Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-02 20:44:23    
Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Kenya, Bw David Waweru azungumzia mwaka mmoja wa kituo cha FM cha Radio China kimataifa huko Nairobi na Uhusiano kati ya Radio China kimataifa na KBC

cri

Leo katika kipindi cha Daraja la Urafiki kati ya China na Afrika, mwandishi wetu wa habari wa jijini Nairobi amepata fursa ya kufanya mahojiano na mkurugenzi wa shirika la utangazaji la Kenya (KBC) bwana David Waweru.

Akielezea uhusiano wa miaka mingi kati ya shirika la utangazaji la Kenya (KBC) na Radio China Kimataifa (CRI) Bwana Waweru alisema kuwa, uhusiano uliopo ni kunufaisha pande zote mbili, kwanza katika ubadilishanaji wa teknolojia ambapo CRI imefunga mitambo ya kunasia sauti kutoka nchini China ambayo imesaidia kuboresha ubora wa matangazo ya KBC, na pili ni misaada ya kifedha, "lakini jambo hili si la muhimu sana kama teknolojia" alisema.

Bwana Waweru pia ameeleza kufurahishwa kwake na kuazishwa kwa kituo cha FM 91.9 cha Radio China Kimataifa kilichopo mjini Nairobi ambacho hivi karibuni kimetimiza mwaka mmoja, aliendelea kusema kuwa ni jambo la kufurahisha kwa CRI kuichagua Kenya kuanza kurusha matangazo ya FM kupitia KBC. Wasikilizaji wengi wa KBC wameoneshwa kufurahishwa na vipindi vya Radio China Kimataifa ambapo wamepata fursa ya kujifunza na kufahamu mambo mengi kuhusu China, lakini licha ya watu wa Kenya hata watu wa China nao wamepata nafasi ya kujua na kujifunza mengi kuhusu Kenya. Kwa mfano muziki unaosikika kwenye Radio China kimataifa umekuwa unawafanya wasikilizaji washindwe kutambua kama unachezwa kutoka Nairobi au moja kwa moja kutoka nchini China, kwa hiyo ni kituo kinachozidi kupata wasikilizaji wengi zaidi.

Akijibu swali ni picha gani aliyoipata kuhusu China na watu wake katika ziara zake mbili alizofanya nchini China, Bwana Waweru alisema "kuhusu mji nilioutembelea wa Beijing kitu cha kwanza una watu wengi sana, una watu zaidi ya milioni kumi na nane ambayo ni karibu na nusu ya idadi ya watu wa Kenya" Mji wa Beijing ni msafi sana, ni mkubwa na una maendeleo makubwa sana ambayo yanaweza kulinganishwa na ya nchi za Ulaya, watu wa Beijing ni wenye furaha na wachangamfu sana kwa wageni, kiasi kwamba ukiwa mjini humo unajihisi uko nyumbani. China ni nchi nzuri na yenye miji mingi ambayo watu wanaweza kutembelea na kujionea yale mambo ambayo pengine wanahisi yanaweza kupatikana Ulaya peke yake tu.

Akiwa mkurugenzi wa KBC, anaona uhusiano kati ya CRI na KBC katika siku za usoni utoe kipaumbele kwanza katika teknolojia, kwa sababu wachina wamepiga hatua kubwa katika teknolojia na hata vifaa vya utangazaji vya KBC vinatoka China. Pili ni katika ujuzi katika nyanja hii ya utangazaji wachina pia wameendelea sana hivyo KBC ingependa kutumia fursa hii ya ushirikiano kutuma wataalamu wake nchini China kujifunza ili waweze kujionea jinsi teknolojia ilivyoendelea.

Kwa hivi sasa KBC imeshafanya mazungumzo na wakuu wa CRI kuhusu kupata usaidizi wa matangazo ya michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, KBC ingependa ushirikiano ili wafanyakazi wake waweze kujifunza jinsi yanavyotangazwa.

Tatu kuna mpango wa kuanzishwa kwa vipindi nchini Kenya ambavyo vinaweza kuwa vya muhimu kwa kuwaelimisha wachina nchini mwao mambo wanayoweza kujionea nchini Kenya, kwa sababu Kenya ni nchi yenye vivutio vingi vya kufurahisha na watalii wengi sana wanakwenda nchini humo. Kwa hiyo matangazo hayo yakirushwa nchini China na Kenya watu watapata fursa ya kujifunza na kuelewa mambo mengi yanayoweza kuongeza ushirikiano katika nyanja za biashara, utalii na kadhalika.

Bwana Waweru alimalizia kwa kukitakia kila heri na fanaka kituo cha FM cha Radio China Kimataifa cha Nairobi kinapoingia katika mwaka wake wa pili na anapenda zaidi KBC na CRI zizidi kushirikiana kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili.