Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-06 20:24:03    
Barua 0304

cri
Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa Dubai Falme za kiarabu, ametutumia barua pepe akisema, akiwa ni msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kupitia masafa mafupi na kupitia njia ya tovuti yetu ndani ya mtandao wa Internet, angependa kuchukuwa fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa maadhimisho ya kutimia kwa mwaka mmoja tangu Radio China Kimataifa ilipofungua kituo chake cha matangazo kwa njia ya mawimbi ya FM 91.9 huko Nairobi Kenya. Anasema kwa kweli mafanikio ya Radio China Kimataifa ya kufungua kituo hicho cha kwanza cha aina hiyo duniani, kunastahili kuhesabiwa kama ni fahari kubwa kwa bara la Afrika kwa vile kituo hicho kwanza kimefunguliwa katika nchi ya Afrika.

Anasema mwaka mmoja wa kituo cha Radio China kimataifa cha huko Nairobi Kenya, unaweza kuwa ni motisha kwa mataifa mengine barani Afrika kushirikiana na Radio China Kimataifa katika kufanikisha azma yake ya kuboresha usikivu wa matangazo yake kwa wasikilizaji wake, pamoja na kujenga daraja la urafiki na udugu wa karibu zaidi baina ya Wachina na Waafrika.

Anasema kwa maoni yake binafsi anaona kuwa kuna mengi ambayo Wachina na Waafrika wataweza kunufaika kupitia njia hii ya mawasiliano ya karibu kwenye matangazo ya radio, hasa tukizingatia kwamba pande hizo mbili tayari zimeweka mikakati ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa dhati katika nyanja mbalimbali za kuliendeleza bara la Afrika kiuchumi na kimaendeleo chini ya maazimio yaliopitishwa na Mkutano wa viongozi wa Baraza Kuu la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Beijing China mwezi Novemba mwaka jana.

Hivyo ni matumaini yake kuwa juhudi za Radio China Kimataifa za kutaka kufungua vituo kama kile cha 91.9 Nairobi Kenya au kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji barani Afrika ili kuweza kupeperusha matangazo yake hewani na kuwafikia wasikilizaji kwa njia bora zaidi, hatimaye zitaweza kufanikiwa na kuzaa matunda.

Mwisho anasema angependa kutuma beti zangu chache kama ni pongezi zangu kwa maadhimisho ya mwaka mmoja wa kituo cha FM 91.9 cha Radio China huko Nairobi - Kenya.

Pongezi ninazitoa * Na nyote mwanisikia

Zawadi tuliyopewa * Mwaka umeshatimia

Kituo kufunguliwa * 91.9FM twajivunia

Nairobi walishangilia * CRI ilipofunguliwa.

Mawimbi yalio tulia * Hewani yanapepea

Wengi huwafikia * Na vyema huyasikia

Wasikilizaji wafurahia * CRI yawanogea

Nairobi walishangilia * CRI ilipofunguliwa.

Vipindi vyapokelewa * Nairobi wavifurahia

FM wakifungua * Redioni wavisikia

Kwa njia iliomuruwa * Hakika twaisifia

Nairobi walishangilia * CRI ilipofunguliwa.

CRI yashukuriwa * Juhudi imechukua

Kituo kukifungua * Wengi tunafurahia

Daima kitaenziwa * Ni kitu cha kujivunia

Nairobi walishangilia * CRI ilipofunguliwa .

Msikilizaji wetu mutanda Ayub Sharif wa Bungoma Kenya ametuandikia barua pepe akisema, ilikuwa ni furaha ilioje kwake kusoma barua pepe tuliyomwandikia. Na yeye anasema anapenda kutusalimu sote, na kutufahamisha kuwa barua pepe yetu imemtia nguvu ya kuweza kuwasiliana nasi mara kwa mara. Kwa kufanya hivyo itakuwa ni rahisi kwetu kuhakikisha urafiki wetu unaendelea milele.

Anasema pia anapenda kutoa pongezi kwa mabadiliko aliyosikia kwenye matangazo ya idhaa ya Kiswahili hasa kwenye kipindi cha salamu zenu, anasema amefurahishwa na kuongezwa kwa burudani ya muziki na namna mpya ambavyo kadi zinasomwa. Lakini pia anasema hata kipindi cha Sanduku la Barua nacho pia kiongeongezwa muda, Vilevile anasema alivutiwa sana na mahojiano kati ya mwandishi wenu wa habari Bw. Xie Yi wa huko Nairobi akimhoji mtangazaji wa KBC Bw. Jacob Mogoe, maoni yake yalimvutia sana.

