Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-02 15:13:24    
Ushirikiano kati ya Afrika na China wanufaishe wananchi

cri

Mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing, mji mkuu wa China, ulimazilika kwa ahadi mbalimbali kutolewa. Katika makala ya maoni ya mhariri iliyochapishwa kwenye gazeti la Nipashe la Tanzania, mhariri alieleza kufurahia ushirikiano kati ya Afrika na China na makubaliano yaliyofikishwa kwenye mkutano huo. Ifuatayo ni makala hiyo yenyewe.

Mwezi Novemba mwaka jana, China iliandaa mkutano mkubwa baina yake na viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika.

Mkutano huo wa siku tatu, uliokuwa na lengo la kupanua ushirikiano baina ya pande hizo, ulimalizika kwa kusainiwa kwa mikataba kadhaa ya kimaendeleo baina ya makampuni ya China na serikali za nchi za Afrika.

Zaidi ya mikataba yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.9, ilitiwa saini kwa ajili ya kuendeleza miradi ya miundombinu, mawasiliano na teknolojia.

Aidha, katika mkutano huo China iliahidi kuongeza mara mbili zaidi misaada yake kwa Afrika na kufikia dola za Kimarekani bilioni 50 ifikapo mwaka 2009.

Katika mkutano huo uliofanyika Beijing na kuhusisha wajumbe kutoka nchi karibu 50 za Afrika, China imeahidi kuendelea na utafiti wa mafuta katika nchi kadhaa za Afrika, ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi iliyokwishaanza katika sekta hiyo barani Afrika.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Jamhuri ya watu wa China kwa kuona umuhimu wa kulisaidia bara la Afrika kujikwamua kutoka kwenye umaskini, licha ya kuwa tajiri wa raslimali mbalimbali kama vile madini, mafuta, misitu na mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Hatua hii inadhihirisha ukweli kwamba China ni rafiki mkubwa na wa kweli wa nchi za Afrika.

Hakuna asiyetambua mchango uliotolewa na China, wakati nchi nyingi za Afrika zikipigania uhuru kutoka kwa wakoloni. China ilitoa msaada mkubwa kwa harakati za ukombozi barani humo.

Na hata baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru, taifa hilo lenye watu wengi zaidi duniani, halikujiweka mbali na wananchi wa Afrika kwani liliendelea kusaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa Tanzania na Zambia, wananchi wa nchi hizo wataendelea kuuthamini mchango wa China kwa kufanikisha ujenzi wa reli muhimu ya TAZARA ambayo imerahisisha usafiri wa watu na mizigo kati ya nchi hizo na zilizo jirani.

Hivi sasa, China inaendesha miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu nchini Angola ambayo iliharibiwa vibaya wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi nchini humo.

Ni jambo la kufurahisha zaidi kuona kwamba sasa China inaingia Afrika kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya...kwa kuwekeza mabilioni ya fedha katika miradi ya mafuta, gesi, madini, chuma na mali ghafi kwa ajili ya mahitaji ya uchumi wake ambao unaendelea kukua kwa kasi.

Nchi nyingi za Afrika zina utajiri mkubwa wa raslimali za aina mbalimbali ambazo tunaamini zikipata mshirika (partner) wa kweli wa maendeleo, zinaweza kupiga hatua kubwa kiuchumi.

Kwa vile China ilishaonyesha hilo tangu awali, tunaamini awamu hii mpya ya ushirikiano itakuwa ya manufaa zaidi katika nyanja za miundombinu, tatizo kubwa linalokwamisha maendeleo ya Afrika.

Ni matarajio yetu kwamba ushirikiano huu utazingatia zaidi kuwaletea wananchi maendeleo wanayohitaji ili nao waweze kunufaika na raslimali ambazo ni urithi wetu sote.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-02