuri watalii.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-01