Na mwisho anasema anasikitika kuwa hakuweza kupata nafasi ya kusherekea vizuri maadhimisho ya mwaka mmoja wa kituo cha FM huko Nairobi, lakini ana uhakika kuwa siku nyingine atapata fursa ya kuadhimisha siku hiyo, lakini pia anasema alifurahishwa sana na mtoto wake Fesbet, ambaye siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja wa matangazo ya CRI 91.9 FM huko Nairobi, alijigamba kwa wenzake kuwa baba yake, yaani Bw Mutanda, yeye husikiliza matangazo ya Radio China kimataifa.

Msikilizaji wetu Wabwire Namude katika barua yake ametutumia maoni matatu, kwanza anatoa shukrani kwa maandalizi bora ya vipindi na matangazo, anasema yeye anaona kila kipindi kimepangwa vizuri na kinatangazwa ipasavyo. Pili, anampongeza Bwana Mutanda Ayub Sharrif kwa kuibuka mshindi wa zawadi maalum ya kuitembelea nchi ya China, anasema kwa hakika amekuwa balozi mwema na maarufu sana. Na tatu anasema, kituo cha FM kilichopo jijini Nairobi hakisikiki kote nchini Kenya, wanaofurahia matangazo ya FM ni wasikilizaji wanaoishi Nairobi, na maeneo ya karibu, anauliza Je yeye pamoja na wasikilizaji wengine wanaoishi mbali na Nairobi ni lini wataanza kufurahia matangazo ya FM, anaimba kama kuna uwezekano hilo lishughulikiwe ili waweze kupata matangazo ya FM.

Msikilizaji wetu mwingine Bwana Edwin Otieno Owuocha, anaanza barua yake kwa salamu, na pia anasema anashukuru sana kwa barua na picha nzuri ya wanyama na ndege pamoja na historia ya Radio China kimataifa tokea 1941 hadi leo. Yeye pamoja wasikilizaji wengine wanaendelea kuwahamasisha watu wasikilize matangazo ya Radio China kimataifa . Na yeye anasema anasikitika kuona ni kwanini matangazo ya FM kutoka Nairobi hayawafikii huko Meru, lakini anatarajia kuwa siku moja matangazo yatawafikia. Mwisho anakamilisha barua yake kwa kutoa pongezi kwa upangaji wa vipindi vinavyoelimisha na vinavyohusu maendeleo ya jamii.

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim kutoka Lindi anaanza barua yake kwa kutoa salamu na pongezi kwa Radio China Kimataifa kutimiza miaka 65.Anaipongeza sana Radio China Kimataifa kwa kuwa daraja la mawasiliano kati yake na wasikilizaji kwa muda wa miaka yote hiyo 65. Anasema anakumbuka kuwa Radio China Kimataifa imepitia safari ndefu yenye kuvuka milima na mabonde kwa muda muda wote huo wa miaka 65, hadi kuwa kiungo kikubwa cha mataifa duniani kwa kuwa na vituo vya matangazo zaidi ya 30 duniani na kutangaza lugha 48 ikiwemo lugha anayozungumza ya Kiswahili.

Akiwa ni msikilizaji mkongwe kabisa wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa anawapongeza walionzisha Radio China kimataifa na wanaoindeleza, mwisho anamalizia barua yake kwa kuitakia Radio China Kimataifa maendeleo na mafanikio mema kwa muda mrefu ujao.

Na msikilizaji wetu Dominic Nduku Muhoro wa Kakamega Kenya, anaanza barua yake kwa kutoa salaam nyingi kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa, akitarajia kuwa tunaendelea kuchapa kazi kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Bwana Dominic anashukuru kwa zawadi alizotumiwa hivi karibuni zikiwemo picha ya ukuta mkuu wa China, kadi inayoonyesha kuadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwa radio China Kimataifa na zawadi nyingine. Anasema hii hatua kubwa na nzuri ya kuzidisha urafiki na ushirikiano kati ya wasikilizaji hasa wa Kakamega, ambao mwenyekiti wao Bw. Yaaqub Saidi Idambira.

Zaidi ya hayo msikilizaji wetu anasema Radio china Kimataifa imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya kisasa ya kurusha matangazo yake hewani kwa njia rahisi katika sehemu mbalimbali duniani. Hali hiyo inaifanya izidi kupata wasikilizaji wengi hasa katika bara la Afrika, ambapo klabu za wasikilizaji zimeongezeka na klabu hizo zinaendelea kutafuta wasikilizaji wengi zaidi.

Msikilizaji wetu mwingine Bwana Edwin Otieno Owuocha anapendekeza kwa idara husika za Radio China kimataifa kuchukua hatua zinazowezekana za kujenga mitambo zaidi magharibi mwa Kenya ambapo hawapati usikivu wa masafa ya FM kutoka kituoa cha Nairobi, kwa wakati huu wanatumia masafa mafupi na ya kati pekee, itakuwa vizuri kama mitambo ikajengwa katika miji kama Kisumu, Eldoret na Kakamega. Anamalizia barua yake kwa kuwapongeza wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio china kimataifa na wafanyakazi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-06