Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-05 15:41:05    
Picha za ukutani ndani ya hekalu la Pilu mkoani Hebei, China

cri

Nje ya mji wa Shijiazhuang upande wa magharibi mkoani Hebei, China kuna hekalu moja linaloitwa Pilu. Hekalu hilo limekuwepo kwa miaka zaidi ya 1200, hekalu hilo linawavutia watu wengi kutokana na picha za ukutani.

Hekalu hilo lilijengwa katika Enzi ya Tang nchini China miaka zaidi ya 1200 iliyopita, picha za ukutani zilizoko ndani ya hekalu hilo zilichorwa mwanzoni mwa karne 14, kwa hiyo picha hizo zina thamani kubwa na ni picha zilizohifadhiwa vizuri zaidi kati ya picha zote za kale zilizochorwa ukutani nchini China. Picha hizo kwa jumla zina mita 200 za mraba, na mada za picha hizo ni nyingi. Baada ya kuingia kwenye hekalu hilo, ukumbi wa kwanza ni ukumbi wa Sakyamuni, mwanzilishi wa dini ya Buddha. Ndani ya ukumbi huo kuna sanamu ya Sakyamuni aliyekaa, na kwenye kuta nne ukumbini kuna picha za kuchorwa zenye mita 80 za mraba. Picha hizo zilichorwa kwa mujibu wa hadithi zilizosimuliwa miongoni mwa watu kuhusu miungu. Mwongozaji wa watalii Bw. Tian Yatao alieleza kuwa picha ndani ya ukumbi huo zinaonesha mambo ya wa Dini za Kibuddha, Dini ya Kidao ambayo inapatikana tu nchini china na nadharia ya Confucius. Alisema,

"Picha ndani ya ukumbi huo ni picha za hadithi, kwa mujibu wa mavazi na majengo yaliyooneshwa, picha hizo zilichorwa kutokana na hali ya maisha ya watu katika miaka ya Enzi ya Ming nchini China lakini zimechanganya nadharia ya Confucius, na mada za picha hizo hazihusiani na Sakyamuni aliyeelezwa ndani ya msahafu wa Dini ya Kibuddha."

Picha zilizohifadhiwa vizuri zaidi ni picha zilizoko katika ukumbi wa nyuma, ukumbi huo unaitwa Pilu, huu ni ukumbi mkubwa zaidi katika hekalu hilo. Ukumbi huo umejengwa juu ya jukwaa lenye kimo cha mita moja kutoka ardhini. Kwenye pande mbili za mgongo wa paa la ukumbi huo kuna sanamu za dragoni na finiksi kama ni mapambo. Picha ndani ya ukumbi huo zina mita 120 za mraba ambazo zimetenganishwa katika safu tatu, yaani safu ya juu, safu ya katikati na safu ya chini. Picha hizo zinaeleza watu na miungu wa aina mbalimbali zaidi ya 500 waliopo peponi, jahanamu na duniani.

Bw. Tian Yatao alisema, kila picha iliyopo ndani ya ukumbi huo ina hadithi yake, na kila mtu kwenye picha ana simulizi zake. Kati ya watu hao kuna mwanamke mmoja ambaye ana umbo la wastani na sura ya kupendeza, huyo ni mama mtakatifu katika Dini ya Kidao.

"Wataalamu wa historia walisema, huyu mama mtakatifu alikuwa ni mtu halisi, alikuwa ni mwanamke mwenye roho nzuri na alikuwa hodari wa kuogelea. Mara kwa mara alikuwa anawasaidia wavuvi, lakini siku moja alikufa maji kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa. Wenyeji hawakuamini kuwa amekufa, walisema amekwenda peponi na kuwa mungu, kwa hiyo walimwabudu kama ni mama wa binadamu."

Ndani ya ukumbi wa Pilu kuna picha nyingi zinazoeleza hadithi kama ya mama huyo mtakatifu. Kwenye picha hizo watu wengi walichorwa wakiwa wanatofautiana, watu hao wako kwenye vikundi mbalimbali na kila kikundi kimetenganishwa na kikundi kingine kwa mawingu yenye rangi ya zambarau, kijani na ya kahawia. Ukitizama kwa makini utagundua kwamba picha kwenye ukuta wa kaskazini ndani ya ukumbi huo zinahusiana na Dini ya Kibuddha, picha kwenye kuta za mashariki na magharibi zinahusu watu mashuhuri wa Dini ya Kidao na picha kwenye ukuta wa kusini zinahusu watu wa kawaida.

Baada ya kufahamu mada za picha ndani ya ukumbi huo, sasa tuone ufundi wa picha hizo. Picha hizo zilichorwa kwa ufundi mkubwa, mpaka sasa rangi zake hazijafifia. Bw. Tian Yatao alisema,

"Picha hizi zilichorwa kama vitu halisi. Kwa mujibu wa historia, picha hizo zilipokamilika zilikuwa zinavutia sana."

Picha ndani ya hekalu la Pilu zinavutia watu wengi na wataalamu nchini China na nchi za nje na wanashtuka sana kutokana na uzuri wa picha hizo. Wanasema picha hizo ni msingi wa kutafiti maisha, mila na desturi za watu enzi za kale na sanaa za zamani. Bw. Zhang Zhen ni mkazi wa mji wa Shijiazhuang ambaye ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kutizama picha hizo alisema,

"Sikudhani kama hapa mjini kwetu kuna picha nzuri kama hizi, natumai zitadumu ili kuvionesha vizazi vyetu vya baadaye utamaduni wetu mkubwa wa zama za kale."

Ili picha hizo zidumu watunza picha hizo wanakuwa makini sana. Lakini cha kusikitisha ni kuwa kutokana na miaka mingi ya uharibifu wa maumbile, picha kadhaa zilibanduka. Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa hekalu hilo Bw. Zhou Yanping alieleza, serikali imetenga yuan laki kadhaa kwa ajili ya hifadhi na utafiti wa picha hizo, wanatumai kupata njia iliyo nzuri ya kisayansi kuzihifadhi picha hizo. Alisema,

"Kwa kufanya ufafanuzi wa kisayansi, tunatumai tutapata njia ya uhakika ya kuzihifadhi picha hizo ili kuzifanya picha hizo zidumu bila kuendelea kuharibika."

Bw. Zhou Yanping aliongeza kuwa hivi sasa picha hizo zimefunikwa kwa utando, na zimechukuliwa hatua za kiwango maalumu cha joto na unyevunyevu kwa mwaka mzima ndani ya ukumbi huo.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-05