|
Katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy tarehe 5 huko Geneva alifanya mazungumzo na wajumbe wa nchi muhimu wanachama wa WTO Marekani, Umoja wa Ulaya na India. Baada ya mazungumzo hayo mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya biashara Bw. Peter Mandelson alisema, Umoja wa Ulaya unashikilia msimamo ule ule wa zamani kuhusu biashara ya mazao ya kilimo. Hii inamaanisha kuwa tofauti kati ya pande mbalimbali zinaendelea kuwepo, na vikwazo kwenye mazungumzo ya duru la Doha vitaendelea kuwepo kwa muda.
Licha ya Bw. Pascal Lamy kufanya mazungumzo na wajumbe wa Marekani, Umoja wa Mataifa na India, tarehe 6 pia alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Brazil Bw. Celso Amorim. Mazungumzo ya wajumbe wa nchi hizo yalisababisha ufuatiliaji mkubwa wa vyombo vya habari, na yalichukuliwa kama ni fursa nzuri ya kuondoa vikwazo kwenye mazungumzo ya duru la Doha. Matumaini hayo ya vyombo vya habari yanatokana na dalili nzuri zilizooneshwa hivi karibuni kuhusu mazungumzo ya duru la Doha. Mwanzoni mwa mwaka huu, rais George Bush wa Marekani alisema, mazungumzo ya duru la Doha yaliyokuwa yamekwama kwa zaidi ya nusu mwaka, ni lazima yarejeshwe mapema, baadaye mjumbe wa biashara wa Marekani Bi. Susan Schwab aliwasiliana na nchi za Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zinazoendelea. Mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya biashara Bw. Peter Maandelson pia alifanya juhudi kubwa katika nchi za Umoja wa Ulaya akitumai kupata maendeleo wakati Ujerumani inapokuwa mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya. Isitoshe, katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy alifanya ziara katika nchi nyingi zinazotegemea zaidi kilimo za Afrika na Asia ili kusuluhisha misimamo. Wiki mbili zilizopita, kwenye hotuba yake nchini Philippines alisema, Marekani, Umoja wa Ulaya, Japani na Korea ya Kusini, nchi ambazo zinatoza ushuru mkubwa wa mazao ya kilimo, zimekubali kupunguza ushuru wa forodha, na hata alidokeza kuwa vikwazo kuhusu mazao ya kilimo vinaweza kuondolewa mwezi Aprili na Mei, na mazungumzo ya Doha yanaweza kurejeshwa katika nusu ya kwanza ya mwaka kesho. Habari hizo zinaonesha kuwa tofauti kati ya pande mbalimbali zimepungua na kuwa karibu kufikia makubaliano. Lakini hali ilivyo ya hivi karibuni imedhihiriasha kuwa vikwazo haviwezi kuondolewa kirahisi kama inavyotazamiwa. Wakati Bw. Peter Mandelson alipozungumza na waandishi wa habari alisema kwa uchungu kuwa, ingawa mazungumzo ya duru la Doha yanainufaisha Umoja wa Ulaya, lakini kama nchi za Umoja huo hazitapiga hatua mazungumzo hayo kamwe hayatafanikiwa.
Vyombo vya habari vinaona kuwa msimamo mkali wa mjumbe wa biashara wa Umoja wa Ulaya Bw. Peter Mandelson unatokana na shinikizo kubwa kutoka Ufaransa na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zilizoendelea katika kilimo. Nchi za Ulaya ya Kaskazini, Uingereza na Ujerumani, ambazo ni nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda zinakubali kupunguza ushuru wa forodha, lakini Ufaransa, Hispania na Ureno, nchi ambazo zimeendelea zaidi katika kilimo zinashikilia sera za sasa zinazotekelezwa na Umoja wa Ulaya, hasa Ufaransa, nchi inayonufaika zaidi na sera hizo. Waziri mkuu wa Ufaransa Bw. Dominique de Villepin tarehe 5 alisema, haifai kwa Umoja wa Ulaya kulegeza masharti kabla ya nchi zinazoendelea kuzifungulia mlango nchi zilizoendelea kwa bidhaa za viwanda na biashara ya huduma. Waziri wa kilimo wa Ufaransa Bw. Dominique Bussereau aliahidi kuzuia nchi za Argentina, New Zealand, Australia na Brazil, ambazo zimekuwa nchi za viwanda na kilimo kunyakua soko la mazao ya kilimo la Umoja wa Ulaya.
Msimamo mkali wa viongozi wa Ufaransa unaonesha kuwa ni vigumu sana kwa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kusawazisha msimamo kuhusu biashara ya kilimo. Hata kama Ufaransa haitakwamisha, mazungumzo ya duru la Doha pia yatakuwa na vikwazo. Uchaguzi mkuu wa Marekani na Ufaransa umekaribia, hakuna hata kimoja kati ya vyama vyenye wagombea urais vinavyotaka kupoteza uungaji mkono wa makundi ya kilimo. Na nchi yenye maendeleo makubwa katika kilimo, Ureno, itakuwa mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya katika nusu ya pili ya mwaka huu, kusuluhisha misimamo ya nchi za Umoja huo itakuwa ni vigumu zaidi.
|